Mar 23, 2018 02:17 UTC
  • Ijumaa, tarehe 23 Machi, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 5 Rajab 139 Hijria sawa na Machi 23, 2018.

Tarehe 5 Rajab miaka 1195 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Bani Abbas kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW) jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na kwa sababu hiyo alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik."

Siku kama ya leo miaka 366 iliyopita, yaani sawa tarehe 23 Machi mwaka 1652, yalianza shambulizi la manowari za kijeshi za Uingereza dhidi ya majeshi ya Uholanzi. Amri ya shambulizi hilo ilitolewa na Oliver Cromwell aliyekuwa dikteta wa wakati huo wa Uingereza. Akipata uungaji mkono wa Bunge la Uingereza, Cromwell alimpindua mfalme wa Uingereza na kisha kulivunja bunge la nchi hiyo. Inasemekana kuwa, lengo la kutekeleza shambulio hilo lilikuwa ni kulimaliza nguvu jeshi la Uholanzi ambalo lilikuwa na nguvu kubwa ya majini.

Oliver Cromwell

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita, ilianzishwa harakati ya Ufashisti nchini Italia kwa uongozi wa Benito Mussolini. Ufashisti kwa ujumla ni utawala wa kidikteta wenye kufuata aidolojia ya kibaguzi na kiutaifa, kuwakandamiza wapinzani, kuondoa uhuru na kuzipotosha itikadi na fikra za wananchi. Hayo yalijiri baada ya Mussolini kunyakuwa wadhifa wa uwaziri mkuu nchini Italia, mwaka 1922 na kuanza duru ya udikteta nchini humo. Muda mfupi baadaye Mussolini alishirikiana na Adolph Hitler, na kuandaa mazingira ya kuanzishwa Vita vya Pili vya Dunia.

Benito Mussolini

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, liliasisiwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani 'WMO'. Shirika hilo linafungamana na Umoja wa Mataifa na taasisi zote za hali ya hewa ulimwenguni hushirikiana na shirika hilo. Miongoni mwa malengo ya kuanzishwa shirika hilo ni kutoa msaada wa elimu ya hali ya hewa kwa wataalamu wa anga, mabaharia, wakulima na shughuli nyingine za kibinadamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana siku ya leo yaani tarehe 23 Machi ikajulikana kuwa Siku ya Hali ya Hewa Duniani.

WMO

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, sawa na tarehe 3 Farvardin 1384 Hijria Shamsia, alifariki dunia Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani, mwanafalsafa na mwanafikra wa Kiislamu baada ya kuugua kwa muda mrefu. Allamah Ashtiyani alizaliwa Ashtiyan katikati mwa Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum na kupata elimu kwa wanachuoni wakubwa kama vile Imam Ruhullah Khomeini, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai. Baadaye alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na kujishughulisha na kulea wanafunzi hadi mwisho wa uhai wake.

Allamah Sayyid Jalaluddin Ashtiyani