Nov 15, 2017 23:56 UTC
  • Alkhamisi 16 Novemba, 2017

Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Safar 1439 Hijria sawa na Novemba 16, 2017.

Miaka 37 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq. Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam. Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.

سوسنگرد

Miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Ayatullah Sayyid Abdul A'alaa Mussawi Sabzavari mmoja wa wanazuoni mashuhuri wa Iran. Ayatullah Sabzavari alizaliwa mwaka 1290 Hijria shamsia katika mji wa Sabzavar huko kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanazuoni huyo alianza masomo ya Kiislamu akiwa na umri wa miaka 14 na baadaye akaendelea na masomo hayo katika mji mtakatifu wa Mash'had Iran. Alielekea katika mji wa Najaf nchini Iraq na kunufaika na elimu ya mafunzo ya Kiislamu na katika kipindi kifupi akafikia daraja ya Ijtihad. Ayatullah Sabzavari amaeandika vitabu vingi na muhimu zaidi ni tafsiri ya Qur'ani yenye juzuu 30 ya Mawahibur Rahman.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, yaani tarehe 16 Novemba mwaka 1946, kwa mara ya kwanza ilitengenezwa mvua bandia. Mvumbuzi wa mvua hiyo aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa wa Marekani akishirikiana na mwanakemia mmoja wa nchi hiyo, walitumia gesi ya kaboni na hewa katika kutengeneza mvua hiyo. Mvua bandia hutumiwa katika maeneo yenye ukame au yenye uhaba wa mvua.

Na siku kama ya leo miaka 72 iliyopita inayosadifiana na tarehe 16 Novemba mwaka 1945, vikosi vya jeshi la Ufaransa viliishambulia Vietnam na kuanza mapambano ya muda mrefu ya wananchi kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo. Baada ya karne moja ya kukoloniwa Vietnam na Ufaransa, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Japan iliidhibiti nchi hiyo. Japan iliondoka Vietnam baada ya kushindwa katika vita hivyo, na Vietnam ikaanza kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa.

Bendera ya Vietnam