Jumanne 14 Novemba, 2017
Leo ni Jumanne 25 Safar 1439 Hijria sawa na 14 Novemba 2017.
Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita Bunge la tatu la kitaifa la Iran lilivunjwa kwa amri ya Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa silsila ya Qajari. Hatua hiyo ambayo haikuwa ya sawa ilichukuliwa baada ya Ahmad Shah kufanya mkutano na Mawaziri wa Urusi ya zamani na Uingereza. Katika wakati huo Russia na Uingereza zilikuwa zikijaribu kuishawishi Iran kushiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia dhidi ya Ujerumani.
Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India. Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.
Miaka 128 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri alizaliwa. Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa. Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri.
Katika siku kama ya leo miaka 484 iliyopita, Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania. Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu.Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa.
Katika siku kama ya leo miaka 301 iliyopita, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo. Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani.
Siku kama ya leo miaka 220 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897, alizaliwa Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na kanuni sahihi za kielimu katika masuala ya geolojia.