Apr 21, 2018 11:02 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (49)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 49.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika vipindi viwili vilivyopita tulieleza kwamba suala la Palestina, ambayo ni kadhia muhimu zaidi ya Ulimwengu wa Kiislamu, lina uwezo na fursa nyingi zinazoweza kutumiwa kwa ajili ya kupatikana sauti moja katika Ulimwengu wa Kiislamu, kwa sababu uadui wa Israel kwa Uislamu na nchi za Kiislamu ni jambo lililo wazi na lisiloweza kukanushika. Lakini isitoshe pia ni kwamba kupatikana haki za Wapalestina na kukabiliana na uchu wa kutotosheka na wa kutaka kujipanua wa Israel ni moja ya matakwa muhimu zaidi ya wananchi katika nchi zote za Kiislamu. Kwa hivyo ikiwa serikali za nchi na mataifa ya Waislamu zitaishughulikia kadhia hii zitazidi kuimarisha misingi ya uhalali wa kisiasa wa kukubalika kwao mbele ya wananchi wao na kuandaa mazingira ya kupatikana umoja baina yao na nchi nyingine za Kiislamu. Nukta nyingine tuliyoashiria ni kwamba ikiwa kuundwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu wakati huo, yaani OIC kilikuwa moja ya vielelezo muhimu vya kuwepo sauti moja katika Ulimwengu wa Kiislamu, suala la Palestina lilikuwa na taathira na mchango muhimu katika kuundwa kwa taasisi hiyo. Katika kipindi chetu cha leo tumekusudia kuzungumzia mkataba wa Camp David ili kuweza kuona jinsi mkataba huo ulivyosaliti malengo matukufu ya Palestina na kusababisha mfarakano na mgawanyiko kati ya nchi za Kiislamu.

Tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, Anwar Saadat, rais wa wakati huo wa Misri alitoa amri ya kufanywa shambulio la kushtukiza dhidi ya ngome za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Mfereji wa Suez ili kufidia kipigo na kushindwa vibaya Waarabu katika vita vya Juni mwaka 1967, maarufu kama Vita vya Siku Sita. Muda mfupi baada ya kuanza shambulio la jeshi la Misri, vikosi vya jeshi la Syria navyo pia vilianzisha mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikuwa imevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la utawala wa Kizayuni katika vita hivyohivyo vya mwaka 1967. Shambulio hilo la jeshi la Syria liliwezesha kuwatimua askari wa Israel katika maeneo yote waliyokuwa wameyateka katika vita hivyo. Kwa kutangazwa hali ya hatari, kuitwa askari wa Israel makambini na kutumwa misaada ya haraka ya Marekani kwa utawala huo, mpaka ilipofika siku ya tatu ya vita, Wazayuni walifanikiwa kuvizuia kusonga mbele vikosi vya majeshi ya Misri na Syria; na hadi kufikia mwishoni mwa wiki ya kwanza ya vita, nao pia wakaanzisha mashambulio ya kujibu mapigo. Hatimaye baada ya kupita wiki tatu tangu vilipoanza vita, na katika hali ambayo Misri ilikuwa imepata mafanikio katika siku za mwanzo za vita, kwa kumiminwa Israel misaada ya silaha za Marekani, vita hivyo pia vilimalizika tarehe 24 Oktoba 1973 kwa kushindwa na kurudi nyuma Waarabu kutoka kwenye ngome zao.

Kongamano la Umoja wa Kiislamu, Tehran, Iran

 

Baada ya kushindwa katika vita vya mwaka 1973, Misri, chini ya uongozi wa Anwar Saadat, iliamua kufanya mabadiliko na mageuzi ya msingi katika sera zake za nje kwa kufungua mlango wa mazungumzo ya ana kwa ana na Israel. Ukweli ni kwamba baada ya kushindwa katika vita vya mwaka 1973, viongozi wa nchi za Kiarabu wakiongozwa na Misri waliachana na fikra ya kupambana na utawala ghasibu wa Kizayuni unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu na badala yake wakaamua kuanzisha mazungumzo na adui huyo na kufuata njia ya kufanya mapatano na Marekani na muitifaki wake huyo. Na hatimaye wakakubali kuutambua rasmi uwepo wa utawala haramu wa Israel na kuifuta akilini mwao fikra ya kuwatosa wazayuni wote baharini. Vinara walioipigia upatu fikra na harakati hiyo ni rais wa wakati huo wa Misri, Anwar Saadat ambaye mnamo mwaka 1977 alifunga safari kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopewa jina la Israel, akalakiwa na kukumbatiana na aliyekuwa waziri mkuu wa Israel wakati huo Menachem Begin. Mnamo mwaka 1978, Rais Anwar Saadat wa Misri na Waziri Mkuu wa Israel Menachem Begin walikutana huko Camp David, Marekani na kusaini makubaliano ya amani mbele ya rais wa wakati huo wa nchi hiyo Jimmy Carter, makubaliano ambayo yalikuja kuwa maarufu kama Mkataba wa Camp David. Anwar Saadat alikuwa rais wa kwanza wa nchi ya Kiarabu kuchukua hatua ya kufanya suluhu na Israel na kuutambua rasmi utawala huo haramu wa Kizayuni. Makubaliano ya Camp David yalijumuisha ndani yake masuala matatu makuu, ambayo ni kufikia suluhu na Israel, kuondoka Israel katika jangwa la Sinai na kuirejeshea Misri eneo lake hilo ambalo ililivamia na kulikalia kwa mabavu wakati wa Vita vya Siku Sita na kuanzisha mazungumzo kwa ajili ya kuundwa nchi ya Palestina inayojiendeshea masuala yake ya ndani katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza. Kufuatia kusainiwa mkataba wa Camp David, pande mbili za Cairo na Tel Aviv zilianzisha rasmi uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia sambamba na kubadilishana mabalozi.

**************

Kusainiwa mkataba huo wa kihaini kati ya Misri na utawala wa Kizayuni kulikofanywa bila kujali wala kuzingatia matakwa ya wananchi wa Palestina na maslahi ya umma wa Kiislamu kulikuwa na maana ya kuhalalisha uvamizi na uchokozi wa uzayuni wa kimataifa na kukanyaga haki za watu wa Palestina. Mkataba huo ambao ulitayarishwa kwa usimamizi wa Marekani haukuwa na matunda mengine yoyote ghairi ya kuifanya Israel istakiri na kujizatiti katika ardhi za Palestina inazozikalia kwa mabavu na wakati huohuo kuzusha hitilafu na mfarakano kati ya nchi za Kiislamu na za Kiarabu. Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa ujumbe maalumu tarehe 5 Farvardin 1358 (sawa na tarehe 25 Machi 1979) kwa mnasaba wa suluhu iliyofikiwa kati ya Misri na Israel, akiwahutubu Waislamu duniani na kulaani mkataba wa makubaliano hayo. Sehemu moja ya ujumbe huo ilieleza kama ifuatavyo:

"Kwa zaidi ya miaka 15 sasa, nimekuwa nikitanabahisha kuhusu hatari ya Israel ghasibu na kuzitangazia ukweli huu nchi na mataifa ya Kiarabu. Kwa mpango huu wa kikoloni wa suluhu ya Misri na Israel, hatari hii sasa imekuwa kubwa zaidi, ya karibu zaidi na yenye uzito zaidi… Iran iko kitu kimoja na ndugu zake Waislamu wa nchi za Kiarabu na iko pamoja nao katika maamuzi watakayochukua. Iran inaitakidi kuwa suluhu ya Saadat na Israel ni usaliti kwa Uislamu na Waislamu na ndugu zake Waarabu na inakubaliana na misimamo ya kisiasa ya nchi zinazopinga mkataba huu."

Siku chache baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilivunja uhusiano wake wa kisiasa na Misri kulalamikia mkataba huo wa kihaini wa Camp David.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kukomea hapa huku nikitumai kwamba mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine ambapo tutakuja kuendelea na maudhui yetu hii. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags