Jumatatu tarehe 18 Juni, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 4 Shawwal 1439 Hijria sawa na Juni 18, 2018.
Siku kama ya leo miaka 1088 iliyopita yaani tarehe 4 Shawwal mwaka 351 Hijria alifariki dunia Muhammad bin Hassan Darqutni, aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu wa karne ya nne Hijria. Darqutni alikuwa miongoni mwa maqari na wafasiri mashuhuri wa Qur'ani wa zama hizo. Mwanazuoni huyo alitumia wakati mwingi wa umri wake kuandika vitabu, na mashuhuri zaidi kati ya vitabu vyake ni "Al Muujamul Akbar" na "al Manasik Wal Maudhi' Fii Maanil Qur'an."
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita inayosadifiana na tarehe 18 Juni 1953 utawala wa kifalme ulisambaratika nchini Misri na kukaasisiwa mfumo wa Jamhuri baada ya Mfalme Farouq wa nchi hiyo kupelekwa uhamishoni. Kufuatia kushindwa Misri katika vita na Israel mwaka 1948 wananchi wa Misri walipoteza imani yao kwa Mfalme Farouq na hivyo hali ya ndani ya Misri kuanza kuharibika. Mwishowe liliundwa shirika la siri ndani ya jeshi lililopinga utawala wa mfalme huyo. Mwaka 1952 shirika hilo lilimlazimisha Mfalme Farouq kujiuzulu kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Muhammad Najib na Jamal. Mwaka mmoja baada ya kutangazwa Jamhuri ya Misri, Jenerali Muhammad Najib aliapishwa kuwa rais wa kwanza wa Misri. Mwaka mmoja baadaye Jamal Abdul Nassir alimuuzulu Muhammad Najib. Abdul Nassir alipata umaarufu mkubwa nchini Misri na duniani kote kwa sababu ya kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Miaka 39 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano ya pili ya kupunguza silaha yaliyojulikana kwa jina la Salt 2 kati ya Marais Leonid Brezhnev wa Urusi ya zamani na Jimmy Carter wa Marekani. Makubaliano hayo yalikuwa na lengo la kupunguza silaha za nyuklia duniani.
Miaka 21 iliyopita katika siku kama ya leo, Najmuddin Erbakan Waziri Mkuu aliyekuwa na misimamo ya Kiislamu wa Uturuki alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya wanajeshi wa nchi hiyo. Chama cha Erbakan kilipata kura nyingi katika uchaguzi wa Disemba mwaka 1994 na kuunda Baraza la Mawaziri. Lakini wasekulari na makamanda wa jeshi walizuia kutekelezwa malengo ya serikali ya Arbekan. Waziri Mkuu huyo alikuwa akiamini kwamba kuwakandamiza wanaharaki wa Kiislamu nchini Uturuki ni kinyume na demokrasia na alipinga kuimarishwa uhusiano wa nchi hiyo na utawala ghasibu wa Israel. Lakini Baraza la Usalama wa Taifa la Uturuki ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa wa wanajeshi Februari 1997 lilitoa amri ya kumlazimisha Erbakan akabiliane na wanaharakati wa Kiislamu. Miezi minne baadaye waziri mkuu huyo alishtakiwa mahakamani kutokana na misimamo yake ya Kiislamu na kuzuia kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa muda wa miaka mitano.