Hadithi ya Uongofu (96)
Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu, kipindi ambacho hukujieni siku na wakati kama huu kutoka hapa Tehran, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia namna ya kudhibiti na kuzuia hasira. Tulisema kuwa, moja ya njia za kukabiliana na hasira ni kwamba, mtu anaposhikwa na hasira kama amesimama na akae, na kama amekaa basi alale na kama hasira zake hazitashuka basi na atie udhu kwa maji ya baridi au aoshe mwili wake. Aidha tulisema pia kuwa, moja ya njia na mbinu za kuzuia na kudhibiti hasira ni kujipamba kwa sifa na tabia nzuri ya subira na uvumilivu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 96 ya mfululizo huu kitazungumzia ushujaa na kubainisha jinsi sifa hii nzuri ya kimaadili ilivyotiliwa mkazo na mafundisho ya Uislamu na kueleza athari zake chanya. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki kusikiliza niliyokuandalieni kwa leo.
Miongoni mwa sifa nzuri ambazo huwa sababu na chimbuko la izza na heshima ya shakhsia ya mtu ni ushujaa. Ushujaa maana yake ni kuwa na hali ya moyo thabiti na kutoogopa kile ambacho hakipaswi kuogopwa. Imam Ali bin Abi Twalib as anasema kuhusiana na ushujaa kwamba: Ushujaa ni kutokubali madhila.
Wapenzi wasikilizaji, ushujaa ni hali ya ndani ya nafsi ambayo ipo katika ujudi na uwepo wa mwanadamu na katika istilahi ya lugha, ushujaa unaelezwa kuwa ni nguvu thabiti na imara iliyopo moyoni ambayo husimama kidete katika mazingira na wakati mgumu. Kwa hakika ushujaa una engo na uga mpana ambapo moja ya uga huu ni ushujaa wa kimwili.
Kusimama kidete na kutotetereka wakati wa kutokea matukio ya kutisha ni aina nyingine ya ushujaa. Aina nyingine ya ushujaa au mtu mtu mwingine shujaa ni yule ambaye sambamba na kuwa na nguvu hii ya kiroho, daima ni mwenye kuzuia hasira na ghadhabu kwa kutumia nguvu ya akili. Kimsingi ni shujaa ni mtu ambaye kabla ya kila kitu ni mwenye kudhibiti matakwa yake mbalimbali. Kwa maana kwamba, mtu anayeweza kudhibiti matakwa na matamanio yake anahesabiwa kuwa ni shujaa. Imam Ali bin Abi Twalib as anasema:
اَشجَعُ النّاسِ مَن غَلَبَ هَواهُ
Yaani- Shujaa zaidi miongoni mwa watu ni yule mwenye kuyashinda matamanio yake ya nafsi.
Aidha amesema pia kuwa, shujaa zaidi miongoni mwa watu ni yule ambaye wakati wa hofu akili yake ni thabiti zaidi na imara zaidi. Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu endapo mtu ataweza kujitenga mbali na dhambi na hali ya kuteleza katika sheria za Mwenyezi Mungu na akadumu katika hilo, basi huyo anahesabiwa kuwa ni shujaa.
Neno ushujaa halijatajwa katika Qur'ani lakini madhumuni ya baadhi ya aya yanabainisha na kuweka wazi sifa hii nzuri ya ukamilifu wa kinafsi. Kwa mfano aya ya 173 katika Surat al-Imran Mwenyezi Mungu anasema:
Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa.
Mwishoni mwa vita vya Uhud, jeshi lililopata ushindi la Abu Sufiyan ambalo lilikuwa likielekea Makka, mara lilibadilisha uamuzi na kukata shauri kuwashambulia tena Waislamu ili liliwamalizie waliobakia. Habari hiyo ikamfikia Bwana Mtume saw na mara moja akawaita Waislamu kwa ajili ya kushiriki katika vita vingine. Majeruhi wote wa Vita vya Uhud nao wakawa wamejiandaa kikamilifu kwa ajili ya vita hivyo na kusema kwamba: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa.
Ni kutokana na ushujaa huo, jeshi la Mushirikina liliamua kuachana na uamuzi wake wa kutaka kuingia vitani tena na Waislamu na likarejea Makka. Katika kuwasifia Waumini Mwenyezi Mungu anasema katika Aya tulizotangulia kuzisoma ya kwamba:
(Wao ni wale) Walio ambiwa na watu: Kuna watu wamekukusanyikieni, waogopeni! Hayo yakawazidishia Imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha, naye ni mbora wa kutegemewa.
Kwa hakika katika tukio hilo la Vita vya Uhud, ushujaa huo wa Waislamu sio tu kwamba, ulizuia kushindwa kukubwa na hatari Waislamu, bali kuliweka jiwe la msingi la ushindi wa baadaye na ukaondoa athari hasi za kushindwa katika nyoyo za wenzao na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu waumini hao wakawa wamewasha taa ya matumaini katika nyoyo za watu. Katika lugha ushujaa kinyume chake ni woga, hawafu na kitete. Sifa ya woga au ukunguru ni miongoni mwa sifa mbaya ambazo mtu anapaswa kujiepusha nazo kwani huwa na athari hasi hata kwa watu wengine.
Ndio maana Bwana Mtume saw alikuwa akitoa amri kwa watu waoga kutoshiriki katika vita vya Kiislamu, ili wasije wakawa chanzo cha kudhoofisha moyo na ari ya watu wengine. Alikuwa akisema: Mtu ambaye anahisi kuwa na woga na kitete asishiriki katika vita.
Mitume, Maimamu, mawalii wa Mwenyezi Mungu na wafuasi wao wa kweli walikuwa wakihesabiwa kuwa watu mashujaa kabisa katika zama zao na walikuwa manguli wakubwa wa muqawama, ujasiri na kusimama kidete kwa ajili ya kuitetea haki na kuhakikisha kwamba, inabakia na kudumu. Mmoja wa mashujaa hao ni Imam Ali bin Abi Twalib as ambaye ametajwa katika hadithi nyingi na Bwana Mtume saw kwamba, alikuwa mtu shujaa, jasiri na nguli asiye na mithili katika kukabiliana na makafiri na maadui wa Uislamu na hakuwa akitetereka hata kidogo katika kuitetea haki na dini ya Mwenyezi Mungu. Imam Ali anajulikana pia kwa lakabu yake mashuhuri ya Simba wa Mwenyezi Mungu mwenye kushinda.
**************
Tukio kubwa kabisa la Vita vya Khandaq ni ushahidi tosha kabisa wa ushujaa usio na kifani wa Imam Ali bin Abi Twalib. Katika tukio hilo na kwa amri ya Mtume saw, Imam Ali alijitokeza kubariziana na kupambana na Amr Ibn Abd al-Wud aliyekuwa shujaa zaidi na nguli wa maadui katika vita. Imam Ali alimshinda shujaa huyo wa makafiri.
Mtume saw aliusifia na kuutaja kwa maneno ya thamani kubwa ushindi huo wa Imam Ali as uliotokana na ushujaa na Imani thabiti aliyokuwa nayo.
Alisema: "Pigo la Ali la siku ya Khandaq ni bora kuliko amali za watu na majini."
Katika hadithi nyingine Bwana Mtume saw amenukuliwa akisema kwamba: Ninaapa kwa ambaye uhai wangu uko katika mamlaka yake, kama amali za maswahaba wote wa Muhammad mpaka Siku ya Kiyama zitakuwa katika upande mmoja wa mizani na huu ushujaa wa Ali ukawa upande wa pili wa mizani, basi thamani ya ushujaa na ujasiri wa Ali una uzito zaidi kuliko amali zote za wafuasi wa Muhammad.
Aidha imenukuliwa katika vitabu vya historia kwamba, kila mara Mtume saw alipokuwa akitaka kuwatisha makafiri na kuleta hofu na wahaka katika nyoyo zao alikuwa akiwatishia uwepo wa Ali. Alikuwa akiwaambia, endapo mtakataa kutii amri na mkaasi, basi nitamtumwa kwenu Ali as.
Kadhalika imenukuliwa kwamba, Bwana mmoja alimuuliza Imam Ali bin Abi Twalib as kwamba, kwa nini wewe huna farasi mwenye kasi ili umtumie katika vita? Imam akamjibu kwa kumwambia, mimi sihitajii farasi mwenye kukimbia kwa kasi, kwa sababu hakuna wakati ambao ninakimbia mashambulio ya adui, yaani si mwenye kukimbia kutoka vitani, na kila mara ninapomshambulia adui yeye ndiye ambaye hukimbia na anapokimbia mimi huwa simkimbizi.
Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa tukutane tena wiki ijayo, asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.