Apr 17, 2018 09:59 UTC
  • Aya na Hadithi (21)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba mko tayari kusikiliza sehemu hii ya 21 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Aya na Hadithi ambavyo bila shaka vinatunufaisha sote kwa pamoja kutokana na masuala tofauti yanayochambuliwa na kujadiliwa humu.

Hivyo basi karibuni tusikilize kwa pamoja yale tuliyokuandalieni kwa juma hili ambapo kwanza tutaanza kwa kusikiliza kwa makini Aya kadhaa zifuatazo ambazo zinatuongoza katika kujua na kutambua vyema utambulisho wa wale watu walioruhusiwa na Mwenyezi Mungu kupigana Jihadi, ambapo Yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu amejiwajibisha kuwanusuru na kusimamisha dola lake kupitia mikono yao. Aya hizo si nyingine bali ni za 38 hadi 41 za Surat al- Haj ambazo zinasema:

Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini, mwingi wa kukufuru. Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila tu kwa kuwa wanasema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu asingeliwakinga watu kwa watu, basi hapana shaka yangelivunjwa mahekalu, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Swala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.

 

Ndugu wasikilizaji, tulipata kujua katika kipindi kilichopita na kupitia Aya hizi tulizosoma kwamba wale ambao Mwenyezi Mungu amewaruhusu kupigana Jihadi na kujilazimisha Yeye mwenyewe kuwanusuru mwishoni mwa Jihadi hiyo, ni kundi maalumu la waumini ambao huwa hawafuatilii jambo jingine kwenye vita hivyo isipokuwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kuthibitisha uadilifu wake miongoni mwa waja wake. Bila shaka waja hao wema wanapasa kuwa na elimu kamili na ya kina ya Mitume kuhusiana na irada ya Mwenyezi Mungu pamoja na mambo mema anayowatakia waja wake. Waja hao wema pia wanapasa kuwa na ikhlasi ya hali ya juu katika kuvumilia matatizo mengi wanayokumbana nayo katika njia hiyo. Hili ndilo jambo linalobainika wazi katika sira na maisha ya Milango ya Mji wa Elimu ya Mtume Muhammad (saw) na Maimamu Watoharifu wa Nyumba yake. Tunasoma katika Nahjul Balagha kauli ya Bwana wa Maimamu hao al-Imam Ali bin Abi Talib (as) ambapo ananong'ona na Mola wake kuhusiana na Jihadi yake dhidi ya Nakitheen (wasaliti na waliokiuka utiifu/agano), Mariqeen (waliotoka kwenye dini) na Qasiteen (waliopotea njia/madhalimu) kwa kusema:

'Ewe Mola wangu! Wewe unajua kuwa tuliyofanya hayakuwa kwa ajili ya kugombania utawala, wala kutaka chochote miongoni mwa majigambo ya dunia, isipokuwa kutaka kurudisha alama za dini yako na kuleta maendeleo katika miji yako, ili wadhulumiwa miongoni mwa waja Wako wawe katika amani, na zitekelezwe hukumu zako zilizotelekezwa…… Ewe Mola wangu! Mimi ni wa kwanza kurejea kwako na mwenye kusikia na kuitika. Hajanitangulia katika Swala ila Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).'

 

Wapenzi wasikilizaji na tunasoma katika historia ya Jihadi ya Imam Hussein (as) katika kitabu cha al-Futuh akimuhusia ndugu yake mpenzi Muhammad bin al-Hanafiyya (MA) kwa kusema: 'Hakika mimi sikutoka (kupigana jihadi) kwa ajili ya maslahi yangu binafsi, kujionyesha, kueneza ufisadi wala kudhulumu bali nimetoka kwa ajili ya kufanya marekebisho katika umma wa babu yangu Muhammad (saw). Ninataka kuamrisha mema na kukataza mabaya na kufuata njia aliyoifuata babu yangu Muahmmad (saw) na njia ya baba yangu Ali bin Abi Talib. Hivyo basi anayenikubali kwa haki, ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayeistahiki haki hiyo zaidi na anayenikatalia hili, nitasubiri hadi Mwenyezi Mungu atakapoamua kwa haki baina yangu na kaumu hii, Naye ni mbora wa wanaohukumu.'

**********

Kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, inabainika wazi kutokana na yale tuliyosoma, maana ya maneno yaliyonukuliwa katika Tafsiri za Ali bin Ibrahim, Majmaul Bayaan, Nuru ath-Thaqalain na vitabu vinginevyo kutoka kwa Imam Swadiq (as), kuhusiana na Aya tukufu tulizotangulia kusoma kuhusiana na wale walioruhusiwa kupigana Jihadi aliposema: 'Ziliteremka kumuhusu Ali, Ja'ffar na Hamza na kisha kuendelea – yaani katika Maimamu wa Ahlul Beit. Na kauli Yake: Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, iliteremka kumuhusu Hussein (as) alipotakiwa na Yazid, Mwenyezi Mungu amlaani, kwenda Sham…..na akauawa huko Taf…..inamuhusu pia al-Qaim - (as) – atakapodhihiri kulipiza kisasi cha damu ya al-Hussein.'

Na Imam Baqir (as) amenukuliwa katika Tafsiri ya Furat al-Kufi (as) akisema kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu inayosema: Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Swala, na wakatoa Zaka, 'Wallahi! Aya hii iliteremka kutuhusu sisi.'

Na katika kitabu hicho hicho, Zaid bin Ali amenukuliwa akisema: 'al-Qaim (Imam Mahdi) kutoka kizazi cha Muhammad atakaposimama atasema: Enyi watu! Sisi ndio wale watu mlioahidiwa na Mwenyezi Mungu katika Kitabu chake kwa kusema: Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Swala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote.'

Na imenukuliwa katika Tafsiri ya Ali bin Ibrahim na katika Tafsiri nyinginezo maana ya Aya hii kutoka kwa Imam Abi Ja'ffar al-Baqir (as) ambapo amesema: 'Aya hii inakihusu kizazi cha Muhammad (as), al-Mahdi na masahaba zake. Mwenyezi Mungu atawapa mamlaka ya mashariki na magharibi ya ardhi ambapo atadhihirisha humo dini na Mwenyezi Mungu kuangamiza bida' na batili kupitia kwake na masahaba zake.

**************

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Aya na Hadithi ambacho mmekuwa mkikisikiliza kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi wakati huu, kwaherini.

 

Tags