Jan 21, 2018 10:43 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (105)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia suala la kupatana na kumaliza ugomvi baina ya watu waliohasimiana.

Tulisema kuwa, kupatana maana yake ni kuweka kando hasama na ugomvi wa hapo kabla na kuanzisha tena urafiki baada ya kuwa kumejitokeza hali ya kuhasimiana na ugomvi baina ya mtu na mtu au kundi fulani na kundi jingine. Tulibainisha kwamba, endapo watu waliogombana na kufarakana hawataweza wao wenyewe kuchukua hatua ya kuhitimisha uhasama baina yao na hivyo kufanya hali ya suluhu na mapatano kupatikana, basi watu wengine wanapaswa kuingilia kati na kumaliza mzozo na ugomvi baina ya wahusika hao.

 Tuliashiria pia kwamba, mtu ambaye amemuudhi mwenzake asiwe na matarajio kwamba, mhusika huyo atarejea haraka katika hali ya kawaida na kuonyesha huba na mapenzi kama ilivyokuwa awali kabla ya ugomvi au uhasama kujitokeza baina ya pande mbili. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 105 ya mfululizo huu kitazungumzia maudhui ya hila na udanganyifu na kukunukulieni baadhi ya hadithi kuhusiana na maudhui hii. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kusikiliza yale niliyokuandalieni kwa juma hili.

 

Alimu, msomi na mwanafalsafa mkubwa wa Kiislamu Mullah Muhammad Naraqi ameandika katika Kitabu cha Akhlaqi cha Jami’u al-Sa’adat kwamba: “Hila na udanganyifu ni miongoni mwa mambo makubwa yanayoangamiza na dhambi yake  kwa dhahiri ni kubwa zaidi ya dhambi ya kuwaudhi watu wengine. Hii ni kutokana na kuwa, katika hali hiyo, mtu wa upande wa pili kutokana na kufahamu nia mbaya ya upande mwingine huchukua tahadhari na kujilinda na mtu huyo na hata kuweza kuyazuia maudhi yanayomlenga.

Lakini mtu aliyekumbwa na mghafa, hachukui tahadhari, kwani hudhania kwamba, mfyanya hila na udanganyifu anampenda, anamuonea huruma na anaguswa na jambo lake na kwa muktadha huo hutumbukia katika mtego wa mwenye hila na hadaa ambaye amevaa vazi la urafiki na huba. Ni kwa msingi huo, ndio maana Bwana Mtume SAW anasema kuwa: Sio katika sisi yule atakayemfanyia hila Mwislamu na akampangia njama.”

Baadhi ya watu wanajidanganya na kwa kukanyanga haki za wengine kwa kutumia hila na hadaa wanajiona kuwa wao ni wajanja na watu wenye akili sana. Watu hawa wanaghafilika kwamba, mtu mjanja ni yule ambaye anajichunga na kutohadaiwa na hila za shetani na ambaye anaweza kuvuka vizingiti vya matamanio ya nafsi na hivyo kusonga mbele katika njia nyoofu akiwa amejitenga mbali kabisa na suala la kukiuka na kukanyaga haki za watu wengine. Imam Ali bin Abi Twalib AS aliwajibu watu wenye fikra finyu ambao walikuwa wakizungumzia uwezo na ujanja wa kisiasa wa Muawiya bin Abi Sufiyan ambao walikuwa wakimuona Muawiya kuwa, ni mtu mwenye akili, mjanja na mwenye kipaji na kwamba, Imam Ali hakuwa na uwezo wa kutosha wa kukabiliana naye ya  kwamba: Ninaapa kwa Mwenyezi Mungu! Kama kusingekuweko na ukuta na ngome wa uchaji Mungu, basi mimi ningekuwa mtu mjanja na mwenye akili zaidi kuliko watu wote.

Kupitia hadithi hii tunajifunza kwamba, ujanja wa Muawiya ulikuwa nje ya uchaji Mungu na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na haukuwa ukizingatia mipaka ya Allah.

MUZIKI

Katika hadithi nyingine yenye madhumuni kama hayo, Imam Ali AS amenukuliwa akisema: Kama isingelikuwa kwamba, natija ya kuwafanyia hila na hadaa watu wengine ni moto, mimi ni mjuzi zaidi wa njia ya hila kuliko mtu mwingine yeyote.

Kwa hakika hila na hadaa ni nyenzo za shetani na mambo haya yamekemewa mno katika dini Tukufu ya Kiislamu.

Mtume SAW anasema: Endapo mtu ataamka asubuhi na akawa ni mwenye kufikiria kumhadaa ndugu yake Mwislamu, basi amejiweka pamoja na ghadhabu na hasira za Mwenyezi Mungu, isipokuwa kama atatubia na kujuta. Lakini kama ataaga dunia katika fikra hii, basi atakuwa amefariki hali ya kuwa si Mwislamu. Kwa hakkika dini Tukufu ya  Kiislamu inazingatia na kulipa umuhimu mno suala la usahihi wa kifikra na uzima wa kiroho wa wanadamu. Katika hilo, Uislamu unamtaka mtu asiruhusu hata kumjia fikra ya kufanya hila na hadaa katika nafsi yake.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Kughushi na kufanya hila ni alama mbaya na zisizofaa za kiroho. 

Wapenzi wasikilizaji, mtu ambaye anafungamana na heshima na utukufu wa mwanadamu na anathamini shakhsia na utambulisho wa kibinadamu, kikawaida hapaswi kutumia hila na hadaa katika mahusiano yake na watu wengine na kutumia vibaya imani na hali ya watu kumuamini

Wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, mtu anayetumia hadaa na hila na kufanya hilo kama ndio njia ya kufikia malengo yake kimsingi huwa anajihadaa mwenyewe. Imam Ali bin Abi Twalib AS anaashiria hilo kwa kusema kuwa:

Mtu ambaye anaifanya akili kuwa wenzo wa hadaa na hila kwa wengine, kimsingi anajihadaa mwenyewe.

Hii ni kusema kuwa, mtu ambaye anatumia akili na kipaji chake kwa ajili ya kwafanyia hila watu wengine huwa anaihadaa na kuidanganya akili yake na uwezo wake. Hivyo basi mtu anapoihadaa akili yake maana yake ni kuwa ameshindwa kutumia kwa njia sahihi neema hiyo aliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Haram ya Imam Ali AS katika mji mtakatifu wa Najaf

 

Tukirejea katika vitabu vya hadithi tunakuta kuwa, kuna riwaya zinazoonyesha kwamba, mtu anayehadaa na kuwafanyia hila watu wengine ili kufikia malengo yake kimsingi hana dini. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Mwenye kuhadaa hana dini.

Kwa hakika dhambi na tabia mbaya daima na kila mahala huwa ni jambo baya na linalochukiza, hususan kama mtu ataaminiwa halafu yeye akautumia vibaya uaminifu wa mtu au watu kwake. Katika baadhi ya riwaya inaelezwa kuwa, dhambi ya kumhadaa mtu aliyekuamini inalingana na dhambi ya kukufuru na kukana Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akisema kuwa: Kumfanyia hadaa na hila mtu ambaye amekuamini na kukuona kuwa ni mkweli na mwaminifu kwake ni kufuru.

Aidha katika mafundisho ya Kiislamu watu wanatakiwa kutoshauriana na watu wenye hila na hadaa na kutowakabidhi amana zao wawahifadhie.. Kwa maana kwamba, msiwakabidhi mambo yenu muhimu ya maishani kwa watu wenye hila na hadaa. Hii ni kutokana na kuwa, kwa mujibu wa Imam Ali AS ni kuwa, mtu mwenye hila sio mwamainifu.

Mtu ambaye ana hila na hadaa katika mahusiano yake na watu wengine, Mwenyezi Mungu huzirejesha kwake hila na hadaa hizo.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nalazimika kukomea hapa kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki. Nina matumaini kwamba, mtajiunga nami tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Hadi wakati huo, ninakuegeni nikikutakieni kila la kheri katika maisha yenu ya kila siku.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.