Aya na Hadithi (13)
Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 13 ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambapo kwa leo tutazungumzia baadhi ya maandiko matakatifu ambayo yanatuongoza kutambua baadhi ya miungu hatari na ya uongo inayomchuikiza zaidi Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kuna Aya nyingi ambazo zimetahadharisha wanadamu dhidi ya kuiabudu miungu hiyo ikiwemo aya ya 23 ya Surat al-Jaathiya ambayo inasema: Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, na Mwenyezi Mungu akamwacha apotee pamoja na kuwa ana ujuzi, na akapiga muhuri juu ya masikio yake, na moyo wake, na akambandika vitanga machoni mwake? Basi nani atamwongoza huyo baada ya Mwenyezi Mungu? Hamkumbuki?
Wapenzi wasikilizaji, kusudio la mwanadamu kufanya matamanio yake kuwa mungu wake ni yeye kufuata hawaa na matamanio yake bila kuzingatia mipaka yoyote kinyume kabisa na anavyomuamuru Mwenyezi Mungu na akaili yake iliyo salama. Mwanadamu kufadhilisha hawaa yake juu ya mapenzi na maamrisho ya Muumba wake mwenye busara, humpelekea kufanya kila linalowezekana kuridhisha matamanio hayo na mwishowe kuidhulumu nafsi yake kwa sababu huitumbukiza kwenye giza la matamanio na dhulma na wakati huohuo kuwadhulumu wenzake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuiridhisha nafsi hakuna mpaka kama tunavyoshuhudia wenyewe katika maisha yetu ya kila siku. Kwa kuzingatia hilo, mwanadamu anayetii na kuabudu matamanio yake huitumbukiza nafsi yake kwenye ufisadi na kueneza dhulma duniani kwa kuwadhulumu wenzake. Kutokana na kuwa Mwenyezi Mungu ni Mrehemevu kwa waja wake na asiyeridhia ufisadi, dhulma na kuudhiwa waja wake, hivyo matamanio na hawaa ni miungu mibaya zaidi inayoabudiwa kinyume na ibada sahili na halisi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na suala hilo, Allama Tabatabai katika kufasiri kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake, ananukuu katika Tasiri yake ya al-Mizan kauli ya Mtume (saw) inayosema kwamba hakuna mungu yoyote anayeabudiwa ardhini na wanadamu anayemchukiza zaidi Mwenyezi Mungu kama matamanio yanayofuatwa (kuabudiwa). Kuna Riwaya nyingine inayofanana na hii inayosema kuwa hakuna mungu yoyote anayeabudiwa kinyume na Mwenyezi Mungu anayemchukiza zaidi kama matamanio yanayofuatwa (kufanywa kuwa mungu).

Sheikh al-Barqi amenukuu katika kitabu chake cha al-Mahasin, Hadithi ya Mtume (saw) inayosema: 'Kuna mambo matatu yanayookoa na matatu yanayoangamiza. Wakasema: Ni yapi hayo yanayookoa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?! Akasema (saw): Kumuogopa Mwenyezi Mungu kwenye siri (faragha) ni kana kwamba unamwona, na kama haumwoni bila shaka Yeye anakuona, uadilifu kwenye ridhaa na ghadhabu na uwastani (kutovuka mpaka) kwenye utajiri na umasikini. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Basi ni yapi yanayoangamiza? Akasema (saw) matamanio yanayofuatwa, bakhili anayetiiwa na mtu anayejigamba (kujivuna).
Wapenzi wasikilizaji, kufuata matamanio na kuyafanya mungu kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu ni sababu kuu ya mwanadamu kupotea njia na kutonufaika na mwongozo wa Mungu Muumba. Hili ndilo jambo linaloashiriwa na Hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Uddatu ad-Dai ambapo Imam Baqir (as) amepokelewa akimnukuu Mtume (saw) kwamba Mwenyezi Mungu aliye Mtukufu amesema kuwa mja hafuati hawaa na matamanio yake kinyume na matakwa ya Mwenyezi Mungu ila huvuruga mambo yake, kuacha dunia imdhibiti na kushughulisha moyo wake na kutompa duniani kile alichomkadaria. Na Mja hafuati matakwa ya Mwenyezi Mungu na kuacha kufauata matamanio yake ila Malaika Wake humlinda na kuziamuru mbingu na ardhi zimdhaminie riziki yake na Mwenyezi Mungu mwenyewe kuwa nyuma ya kila biashara anayofanya na kila mfanyabiashara na dunia kumjia hali ya kuwa imenyenyekea.
Na ibada ya mwanadamu kwa matamanio yake kinyume na Mwenyezi Mungu kwa hakika ina maana ya kumuabudu shetani na kutumbukia kwenye mtego wake pamoja na kubadilika kwake kuwa chombo kinachotumiwa kwa ajili ya kueneza ufisadi kama anavyoashiria suala hilo Imam Ali (as) katika moja ya hotuba zake katika Nahjul Balagha kwa kusema: Enyi Watu! Hakika chanzo cha kutokea fitina ni kuendekeza na kufuata matamanio, na hukumu kuzushwa. Humo Kitabu cha Mwenyezi Mungu huendwa kinyume, kwa hilo watu wanasaidiana wao kwa wao, kinyume na Dini ya Mwenyezi Mungu. Lau batili ingekuwa tupu bila ya kuchanganyika na haki isingefichika kwa wenye kuitafuta, na lau haki ingekuwa imeepukana na kuvikwa na batili, ndimi za wapinzani zingekatika. Lakini huchukuliwa kutoka huku fumba (kicha cha majani) na huku fumba na kuchanganywa. Hapo Shetani huwashinda rafiki zake, wataokoka wale waliotunukiwa wema kutoka kwa Mwenyezi Mungu hapo kabla.

Na wale waliotunukiwa wema kutoka kwa Mwenyezi Mungu bila shaka ni wale ambao huepuka kumuabudu mungu huyu na matamanio yao na daima kumuomba Mwenyezi Mungu awaepushe ibada hiyo na kuwaonyesha njia ya haki. Sayyid Ibn Tawous anasema katika kitabu cha Falah as-Sail: 'Ni muhimu pia baada ya swala ya mwisho ya Ishaa kusoma dua maalumu iliyoainishwa kwa ajili ya faradhi hii kati ya dua za Maulana a-Swadiq (as) na ambayo imepokelewa na Muawiyya bin Ammar, ambayo husomwa baada ya swala nayo ni: Bismillahir Rahmaanir Raheem. Allahumma! Mswalie Muhammad na Aali Muhammad, swala ambayo itatufikisha kwenye ridhaa yako na Pepo na kutuokoa kutokana na ghadhabu na Moto. Allahumma! Mswalie Muhammad na Aali Muhammad na nionyeshe haki kuwa haki ili nipate kuifuata na batili kuwa batili ili nipate kuiepuka. Ijaalie hawaa yangu ifuate ridhaa na utiifu wako, na jichukulie ridhaa kutoka katika nafsi yangu. Kwa idhini yako, niongoze kwenye yale yaliyochanganyika na haki, hakika Wewe unamuongoza unayempenda kwenye njia iliyo nyooka.'
Tunakushukuruni nyote wapenzi wasikilizaji, kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho mmekisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atakabali dua na amali zenu…Amin, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.