Jun 24, 2018 01:11 UTC
  • Jumapili, Juni 24, 2018

Leo ni Jumapili tarehe 10 Shawwal mwaka 1439 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 24 Juni 2018 Miladia

Siku kama ya leo miaka 1111 iliyopita alifariki dunia Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi, maarufu kwa jina la 'Ibn Muqlah', mwandishi, mchora hati na mvumbuzi wa hati tofauti za uchoraji. Alizaliwa mjini Baghdad na kujifunza masomo ya dini kwa wasomi mashuhuri wa mji huo kipindi hicho. Akiwa kijana Ibn Muqlah aliingia katika idara ya vyombo vya mahakama katika utawala wa Ibn Abbas. Hata hivyo muda mfupi na kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya utawala na mienendo iliyokuwa kinyume na dini ya watawala hao, walipatwa na hasira na hivyo kumtia jela Ibn Muqlah. Hatimaye na kutokana na amri ya mtawala wa wakati huo, watumishi wa utawala walimkata ulimi na mikono msomi huyo na kisha kumuua shahidi muda punde baadaye. Umashuhuri wake mwingi ulishuhudiwa katika sekta ya uchoraji. Miongoni mwa vitabu vya Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi ni pamoja na 'Risaalat fi Ilmil-Khat wal-Qalam' na 'Risalat fi Mizaanul-Khat.'

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar. Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri tukio hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi walivishambulia vikosi vya Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao. Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812.

ناپلئون بُناپارت

Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.

Henry Bessemer

Siku kama ya leo miaka 206  iliyopita yaani tarehe 24 Juni, Caracas mji mkuu wa Venezuela ulidhibitiwa na Simon Bolivar ikiwa ni wakati wa mapambano ya mpigania uhuru huyo dhidi ya wakoloni kwa ajili ya kuyakomboa maeneo ya Amerika ya Kusini. Mkoloni Muhispania alishindwa katika vita hivyo vilivyodumu kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja na baada ya ushindi huo Simon Bolivar anayejulikana kama shujaa wa mapambano dhidi ya wakoloni huko Amerika Kusini, aliasisi Shirikisho la Colombia Kubwa. Shirikisho hilo lilijumuisha nchi za Venezuela, Colombia, Panama na Ecuador, na Bolivar akachaguliwa kuwa rais wa kwanza wa shirikisho hilo.

 

Tags