Jul 10, 2018 12:49 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (114)

Ni wakati mwingine mpenzi msikilizaji mnapojiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia moja ya tabia mbaya za kimaadili ambayo ni kusengenya. Tulisema kuwa, kusengenya, ni moja ya madhambi ambayo huwa ni utangulizi wa kufanywa madhambi mengine na kuenea maovu katika jamii na mwishowe na kutokuweko maelewano baina ya wanajamii. Na hilo huthibiti kwa sura hii, kwamba wakati mtu anapotangaza aibu na mabaya ya watu husababisha kuenea maovu na kuyafanya maovu hayo yazoeleke na kutohisika tena kuwa ni kitu kibaya katika jamii. Aidha tulibainisha baadhi ya njia za kukabiliana na usengenyaji kama kumzindua mwenye kusengenya na kumtaka asisengenye, kujaribuu kubadilisha maudhui unaposikia mtu akisengenywa au mtu kujiepusha kukaa katika vikao ambavyo kunafanyika usengenyaji na kuramba visogo vya wengine. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 114 ya mfulizo huu, kitaendelea kujadili maudhui ya kusengenya na jinsi ya kutubia dhambi hii. Jumuikeni name hadi mwisho wa kipindi hiki.

Wapenzi wasikilizaji, kusengenya ni katika madhambi makubwa na ni wajibu na jukumu kwa Mwislamu mwanamume na mwanamke kutokaa katika vikao ambavyo watu wanasengenya na kuwaramba visogo watu wengine. Hii ni kutokana na kuwa, msikilizaji wa dhambi ya kusengenya hana tofauti na yule anayesengenya. Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema: Msikilizaji wa dhambi ya kusengenya ni mithili ya msengenyaji.

Mafundisho ya Uislamu yanamtaka kila Mwislamu achunge na kulinda heshima ya ndugu yake muumini kadiri ya uwezo wake na asiruhusu hadhi na heshima ya ndugu yake muumini itiwe dosari na kuchafuliwa.

Wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anaye penda kuila nyama ya nduguye aliye kufa? Mnalichukia hilo!

Inapotokea mathalani umejikuta katika kikao ambacho mtu anasengenywa na kusemwa vibaya, basi ni jukumu lako kama Mwislamu kuamrisha mema na kukataza maovu na kumtetea anayesengenywa. Ikitokea kwamba, huna uwezo kwa namna yoyote ile ya kuzuia kitendo hicho cha kusengenywa mtu, basi unapaswa kuchukua hatua nyingine kama vile kujaribu kubadilisha mazungumzo. Endapo hutaweza kuzuia kufanyika dhambi hiyo basi unapaswa kuinuka na kuuondoka katika kikao chenye mazungumzo hayo ya usengenyaji. Endapo hilo nalo haliwezekani, basi kwa uchache uonyeshe katika moyo wako juu ya kutoridhishwa na mazungumzo hayo. Hii ni kutokana na kuwa, kama mtu ataridhia kusengenywa mwenzake na kufurahishwa na kufichuliwa aibu zake, atakuwa ametenda dhambi hata kama hatashiriki katika tabia hiyo chafu ya kusengenya. Sehemu ya aya ya 12 ya Surat al-Hujuraat inasema:

…Wala msipelelezane, wala msisengenyane nyinyi kwa nyinyi. Je! Yupo katika nyinyi anayependa kuila nyama ya nduguye aliyekufa? Mnalichukia hilo! 

Inanukuliwa kwamba, siku moja Bwana mmoja alimsema vibaya mtu mbele ya Mtume (saw) na hapo hapo akajitokeza mtu mwingine na kumtetea yule aliyesemwa vibaya. Mtume (saw) akasema: Mtu ambaye atazuia heshima ya ndugu yake muumini kuharibiwa, atasalimika na moto wa Jahanamu. Aidha imepokewa katika hadithi nyingine kwamba:  Ikiwa mtu atazuia kusengenywa ndugu yake muumuni, Mwenyezi Mungu humuepusha na shari na mabaya elfu moja, lakini ikiwa hatalizuia hilo na bali akaonyeshwa kushangazwa, basi dhambi zake ni sawa za yule anayesengenya.

Kwa hakikka kukataza tu kusengenya haitoshi, bali kila mtu analazimika kutonyamaza anaposikia mtu anasengenywa bali anapaswa kusimama na kumtetea ndugu yake huyo anayerambwa kisogo na kufanya juhudi za kulinda heshima ya ndugu yake huyo. Kimsingi ni kuwa, kila Mwislamu ana jukumu la kuhahalisha kwa njia sahihi ukosoaji na mapungufu ya ndugu yake muumini na kuyatetea na hivyo kuufunga mlango wa kujitokeza tetesi na uenezaji wa habari na uzushi kuhusiana na ndugu yake huyo.

Qur'ani Tukufu na mafundisho ya Uislamu yamekataza kusengenya

Imam Ja'far bin Muhammad al-Swadiq (AS) amenukuliwa akisema maneno yenye thamani kubwa kuhusiana na maudhui hii: Anasema: Usisengenye kwani na wewe utasengenywa, usimchimbie shimo ndugu yako kwani utatumbukia mwenyewe; na tenda ukijua utatendewa kama unavyotenda.  

Kwa mujibu wa hadithi hii, mtu ambaye anawasengenya wengine basi mwenyewe pia anajiweka katika mazingira ya kusengenywa. Imenukuliwa katika hadithi kwamba, Bwana mmoja alimwambia Imam Ali bin Hussein Sajjad (as) kwamba: Fulani anakusema vibaya wewe na kukutaja kuwa ni mpotoshaji na mwenye kuleta bidaa na uzushi.

Imam Sajjad AS akamwambia Bwana yule, hukuwa na haki ya kukaa pamoja naye, kwani umenifikishia maneno aliyoyasema kunihusu mimi. Aidha hukunitendea haki kwani umenifikishia kitu kutoka kwa ndugu yangu ambacho sikuwa na habari nacho!…jiepushe na kusengenya, kwani hiyo ni mboga ya mbwa wa motoni; na tambua kwamba, mtu ambaye anataja aibu na mapungufu ya watu wengine inaonyesha kwamba, anazitafuta aibu hizo kwa wengine kwa kiwango kile kile ambacho anazo yeye.

Wapenzi wasikilizaji kutubia madhambi ni wajibu na kila Mwislamu anapaswa kuonyesha majuto ya dhambi aliyofanya bila kupoteza muda na atubie; na kama hatafanikiwa kutubia dhambi hiyo na akaaga dunia, basi Siku ya Kiama atakabiliwa na madhambi makubwa.

Imekuja katika hadithi kwamba, kila ambaye ana haki ya ndugu yake katika dini (heshima au mali) anapaswa kupata ridhaa yake (kuomba msamaha na kuridhiwa) kabla ya kuwadia Siku ya Kiama ambako dirhamu na dinari hazipatikani na badala yake, mtu huchukuliwa matendo yake memo na kupatiwa yule aliyemfanyia ubaya kama mbadala. Endapo mtu huyo hatokuwa na amali njema, basi huchukuliwa katika dhambi za alimyemdhulumu au kumkanyagia haki yake na kuongezewa yeye katika fungu la dhambi zake.

Kwa msingi huo, basi msengenyaji na mtu anayesikia mtu akisengenywa na kutochukua hatua yoyote ya kuzuia usengengaji au kutoondoka katika kikao hicho wanapaswa kutubia dhambi yao hiyo.

Hata hivyo katika Uislamuu toba ina masharti yake na miongoni mwayo ni  kuacha na kutotenda tena dhambi hiyo, kujutia dhambi yenyewe na kuchukua uamuzi wa kutorejea tena kufanya dhambi husika na kufanya matendo mengine mema ya kufidia dhambi aliyoifnya mhusika.

Wapenzi wasikilizaji, kufanya toba na kujutia dhambi ni njia bora kabisa ya mja kusamehewa na kufutiwa dhambi zake. Pamoja na hayo, kutenda wema na hisani, nayo ni amali yenye taathira katika kusamehewa dhambi za mtu.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 114 ya Surat Hud: "Hakika mema huondoa maovu."

Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 71 ya Surat Furqan:

Na aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu.

Muda wa kipindi chetu kwa leo nao umefikia tamati. Tukutane tena juma lijalo siku na wakati kama wa leo katika mada na maudhui nyingine katika mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu..

Ninakuageni huku nikumomba Allah atupe tawfiki ya kuepukana na dhambi ya kusengenya na kuwa na ujasiri wa kumzuia na kumzindua msengenyaji na kumtaka asisengenye.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…