Jun 30, 2018 07:58 UTC
  • Aya na Hadithi (23)

Assalaam Aleikum Wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakukaribisheni kusikiliza sehemu ya 23 ya kipindi hiki cha Aya na Hadithi huku tukimwomba Mwenyezi Mungu atupe sote nguvu na taufiki ya kutekeleza yale anayoyaridhia na kujiepusha na yale anayoyachukia.

Tuko pamoja nanyi katika dakika hizi chache za kipindi hiki ambapo leo tutajadili Aya za mojawapo ya Sura Tukufu zaidi za Qur'ani Tukufu na ambayo Hadithi zinawasihi Waislamu kuisoma kwa wingi kutokana na utukufu mkubwa wa Sura hiyo. Sura hiyo si nyingine bali ni Surat al-Qadr ambayo tunatangulia kuisoma hapa kwa makini ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:  Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Hakika Sisi tumeiteremsha Qur'ani katika Usiku wa Heshima (Laylatul Qadri). Cheo Kitukufu. Na nini kitachokujuulisha nini Laylatul Qadri? Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. Huteremka Malaika na Roho katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo.  Ni amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri.

 

Sura hii Tukufu inazungumzia usiku ulio bora zaidi duniani ambao hujikariri kila mwaka na ambapo Mwenyezi Mungu huwakadiria waja na viumbe wake mambo yao katika kipindi cha mwaka mzima. Kwa mtazamo huo usiku huu muhimu na mtukufu ni usiku wa kudhihirishwa Umola wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa viumbe wake na kwa mtazamo wa pili ni usiku wa Walii Mtukufu wa Mweynyezi Mungu katika kila zama, kwa sababu Malaika humteremkia (as) huku wakiwa wamebeba makadirio ya mwaka mzima ya Mwenyezi Mungu. Walii Maasumu wa Mwenyezi Mungu huwa ni khalifa na mtekelezaji wa mipango yake kwa viumbe na waja wake.

Kutokana na hakika kuwa Umola wa Mwenyezi Mungu huwa haukutatiki na riziki yake kwa waja wake inaendelea kuwepo, hivyo Usiku wa Leilatul Qadr hujadidika kila mwaka. Allama Tabarsi anasema katika Tafsiri yake ya Majmaul Bayaan: 'Imenukuliwa kutoka kwa Abu Dhar kwamba alisema: Nilisema, Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Usiku wa Leilatul Qadr ni jambo linalofungamana na zama za Mitume. Hivyo basi, je, wanapoaga dunia, usiku huo nao pia hukatika na kuondolewa? Mtume alijibu kwa kusema: La hasha, bali utaendelea kuwepo hadi Siku ya Kiama.'

 

Na imenukuliwa katika Tafsiri ya Nur ath-Thaqalain ya Sheikh al-Huwaizi (MA) kutoka kwa Abu Ja'ffar wa pili yaani Imam al-Jawad (as) kwamba Imam Ali (as) alimwambia Ibn Abbas: 'Hakika Lailatul Qadr ipo katika kila mwaka na katika usiku huo huteremka mambo ya mwaka mzima. Na kuna Mawalii (viongozi/wasimanizi) wanaosimamia mambo hayo baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw). Ibn Abbas akauliza: Je, Watu hao ni akina nani? Akajibu Imam: Ni mimi na watu wengine 11 kutoka kizazi changu.'

Na Sheikh Swadouq (MA) ameandika katika kitabu cha Maani al-Akhbar akimnukuu al-Asbagh bin Nabata kutoka kwa Ali bin Abi Talib (as) kwamba alisema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: Ewe Ali! Je, unajua maana ya Leilatul Qadr? Nikasema: Hapana ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu katika usiku huo amekadiria (amejaalia) kila jambo litakavyokuwa haidi Siku ya Kiama, na miongoni mwa mambo yaliyokadiriwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Wilaya yako na Wilaya ya Maimamu kutoka kizazi chako hadi Siku ya Kiama.'

************

Kwa maelezo hayo wapenzi wasikilizaji, inabainika wazi kwamba Sura tukufu ya al-Qadr ni miongoni mwa dalili zilizo wazi zaidi za Qur'ani kuhusiana na udharura wa kuwepo Khalifa na Imam Maasumu katika kila zama. Hii ni dalili na hoja ya wazi zaidi ya udharura wa kuwepo Walii wa Mwenyezi Mungu katika kila zama, awe ni wa kudhihiri waziwazi miongoni mwa watu au kuzibwa na kuwa kwenye ghaiba, ili Malaika na Roho waweze kuteremka kwake kwa idhini ya Mola wao kama inavyosisitiza Sura hii tukufu. Imepokelewa kwa wingi katika Tafsiri za Nur ath-Thaqalain, Mizaan, Kanz ad-Daqaiq, Burhan na tafsiri nyinginezo kutoka kwa Abu Ja'ffar al-Imam al-Baqir (as) Hadithi inayosema: 'Enyi makundi ya Mashia! Piganeni (shindaneni) kwa kutegemea Sura ya Inna Anzalanahu, mtashinda. Wallahi Sura hii ni Hoja ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa viumbe Wake baada ya Mtume Wake (saw) nayo ni bwana wa dini yenu na mwisho (upeo wa juu) wa elimu yetu. Enyi Makundi ya Mashia! Shindaneni kwa 'Haa Meem, Walkitaab al-Mubeen, Inna Anzalnahu fii Lailatin Mubarakatin Inna Kunna Mundhireen', kwani (Sura hii) ni Mawalii (wasimamizi) maalumu wa mambo baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw).'

 

Wapenzi wasikilizaji, na katika ukarimu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kuwa, ameujalia usiku huu wa Lailatul Qadir kuwa salama hadi mapambazuko ya alfajiri, na katika dalili za wazi za jambo hilo ni kuongezwa maradufu thawabu za mtu anayefanya ibada katika usiku huo huku akiwa anautambua utukufu wake. Imam Baqir (as) amenukuliwa katika Tafsiri ya Ali bin Ibrahim na Tafsiri nyinginezo akisema baada ya kuulizwa maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu inayosema: 'Lailatul Qadir ni bora kuliko miezi elfu': 'Kutenda mambo mema katika usiku huu kama vile Swala, Zaka na mambo mengine ya kheri, ni bora kuliko kuyafanya mambo hayo katika miezi elfu isiyokuwa na Leilatul Qadr…..'

Kuhusu suala hili kuna Hadithi nyingi mno ambazo zimepokelewa kuhusiana na fadhila za kusoma Suratul Qadr katika Swala na sehemu nyinginezo, kwa mfano kwa ajili ya kupata shufaa kutokana na maradhi mbalimbali ya kimwili, kisaikolojia na kiroho. Maulama wa irfani wanasema kuwa Sura hii ni miongoni mwa dhikri za kuaminika na zenye athari kubwa katika kung'arisha na kuangaza moyo, nasi hapa tutatosheka kwa kutaja Hadithi moja ambayo imenukuliwa na Sayyid bin Taus (MA) katika kitabu cha Muhj ad-Da'waat. Inasema Imam Swadiq (as) aliulizwa: 'Je, ulijikinga na kitu gani ulipofika mbele ya Mansur? Akajibu: Na Mwenyezi Mungu na kwa kusoma, Inna Anzalnahu, kisha nikasema: Ya Allahu! Ya Allah! Mara saba, ninatafuta shufaa kwako kupitia Muhammad na Aali zake (saw) – ili unibadilishie (mtu huyu)…… Hivyo anayekumbwa na hali kama hiyo basi na afanye nilivyofanya mimi, na kama tusingekuwa tunaisoma – yaani Suratul Qadr – na kuwaamuru Mashia wetu kuisoma pia, bila shaka wangelitekwa nyara na watu, lakini Wallahi Sura hiyo ni pango (ngome) kwao.'

************

Mwenyezi Mungu akutakabalieni amali zenu wapenzi wasikilizaji mliobahatika kusikiliza kipindi cha juma hili cha Aya na Hadithi ambacho mmekitegea sikio kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags