Nov 25, 2017 19:33 UTC

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 17 ya makala yanayozungumzia chuki na matukio ya kibaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla katika nchi za Magharibi.

 

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia shambulizi la kigaidi lililotokea mwezi uliopita huko mjini Las Vegsa nchini Marekani na ambalo lilifanywa na mtu mmoja kwa jina la Stephen Paddock, gaidi Mkristo. Tukakunukulieni maoni ya waandishi wa habari wa Marekani ambao walisema kuwa, lau kama gaidi huyo angekuwa ni Mwislamu, basi Marekani ingetumia hujuma hiyo kuivamia nchi anakotokea. Leo tutaendelea kujadili maoni hayo hivyo endeleeni kuwa nami hadi mwisho wa kipindi.

Chumba alichokuwa ndani yake Stephen Paddock

Kadhalika Thomas Friedman mwandishi wa gazeti la New York Times anaeleza baada ya kubainika kuwa muhusika wa shambulizi la Les Vigas  alikuwa ni Mkristo na si Mwislamu kama ilivyodhaniwa awali kwa kusema: "Hata hivyo wakati inapotokea muhusika wa shambulizi ni Mmarekani mwenye msongo wa mawazo, kwa kutumia silaha ambazo ziliidhinishwa na sheria za umiliki silaha za moto au kutokana na sheria ambazo zilitungwa na Wamarekiani wenyewe, unadhani ni hatua gani ingechukuliwa? Ninafahamu kungetokea yale yaliyotokea. kilichotokea ni rais pamoja na chama cha Republican kujaribu kulimaliza suala hilo na kisha kusisitiza kwamba halitakiwi kuchukuliwa kama la kisiasa, huku wakishindwa kuangalia upya sheria za umiliki silaha nchini humo." Friedman anailaumu serikali ya Marekani na wawakilishi wa Kongresi ya nchi hiyo kwa kurahisisha sheria ya umiliki salaha ambazo hadi sasa zimesababisha mauaji ya raia wengi wasio na hatia wa taifa hilo.

Tukio la kigaidi lililofanywa na gaidi Mkristo las vegas, Marekani

Akiashiria kukamatwa aina ya silaha 42 katika eneo alilokuwa anaishi Stephen Craig Paddock anaandika kwa kusema: "Ufisadi na mashinikizo ya lobi ya wamiliki wa mashirika ya uuzaji silaha nchini Marekani, vimewafanya watawala kushindwa kabisa kubadili sheria zinazohusiana na silaha." Mwisho wa kunukuu.

*********************************

Ndugu wasikilizaji ni vyema mfahamu kwamba kile kilichotokea Las Vegas, Marekani hakilingani hata kidogo na jinai kubwa inayotekelezwa dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar. Lakini pamoja na hayo ni kwamba tukio Las Vegas lilipewa umuhimu mkubwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi kiasi cha kushangaza tofauti kabisa na vinavyoakisi mauaji kuhusu Waislamu wa Rohingya.

Ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu huko Magharibi

Aidha takwimu zinaonyesha kuwa, Waislamu ni wahanga wakubwa wa jinai za halaiki na mauaji ya kimbari barani Ulaya, Afrika na Asia katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, huku Waislamu hao hao wakiwa ni watuhumiwa nambari moja wa vitendo vya kigaidi katika nchi hizo hizo za Magharibi. Inakuwaje wafuasi wa dini ya amani (Uislamu) ambao ndio wahanga wakubwa wa jinai na ukatili katika kipindi chote cha muongo uliopita, hii leo wawe ndio watuhumiwa wa kuenea wimbi la ugaidi na vitendo cha kuchupa mipaka? Aidha ni kwa nini mauaji na jinai wanazofanyiwa Waislamu, haziakisiwi katika ngazi za vyombo vya habari vya Kimagharibi? Na kwa nini mauaji na jinai zihusishwe tu na wafuasi wa mafundisho ya dini ya Uislamu? Majibu ya maswali haya ni kwamba yote hayo yanatokana na propaganda za kueneza chuki na ubaguzi dhidi ya dini ya Kiislamu na wafuasi wake, propaganda ambazo zinatekelezwa kwa malengo maalumu ya kujitanua madola ya Magharibi katika nchi za Kiislamu.

**********************************

Ndugu wasikilizaji mtafahamu kwamba, chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi unaongezeka huku Waislamu wakiendesha harakati za kupinga matumizi ya vitendo vya utumiaji mabavu, kuchupa mipaka na ugaidi dhidi yao.

Waislamu katika nchi za Ulaya, licha ya kuishi kwa amani lakini wanaandamwa na chuki

Gazeti la Uingereza la The Independent limetoa ripoti katika uwanja huo kwa kuandika kuwa, polisi ya Uingereza  imeripoti kesi 110 zinazotokana na chuki dhidi ya maeneo ya ibada ya Waislamu katika kipindi cha msimu wa machipuo hadi msimu wa joto mwaka huu 2017. Hii ni katika hali ambayo katika muda kama huo mwaka uliopita kuliripotiwa kesi 47 pekee. Vitendo vya udhalilishaji na ubaguzi, uharibifu na kuvunja milango ya misikiti na vitisho vya utegaji mabomu dhidi ya maeneo hayo ya ibada, ni miongoni mwa mashambulizi ambayo yanawakabili Waislamu wa mataifa hayo ya Magharibi. Aidha kuvunjwa madirisha ya misikiti, kuharibiwa magari yaliyo kando na maeneo hayo, kuandika matusi kwenye kuta za misikiti, kuwashambulia kimwili waumini wanapokuwa wakitoka au kuingia misikitini, kuchoma moto au kuweka nyama ya nguruwe katika milango ya maeneo hayo, ni miongoni  mwa mashambulizi hayo yanayowalenga Waislamu. Diane Abbott, Waziri wa Mambo ya Ndani wa serikali kivuli nchini Uingereza aliielezea ongezeko la kesi za mashambulizi dhidi ya Uislamu kuwa ya kutisha. Anasema: "Shambulizi lolote dhidi ya kundi au jamii ya kidini ya wachache, ni jambo lisilokubalika. Bila shaka mtu yeyote aliye huru anapinga mashambulizi kama hayo." Mwisho wa kunukuu.

Licha ya viongozi wa kisiasa kujifanya kutowabagua Waislamu lakini kivitendo, ndio wanachochea chuki dhidi ya Waislamu hao

Akizungumza na gazeti la The Independent Fayad Muuqaali, kiongozi wa taasisi inayojishughulisha na kuzikurubisha pamoja jamii za Uingereza amesema: "Mashirika na mitandao ya kijamii inapasa kuwajibika kwa sababu kueneza chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu, kunafungua milango ya kushambuliwa misikiti ya Waislamu. Watu na taasisi zinazoendesha kampeni ya kupinga wahajiri na Uislamu nchini Uingereza, zimeongeza sana harakati zao katika mitandao ya kijamii na kupalilia chuki dhidi ya Waislamu." Mwisho wa kunukuu. Kwa mujibu wa takwimu za polisi ya Uingereza, kila kunapojiri shambulizi la kigaidi ndipo kunapoongezeka hujuma dhidi ya misikiti na maeneo ya ibada ya Waislamu. Kwa ibara nyingine ni kwamba, makundi ya kigaidi na ukufurishaji kama vile Daesh, ni kisingizio bora kinachotumiwa na harakati za kibaguzi kwa ajili ya kuendesha mashambulizi yao dhidi ya misikiti, vituo vya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla.

*********************************

Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni Waislamu wamefanya juhudi kubwa za kueneza ujumbe wa Uislamu wa kweli katika jamii za Magharibi kupitia mafundisho bora ya Uislamu ambayo ni ya kulingania amani, uadilifu na upendo kati ya watu. Matukio ya hivi karibuni kabisa kuhusiana na suala hilo ni kukusanyika Waislamu wengi mjini Londan katika kulaani makundi ya kigaidi na yanayohusika na vitendo vya utumiaji mabavu.

Hali halisi ya Waislamu katika nchi za Magharibi

Taasisi isiyo ya kiserikali ya 'Mapambano katika Kukabiliana na Ubaguzi' iliitisha maandamano mjini London katika kulaani kimya cha wanasiasa wa mrengo wa kulia kuhusiana na vitendo vya chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu vinavyofanywa na makundi yenye kufurutu ada nchini Uingereza. Washiriki wa maandamano hayo walibeba mabango yaliyokuwa na jumbe mbalimbali za kulaani ubaguzi na chuki dhidi ya dini ya Uislamu na Waislamu kwa jumla. Suala la kufaa kuashiria hapa ni kwamba, Waislamu hawajasalia kimya juu ya mienendo na miamala hiyo ya kibaguzi dhidi yao na katika kila fursa inayopatikana hujaribu kutumia mwanya huo kueneza mafundisho halisi ya Uislamu katika jamii. Kwa mfano katika kipindi cha mwezi wa Muharram wafuasi wa Ahlu Bait wa Mtume (saw) huadhimisha kumbukumbu za mauaji ya kinyama yaliyofanywa dhidi ya mjukuu wa Mtume al-Imam Hussein (as) na watu wa famili ya Mtume (saw).

Waislamu barani Ulaya wakifanya marasimu ya kumbukumbu za kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Imam Hussein (as)

Itakumbukwa kuwa, Imam Hussein (as) aliamua kujitolea yeye na watu wa familia yake kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu ambayo ilikuwa ikipotoshwa na kundi la watu wachache ambao walikuwa wakitumia dini hii kufikia malengo yao machafu. Hii leo pia fikra za kufurutu ada na za ukatili za makundi ya kigaidi na ukufurishaji kama vile Daesh, yanafuata mienendo ile ile ya watu waliomuua Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Tangu miaka 1400 iliyopita, Waislamu na wafuasi wa watu wa familia ya Mtume (saw) katika siku ya 10 ya mwezi Muharram maarufu kwa jina la 'Siku ya Ashura' hufanya marasimu ya kumbukumbu za mauaji dhidi ya mtukufu huyo (Imam Hussein (as) sambamba na kukumbuka harakati zake katika kupambana na dhulma na udikteta wa watawala waovu. Kupitia kumbukumbu hizo, maelfu ya jumbe hutolewa kuhusiana na dini tukufu ya Uislamu. Kinyume na fikra za kufurutu ada na ugaidi za makundi ya ukufurishaji kama vile Daesh, Jab'hatu Nusra, Al-Qaidah, Taleban, ash-Shabab na Boko Haram ambayo hujihusisha tu na jinai na mauaji dhidi ya watu wasio na hatia, Uislamu ni dini inayolingania kupambana na utawala wa kidhalimu, udikteta na kuwatetea watu wanaodhulumiwa.

Kumbukumbu za kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Imam Hussein (as)

Ukweli ni kwamba, ujumbe wa Uislamu ni kulingania umoja, uhuru na uadilifu. Harakati ya Imam Hussein (as) dhidi ya utawala dhalimu wa Yazidi mwana wa Muawiya, ilisimama juu ya msingi huo. Aidha lengo kuu la Imam Hussein lilikuwa ni kuhuisha mafundisho halisi ya Mtume Muhammad (saw) ambayo yalikuwa yameanza kupotoshwa na watu wenye fikra kama za magaidi wa leo. Ni kwa msingi huo ndio maana Waislamu wakawa wanahuisha kumbukumbu za mjukuu huyo wa Mtume al-Imam Hussein (as).

Ndugu wasikilizaji sehemu ya 17 ya makala haya yanayozungumzia chuki na ubaguzi unaofanywa na viongozi na serikali za nchi za Magharibi dhidi ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla inakomea hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar. Was-Salaamu Alaykum warahmatullahi wa barakaatu…………./

 

 

 

 

Tags