Jan 02, 2018 04:12 UTC
  • Jumanne, Januari 2, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 14 Mfunguo Nane Rabiuthani 1439 Hijria sawa na Januari 2, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1373 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali bin Abi twalib a(as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Mwaka 61 Hijria Imam Hussein (as) akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi.

Miaka 152 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia. Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford. Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'.

Gilbert Murray

Katika siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia. Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana. Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii.

Isaac Asimov

Katika siku kama ya leo miaka 2 iliyopita yaani tarehe Pili Januari 2016 utawala wa Saudi Arabia ulimuua mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al Nimr. Baqir al Nimr aliyekuwa mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia wa Saudia alizaliwa tarehe 21 Juni mwaka 1959 katika mji wa Awwamiyya huko mashariki mwa Saudi Arabia. Alipata elimu ya msingi katika mji huo na mwaka 1400 Hijria yaani mwaka 1989 alielekea Tehran nchini Iran na kupata elimu katika chuo cha kidini cha Qaim kilichoasisiwa na Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi. Baada ya kupata elimu katika chuo hicho kwa kipindi cha miaka 10 Sheikh Nimr alikwenda Syria na kuendelea kutafuta elimu zaidi katika Chuo cha Kidini cha Bibi Zainab (as). Aliporejea Saudi Arabia, Sheikh Nimr aliasisi kituo cha kidini cha al Imam al Qaim katika mji wa Awwamiyya ambacho kiliweka jiwe la msingi la kuanzishwa Kitiuo cha Kiislamu hapo mwaka 2011.

Sheikh Nimr Baqir al Nimr

Mwanazuoni huyo wa Kiislamu daima alikuwa akikosoa siasa za ukandamizaji na kibaguzi za utawala wa kifalme wa Saudia na alifungwa jela mara kadhaa kutokana na kusema haki na kweli. Mara ya mwisho Sheikh Baqir Nimr alikamatwa tarehe 8 Julai mwaka 2012 katika maandamano makubwa ya Waisalmu wa Kishia ya kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud na tarehe 15 Oktoba msomi huyo wa Kiislamu alihukumiwa kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo. Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016. Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu.       

Tags