Jan 24, 2018 13:33 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (106)

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia maudhui ya hila na udanganyifu.

Tulisema kuwa, baadhi ya watu wanajidanganya na kwa kukanyanga haki za wengine kwa kutumia hila na hadaa wanajiona kuwa wao ni wajanja na watu wenye akili sana. Watu hawa wanaghafilika kwamba, mtu mjanja ni yule ambaye anajichunga na kutohadaiwa na hila za shetani na ambaye anaweza kuvuka vizingiti vya matamanio ya nafsi na hivyo kusonga mbele katika njia nyoofu akiwa amejitenga mbali kabisa na suala la kukiuka na kukanyaga haki za watu wengine. Tulibainisha pia kwamba, wataalamu wa mambo wanaamini kuwa, mtu anayetumia hadaa na hila na kufanya hilo kama ndio njia ya kufikia malengo yake kimsingi huwa anajihadaa mwenyewe na hata kuna hadithi nyingi zinazobainisha hilo. Kipindi chetu cha juma hili ambacho ni sehemu ya 106 ya mfululizo huu kitazungumzia maudhui ya haraka na kufanya mambo kwa pupa na papara na kukunukulieni baadhi ya hadithi kuhusiana na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho. Karibuni.

Kwa hakika pupa au tutuo ni nia ya mtu kutaka kumaliza au kufikia mwisho wa jambo kwa haraka bila ya umakini. Wakati mwingine hali hiyo inafahamika pia kama ni kukosa subira na uvumilivu katika kufanya jambo. Pupa na papara au tutuo inatajwa katika vitabu vya maadili ya Kiislamu kama ni haraka na kutokuwa na utulivu katika kufanya mambo. Pupa na haraka humfanya mtu aifanye kazi ambayo kimsingi mazingira yake ya kuifanya bado hayajatimia au bado hayajaandaliwa. Kufanya hivyo ni sawa na kuchuma tunda ambalo bado halijaiva. Au kupanda mbegu za zao fulani kabla ya kuiandaa ardhi husika, matokeo yake ni kuiangamiza bure bilashi mbegu yenyewe.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuwa: Jiepushe na haraka na kufanya mambo kabla ya kufika muda wake, na usizembee kufanya mambo kwa wakati munasibu na unaofaa.

 

Waswahili wana msemo na methali mashuhuri inayosema, haraka haraka haina baraka. Methali hii inaonyesha ni kwa namna gani suala la kufanya mambo kwa haraka na pupa lisivyokuwa na matokeo mazuri. Haraka na pupa ni jambo lenye taathira hasi, na muhimu kuliko yote ni kwamba, huongeza uwezekano wa kukosea na kufanya kosa katika kazi anayoifanya mtu. Kwa maana kwamba, kazi unayoifanya kwa haraka na papara uwezekano wa kukosea ni mkubwa zaidi ikilinganishwa na kazi unayoifanya kwa utulivu na polepole. Kazi ambayo mtu anaifanya kwa utulivu na upole huwa na umakini ndani yake ikilinganishwa na kazi inayofanywa kwa pupa na haraka. Wakati mwingine kufanya mambo kwa haraka hufuatiwa na hasara. Katika aya ya 11 ya Surat al-Israa Mwenyezi Mungu anabainisha kwamba, sababu ya mtu kukosea au kushindwa kutambua jambo lenye faida ni haraka na pupa. Kwani katika hali hiyo mtu hushindwa kufahamu jambo lenye faida na yeye kutokana na haraka na pupa aliyonayo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Mwenyezi Mungu anatahadharisha jambo. Aya hiyo inasema:

Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa.

Wafasiri wa Qur'ani wanaamini kwamba, daima mwanadamu ni mwenye pupa na haraka na kwa kuwa mwanadamu ni mwenye pupa katika mambo, huona shari na kheri yake katika hali moja na hufanya haraka na pupa kwa ajili ya mawili hayo. Ni katika mazingira hayo ndipo mhusika anapokosea njia na kushindwa kufikia katika lengo maridhawa na matulubu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Mtume saw anaitaja haraka na pupa kwamba, ni sababu ya kuangamia mtu na anasema:  Kwa hakika watu wameangamizwa na pupa na haraka, laiti wangejitenga mbali na pupa na haraka asingeangamia mtu.

Wapenzi wasikilizaji, moja ya sifa za kimaadili na mbinu za shetani kwa ajili ya kuwahadaa watu ni haraka na pupa katika mambo. Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, pupa na haraka katika mambo inatoka kwa shetani na utulivu katika kazi unatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kazi ya shetani ni kumfanya mtu afanye mambo kwa haraka na nafsi ya mwanadamu nayo imegubikwa na kufanya mambo kwa haraka. Kwa msingi huo adui wa nje yaani shetani na adui wa ndani yaani nafsi, hushirikiana kwa ajili ya kumpotosha mwanadamu huyu. Kwa hakika endapo mwanadamu atafanya jambo kwa pupa na haraka, uwezekano wa mtu huyu kufanya jambo husika kwa usahihi huondoka na hivyo kuelekea katika mkondo usio sahihi.

Kupenda jambo fulani kupita kiasi, kutazama mambo kijujuu na kutawaliwa mwanadamu na matamanio ya nafsi, kila mojawapo kwa nafasi yake linahesabiwa kuwa linaweza kuwa sababu ya kufanya mambo kwa pupa na haraka. Kuwa na haraka na pupa katika kununua na kuuza, muamala na biashara ya nyumba au gari au katika suala muhimu la ndoa au katika kuchagua mshirika wa biashara, ni hatua ambayo yumkini ikamletea mhusika matatizo mengi na hasara ambazo pengine haitoweza kufidika tena. Hii ni kutokana na kuwa, uchunguzi wa kijujuu na usio na umakini, haraka na pupa katika jambo halimpi fursa mtu ya kudhihirika ukweli na uhakika wa jambo lenyewe.

Aghalabu ya hatua zinazochukuliwa bila kutaamali na kutafakari kwa umakini au kwa pupa na haraka huwa chimbuko la mtu kukwama na kukumbwa na matatizo. Imam Ali bin Abi Twalib AS analitambua suala la pupa na haraka kwamba, linaambatana na kutotumia hekima na busara.  Imam Jawad AS anasema kuwa, vitu vitatu kama mtu atavichunga hatajuta. Cha kwanza kati ya vitatu hivyo ni kujiepusha na haraka na pupa.

Kikawaida kufanya mambo kwa haraka na pupa inahesabiwa kuwa miongoni mwa tabia zisizofaa. Hata hivyo tunapaswa kuashiria nukta hii kwamba, kuna tofauti kubwa baina ya kuharakisha na kutochelewesha kufanya jambo la kheri na pupa na tutuo katika kufanya mambo. Hii ina maana kwamba, pupa na papara au tutuo au kwa maneno mengine haraka ambayo ni mbaya na isiyofaa ni ile ya kufanya jambo au kazi fulani bila ya kuchunguza pande za kazi yenyewe. Lakini pindi mtu anapokuwa ameshafanya uchunguzi na utafiti wa kila engo ya kazi husika na kupima kona zake zote kwa maana ya madhara na faida zake na akaona kwamba, kuna manufaa basi katika mazingira haya mtu hapaswi kusita hata kidogo kuifanya kazi hiyo. Bali anatakiwa kuharakisha na kutoichelewesha kazi husika au jambo hilo. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 33 ya Surat al-Imran kwamba:

 

"Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu.

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anawataka watu wayakimbilie na kuyaharakishia maghfira Yake. Aya hii inaonyesha kuwa, si kila haraka ni yenye kuchukiza, la hasha, bali kuna baadhi ya mambo ni lazima na wajibu mtu kuyaharakia na kulifanya hilo pasina kuchelewa wala kusita.

Aidha kuna hadithi nyingi zinazowataka Waumini kuharakisha katika kufanya mambo ya kheri. Mtume saw amenukuliwa akisema: Mwenyezi Mungu anapenda amali njema ambayo inafanywa kwa haraka yaani bila kucheleweshwa.

Kuna wakati mtu anataka kufanya jambo la kheri lakini kutokana kuchelewesha au kuwajulisha marafiki zake, ndugu, watoto au watu ambao hawana hamu na shauku sana ya kufanya mambo ya kheri, mtu huyu hukumbwa na hali ya hatihati na kusitasita na kuwa baina ya aifanye kazi hiyo ya kheri au aiache. Matokeo yake hushindwa kuifanya amali hiyo ya kheri.

Imam Ja'afa Swadiq AS amenukuliwa akisema maneno yaliyojaa hekima kwamba: Mtu ambaye amekata shauri kufanya jambo la kheri anapaswa kuharakisha, kwani kila kazi inayocheleweshwa, shetani hutia hila ndani yake. Aidha anasema: Baba yangu Imam Muhammad Baqir AS amesema:  Kila unapoazimia kufanya jambo zuri, basi harakisha kufanya hivyo, kwani hujui nini kitatokea baadaye.

Kwa leo tunakomea hapa kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki. Tukutane tena wiki ijayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.