May 12, 2018 04:14 UTC
  • Jumamosi, Mei 12, 2018

Leo ni Jumamosi tarehe 25 Shaaban 1439 Hijria mwafaka na tarehe 12 Mei 2018 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 278 na hivyo likawa limekubaliana na ombi la wananchi wa Bahrain la kutaka kutumwa nchini humo, mjumbe wa Umoja wa Mataifa. Mjumbe huyo alisalia nchini Bahrain kwa muda wa wiki mbili na kukutana na viongozi wa kisiasa na kikabila waliokuwa na ushawishi nchini humo. Natija ya mazungumzo hayo ikawa ni Bahrain kutangaza uhuru wake. ***

Bahrain

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, yaani tarehe 22, Ordibehesht, mwaka 1364 Hijria Qamaria, makumi ya watu walikufa shahidi na kujeruhiwa kutokana na shambulizi ya bomu lililotekelezwa na kundi la kigaidi la Munafiqiin (MKO) mjini Tehran. Mripuko huo mbali na kusababisha uharibifu mkubwa, uliteketeza kikamilifu jengo moja la ghorofa mbili na karakana ya ufumaji nguo katika barabara ya Naser Khosro na kuua watu 9 na kujeruhi wengine 45. Katika hujuma hiyo ya kigaidi, magaidi wa MKO walitumia bomu lililokuwa na mada za milipuko za TNT zilizokuwa na uzito wa pauni 50. Kundi hilo la kigaidi limekuwa likifanya mashambulizi ya aina hii hapa nchini kwa shabaha ya kupiga vita Mfumo wa Kiislamu na kudhoofisha usalama wa taifa. Mauaji hayo ya kinyama kwa mara nyingine tena yaliidhihirishia dunia jinai za kutisha za kundi la kigaidi la MKO, lenye kuungwa mkono na madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni. ***

Mlipuko wa bomu katika barabara ya Nasser Khosro, Tehran

 

Na siku kama ya leo miaka 10 iliyopita, tetemeko kubwa la ardhi lililokuwa na ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China. Katika tetemeko hilo la kutisha, watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Aidha tukio hilo la kutisha liliwaacha bila makazi mamilioni ya watu nchini China. Zilzala hiyo inahesabiwa kuwa moja ya mitetemeko mikubwa ya ardhi iliyowahi kuikumba China katika miongo mitatu iliyopita. ***

Mtetemeko wa ardhi katika mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China

 

Tags