Jumatano, 22 Novemba, 2017
Leo ni Jumatano tarehe 3 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1439 Hijria sawa na tarehe 22 Novemba mwaka 2017.
Tarehe 3 Rabiul Awwal miaka 998 iliyopita alifariki dunia mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul A'laa al Maarry. Alizaliwa mwaka 363 Hijria katika Syria ya sasa na baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul A'laa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake.
Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."
Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, alizaliwa Bi. Mary Ann Evans maarufu kwa jina la George Eliot, mwandishi wa riwaya na simulizi wa Uingereza. Akiwa mtoto mdogo Evans alipendelea zaidi kusoma vitabu, na taratibu akaingia katika fani ya uandishi. Aidha akiwa kijana Evans alikuwa na misimamo mikali ya dini ya Kikristo, hata hivyo misimamo hiyo ilipungua baadaye. Akiwa na umri wa miaka 30, aliandika kitabu cha ‘Maisha ya Nabii Issa-as’ huku akiandika vitabu mbalimbali vya riwaya simulizi na kutokea kupata umaarufu mkubwa katika karne ya 19 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, kufuatia kujiri kwa Vita vya Pili vya Dunia, nchi ya Lebanon ilijipatia uhuru wake. Lebanon ilitoka katika udhibiti wa utawala wa Othmania mnamo mwaka 1918 Miladia na kudhibitiwa baadaye na Ufaransa. Mwaka 1923 Miladia Ufaransa iliikalia nchi hiyo kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Tangu wakati huo Lebanon ikaanza kushuhudia siasa za ukoloni wa Mfaransa vikiwemo vitendo vya ubaguzi na machafuko. Nchi hiyo ilijipatia uhuru wake mwaka 1943.
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 242 kuhusu Palestina. Miongoni mwa vipengee vya azimio hilo ni udharura wa kuondoka askari wa utawala ghasibu wa Israel katika ardhi zote za Palestina zilizokaliwa kwa mabavu Juni mwaka 1967 katika vita vya Waarabu na Israel, kusimamishwa operesheni za kijeshi na kutatuliwa kadhia ya wakimbizi wa Palestina kwa njia ya uadilifu. Hata hivyo kutokana na himaya ya pande zote ya Marekani na nchi za Magharibi kwa utawala ghasibu wa Israel, utawala huo haramu umekataa kutekeleza azimio hilo.
Na siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, John F. Kennedy, rais wa wakati huo wa Marekani aliuawa na raia mmoja wa nchi hiyo akiwa ziarani katika mji wa Dallas huko katika jimbo la Texas. Kennedy alizaliwa mwaka 1917 na alikuwa mwakilishi wa bunge la Marekani kwa duru tatu kuanzia mwaka 1946 na duru moja alikuwa mwakilishi wa seneti ya nchi hiyo. Siku kadhaa baadaye Lee Harvey Oswald ambaye alimuua Kennedy naye pia aliuawa na mtu aliyejulikana kwa jina la Jack Ruby na polisi ya Marekani ilidai kuwa mtu huyo vilevile aliaga dunia baadaye akiwa jela kutokana na maradhi ya saratani.