Jumatano, 4 Aprili, 2018
Leo ni Jumatano tarehe 17 Rajab 1439 Hijria inayosadifiana na 4 Aprili, 2018.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita Zulfiqar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa. Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971. Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kwa kufanya mauaji na kuisaliti Pakistan. Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhutto alinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe.
Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo Martin Luther King kiongoziwa mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana. Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadae akaanza kuongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani. Katika kipindi hicho raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiwatambua wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.
Na siku kama hii ya leo miaka 58 iliyopita Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 Miladia na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic huku ikipakana na Mauritania, Mali na Guinea Bissau.