Hadithi ya Uongofu (111)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfulluizo huu wa Hadithi ya Uongofu.
Kipindi hiki hujadili maudhui mbalimbali za kijamii, kisiasa, kimaadili, kidini na kadhalika na kukunukulieni hadithi na miongozo ya Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu AS. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia tabia mbaya ya kusema uongo. Tulisema kuwa, kusema uongo ni katika aibu na mapungufu mabaya kabisa na ni katika madhambi makubwa kabisa.
Uongo kwa hakika ni chimbuko la mambo mengi machafu na mabaya. Katika mafundisho ya Kiislamu uongo au kusema uongo kunatajwa kuwa chimbuko la machafu mengi. Miongoni mwa hadithi tulizokunukulieni katika kipindi cha juma lililopita ni ile ya Imam Hassan Askary AS ambaye amenukuliwa akisema: Uongo ni ufunguo wa kila shari.
Tulieleza pia kwamba, uongo ni katika madhambi ambayo yameharamishwa katika dini zote za Mwenyezi Mungu na kuhesabiwa kuwa miongoni mwa dhambi chafu na mbaya kabisa. Aidha tulisema kwamba, kula yamini au kiapo ni katika mbinu zinazotumiwa kwa ajili ya kuwafanya wanajamii wengine wamuamini mtu. Hata hivyo baadhi ya watu hasa waongo hutumia suala la halafa na kiapo kama ilivyo kwa jambo jingine tukufu kama wenzo wa kuwahadaa watu wengine. Hii ni katika hali ambayo, Mwenyezi Mungu amewaonya na kuwatahadharisha waumini na jamii za mwanadamu kwamba, wasiyafnye matukufu kama Allah na kiapo kama kitu cha kufikia malengo yao ya kidunia.
Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 111 ya mfululizo huu, kitazungumzia uongo ambao sio haramu nao ni uongo wenye maslahi. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chake ili muweze kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa juma hili. Karibuni.
Baadhi ya matendo asili na dhati yake ni mabaya na yasiyofaa. Kwa mfano dhulma na kuwakandamiza watu wengine ni jambo baya katika mazingira yoyote yale. Kwa maana kwamba, mwanadamu haruhusiwi kutenda dhulma kwa namna yoyote ile, hata kama anayemtendea dhulma atakuwa ni adui wa dini ya Mwenyezi Mungu. Lakini kuna baadhi ya matendo mengine kama kusema uongo, ambayo huwa haramu katika mazingira mahususi na maalumu.
Katika baadhi ya mazingira uongo si tu kwamba, ni jambo linalofaa, bali la kupendeza na hata kuwa ni wajibu na lazima. Imam Ja’afar Muhammad Swadiq AS anasema: Uongo ni jambo baya, isipokuwa kama (uongo huo) utakuwa kwa ajili ya kuondoa shari ya dhalimu na kuleta suluhu baina ya watu. Mtume Muhammad SAW amesema: Kwa hakika Mwenyezi Mungu anapenda uongo ambao uko katika njia ya urekebishaji na anachukia maneno ya ukweli ambayo hupelekea kutokea ufisadi. Imam Ali bin Mussa al-Ridha AS anazungumzia uongo wenye maslahi kwa kusema:
Kwa hakika mtu ambaye anasema maneno ya kweli na kwa maneno hayo anamtumbukiza katika matatizo ndugu yake Mwislamu, mbele ya Mwenyezi anahesabiwa kuwa miongoni mwa waongo; na hakika mtu ambaye anasema neno la uongo kuhusu ndugu yake Mwislamu na kwa neno hilo la uongo anamuepusha ndugu yake huyo na madhara, mbele ya Mwenyezi Mungu anahesabiwa kuwa miongobni mwa wakweli.
Baadhi ya watu wanakosea kwa kudhani kwamba, kigezo cha idhini ya kusema uongo ni maslahi na madhara kwao. Kwa muktadha huo, kila mahala wanapoona maslahi yao yapo hatarini wanaweza kusema uongo kwa wepesi kabisa.
Siku moja Imam Mussa al-Kadhim AS alimuusia na kumuwaidhi Hisham bin al-Hakam aliyekuwa msomi wa elimu za akili na mmoja wa masahaba wa Imam Ja’afar Swadiq AS kwa kumwambia: Ewe Hisham! Mwenye akili katu hasemi uongo hata kama maslahi yatakuwa katika uongo wake.
Kwa msingi huo basi, tunapaswa kufahamu kwamba, mtu anaruhusiwa kusema uongo katika mazingira maalumu ambapo kuna maslahi muhimu kama vile kuokoa roho na maisha au kulinda heshima ya Muumini katika masuala nyeti na vile vile kuondoa fitina na ufisadi.
Tukirejea vitabu vya hadithi tunaona kwamba kusema uongo kwa ajili ya kuokoa maisha ya nduguyo Mwislamu ni jambo ambalo limeruhusiwa na bali ni wajibu. Mtume saw amenukuliwa kuhusiana na maudhui hii akisema:
Ninaapa kwa Mola, sema uongo ili umuokoe ndugu yako na kifo. Kwa upande wake Imam Swadiq AS anasema: Endapo mtu ataapa kiapo na halafa ya uongo kwa dharura na kulazimika, hakuna tatizo katika hilo. Katika kubainisha zaidi maudhui hii, Imam huyo wa Sita katika mlolongo wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume saw anasema: Kiujumla, kila haramu katika dharura huwa halali.
Hivyo basi wapenzi wasikilizaji, katika Uislamu uongo ni jambo linalochukiza hata kama ni kwa ajili ya maslahi muhimu, lakini uongo umeruhisiwa katika mazingira maalumu.
Katika mazingira ambayo mtu anaweza kusema uongo wenye maslahi ni pale watu wawili wanapokuwa wamegombana na kuhasimiana na wakawa na chuki na kinyongo baina yao, hali ambayo imepelekea kukatika uhusiano kati ya wawili hao. Katika mazingira kama haya ili kuleta suluhu, mapatano na maridhiano mtu anaweza kusema uongo.
Yaani kusema mambo ambayo ni ya uongo lakini yanayolenga kuondoa ugomvi na uhasama baina ya wawili hao na kuandaa mazingira ya wao kupatana na kurejesha tena uhusiano wao. Kwa utaratibu huo, mtu anaweza kwenda kwa mmoja wa wagomvi hao na kumwambia kwamba: Fulani anakutaja kwa wema na anakusifia sana kwa tabia nzuri na kwamba anasononeka na kusikitika mno kwamba, kwa nini amegombana na kununiana na wewe. Nilivyomuona mimi naona ana hamu na shauku ya kupata na wewe.
Aidha akiondoka hapo, aende kwa yule mwingine na kumwambia maneno yale yale. Hali hii itamfanya kila mmoja awe na mtazamo mzuri na chanya na mwenzake na hivyo kuandaa mazingira ya wawili hao kupatana na kusahau ugomvi wao. Uongo kama huu kwa hakika sio tu kwamba, sio haramu, bali ni wenye kufaa.
Katika wasia wake kwa Imam Ali AS, Bwana Mtume saw anasema: Ewe Ali! Mwenyezi Mungu anapenda uongo ambao ni sababu ya kuleta mapatano baina ya watu na anachukia ukweli ambao unapelekea kutokea fitina na nifaki.
Katika hadithi hii Mtume saw anataka kutuonyesha kwamba, hata suala la ukweli kuna wakati mtu hapaswi kusema ukweli ili kulinda maslahi fulani na kuna wakati mtu anapaswa kusema uongo ili kuzuia kutokea fitina baina ya mtu na mtu au kundi Fulani na kundi jingine.
Wapenzi wasikilizaji, muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, msisite kujiunga nami juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu ambapo tutajadili suala la kutoa ushahidi wa uongo.
Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.
Na Salum Bendera