Jan 07, 2018 07:50 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (100)

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia suala la kuwa na izza, heshima na utukufu.

Tulisema kwamba, kuwa na izza, heshima na utukufu au kuwa azizi ni takwa linalofaa kwa kila mtu na ili mtu apate izza, utukufu na heshima ya kweli anapaswa kumuelekea Mwenyezi Mungu na kufungua Kitabu cha mbinguni cha Qur'ani ili kwa hatua iyo aweze kupata njia bora kabisa ya saada na heshima. 

Tulinukuu pia hadithi ya Bwana Mtume saw inayosema: Kila anayetaka kuwa mtu mwenye heshima na utukufu zaidi miongoni mwa watu na atangulize mbele taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu.

Kadhalika tulieleza kuwa, moja ya njia za kumfanya mtu awe na hadhi, heshima na utukufu ni kutokuwa mhitaji wa wengine. Tulimalizia kipindi cha juma lililopita kwa kuonyesha jinsi kukesha kwa ajili ya ibada na kumtegea Mola mlezi kulivyokuwa na mchango mkubwa katika kumletea heshima na utukufu mja wa aina hiyo..

Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 100 ya mfululizo huu kitazungumzia kiburi na jinsi ya kujiepusha na tabia hii mbaya ya kimaadili. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

 

Kiburi ni hisia ya mtu kujiona kuwa yeye ni bora kuliko watu wengine. Kiburi inajulikana pia kuwa ni hali ya kutakabari, kuwa na majivuno na kuwaona watu wengine si lolote si chochote. Hali hii huambatana na dharau. Aidha mtu ambaye amekubwa na maradhi ya kiroho ya kiburi na anataraji watu wengine wamuheshimu na kumkirimu anatambulika kwamba, ni mwenye kiburi, mwenye kujiona na mwenye sifa ya majivuno. Katika aya na hadithi mbalimbali, kiburi kimekewa mno na moto wa Jahanamu kutajwa kuwa ndio makazi na mafikio ya wenye kiburi.

Wasomi na wanazuoni wa elimu ya akhlaqi na maadili wanasema kuwa, kiburi ni aina fulani ya mtu kutojitambua vyema au kujitambua lakini kwa njia isiyo sahihi yaani kutojielewa vyema. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana maamrisho na mafundisho ya dini Tukufu ya Kiislamu yametilia mkazo mno suala la watu kujiepusha na kiburi na hali ya kujiona na kujikweza. Mtume saw ambaye ni mbora wa viumbe  amenukuliwa akiwausia watu wajiweke mbali na kiburi na kujiona bora kuuliko watu wengine kwa kusema: Jiepusheni na kiburi, kwani yumkini mja akajipamba na kiburi kiasi cha Mwenyezi Mungu kufikia kusema kuwa: Andikeni jina la mwenye kiburi na kujiona katika kundi la madhalimu. (Mizan al-Hikmah Juz 8).

Moja ya athari za kiburi ni kutakabari na kujifakharisha au kujikweza. Mtu mwenye kujiona kuwa ni bora kuliko watu wengine hutaraji ukubwa na kufanyiwa huduma kutoka kwa wengine na wakati mwingine hujiepusha kusahabiana na kuongoza na watu wengine kwa kujiona kwamba, yeye hayuko daraja moja na watu hao, seuze kukaa na kula nao pamoja. Miamala kama hii jina lake ni kutakabari na tabia hii mbaya ya kimaadili ya kujiona au kujikweza au hata kudharua watu wengine na kujiona kwamba, yeye ni bora na yuko juu zaidi yao, huharibu mahusiano ya mhusika na watu wengine katika jamii.

 

Watu wengine hujitenga na mtu mwenye kiburi kutokana na tabia yake mbaya ya kujiona na ya kuwa na majivuno mbele ya wengine huku akidharua wenzake.

Imam  Muhammad Baqir as anasema katika riwaya moja kwamba: Katika siku ya Fat’h Makka (kukombolewa Makka) Mtume saw alisimama na kuwahutubia watu. Mwanzoni mwa hotuba yake Bwana Mtume saw alimshukuru na kumhimidi Mtume Mwenyezi Mungu na kisha akasema: Nyinyi mliopo hapa, wafikishieni ujumbe huu wasiokuwepo ya kwamba, Mwenyezi Mungu katika kivuli cha Uislamu ameondoa kiburi cha ujahilia na kujiona kwa sababu ya baba, familia na ukoo.  Nyinyi mnatokana na kizazi cha Adamu na Adamu ameumbwa kwa udongo, tambueni kwamba,  hii leo mtu bora kabisa miongoni mwenu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye kumcha zaidi Allah na mwenye kumti zaidi.

Kwa muktadha huo, mtu ambaye anataka izza, heshima na awe mwenye kupendwa zaidi miongoni na watu anapaswa kuwa mnyenyekevu ili awafanye watu waongeze hamu na shauku ya kuwa na mahusiano na yeye. Mkabala wa hilo, yaani kiburi na kujiona humfanya mtu mwenye tabia hii mbaya kuwa mbali na watu yaani watu hujitenga na kuwa mbali naye.

Wakati mwingine kiburi huwa ni aina fulani ya kujihami na kujitetea. Mtu ambaye anajiona duni na dhalili na anataabika kwa hali hiyo ya uduni na udhalili hufanya juhudi za kufidia hali hiyo.

Moja ya njia ambazo mtu huyo huichagua kufidia hali yake ya kujiona dhalili na duni ni kiburi. Mtu wa aina hii hudhani kwamba, kama atawaonyesha kiburi na hali ya kujiona watu wengine, basi hali yake ya uduni na udhalili wa ndani aliyonayo, itafunikwa.

Ndio maana mtu wa aina hii daima utamuona akijikweza na kujipamba mambo kama mimi nimesoma sana, nina pesa, baba yangu fulani, mimi mtoto wa fulani, familia yetu ya fulani bin fulani, yaani daima yuko katika hali ya kujifakharisha na kujikweza. Hii ni katika hali ambayo, dhana hii si sahihi hata kidogo.

 

Mtu mwenye kiburi na hali ya kujiona huogopa sana kudhihirishwa udogo wake na ndio maana hulifunika hilo kwa kufanya kiburi na majivuno na hudhani kwamba, kwa kufanya hivyo watu watamuona kwamba, yeye ana shakhsia kubwa na mtu mwenye hadhi ya juu. Hii ni katika hali ambayo, hatua hiyo si tu kwamba, haimfanyi apate izza na heshima bali humfanya adharaulike na kuonekana mdogo na dhalili zaidi kuliko hapo awali.

Imam Ali bin Abi Twalib as anasema: Kila mwenye kuwafanyia kiburi watu, huwa dhalili na dunia baina ya watu hao.

Kwa hakika kufanya kiburi ni moja ya ishara za uchache wa akili. Watu wadogo na wasio na shakhsia, wanapopata mali kidogo au elimu au anapopata cheo fulani, basi hukumbwa na kiburi, jeuri na hali ya kutakabari na kujiona na hujiona yeye ni bora kuliko watu wengine. Kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu watoharifu (as) ambazo zinaonyesha kwamba, kadiri kiburi kinavyoingia katika nafsi ya mtu basi ni kwa kiwango hicho hicho akili yake hupungua. Katika matini za dini, Iblisi ametajwa kuwa kigezo cha kiburi na kujiona.

Imam Ali bin Abi Twalib (as) anasema katika moja ya nasaha na mawaidha yake kwamba, ….Ikiwa Mwenyezi Mungu alimfanya Iblisi kuwa duni na dhalili licha ya kuwa alimuabudu Allah kwa miaka elfu sita kwa sababu tu alifanya kiburi, je watu wengine kama watafanya kiburi na kujiona wao ni wabora kwa wengine wataingia peponi?

Aidha imenukuliwa katika nasaha za Luqman al-Hakiim akimwambia mwanawe kwamba: Ewe mwanangu! Ole wake mwenye kudhulumu na kuwa na kiburi. Vipi anajiona mkubwa na mbora hali ya kuwa ameumbwa kwa udongo na atarejea katika udongo na hajui atakwenda wapi?

Kwa nasaha hiyo ya Luqman al-Hakim kwa mwanawe ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa wiki hii msikose kujiunga nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullah Wabakaatuh.