Jun 26, 2018 14:32 UTC
  • Jumanne tarehe 26 Juni, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 12 Shawwal 1439 Hijria saw ana Juni 26, 2018.

 Siku kama ya leo miaka 409 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai. Sheikh Bahai ambaye alikuwa mtaalamu wa fiqhi, nujumu na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 952 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin.

Miaka 182 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini, na alikuwa akiimba mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na kutunga pia nyimbo za hamasa na kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina "La Marseillaise" ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa.

Rouget de Lisle

Miaka 73 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika vita hivyo.

سازمان ملل متحد

Na siku kama ya leo miaka 58 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika katika karne ya 18. Mwishoni mwa karne ya 19 Ufaransa ilifanikiwa kukidhibiti kikamilifu kisiwa cha Madagascar. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa.

Bendera ya Madagascar

 

Tags