Aug 10, 2018 02:23 UTC
  • Ijumaa, Agosti 10, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 27 Mfunguo Pili Dhulqaada 1439 Hijria sawa na Agosti 10, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano yaliyojulikana kwa jina la The Treaty of Sèvres kati ya utawala wa Othmaniya uliokuwa umeshindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia na waitifaki wake. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa dola ya Othmaniya ulipoteza karibu asilimia 80 ya ardhi yake iliyokuwa ikiitawala, na kupunguza eneo ililokuwa ikilitawala kutoka kilomita mraba milioni tatu hadi kilomita mraba laki sita tu. Makubaliano hayo yalitambua rasmi makubaliano ya awali ya Ufaransa na Uingereza juu ya kugawana ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Othmania, ambapo Uingereza ilizitawala Iraq, Jordan na Palestina na Ufaransa nayo ilizitwaa na kuzidhibiti Syria na Lebanon.

The Treaty of Sèvres

Siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, vilianza vita vya miaka miwili kati ya Japan na China juu ya mzozo wa maeneo ya Yangtze na Canton ambayo yalikuwa maeneo ya kistratijia ya ardhi ya China. Canton ilikuwa bandari muhimu mno huko kusini mwa China ambayo Wachina walipigana vita vya miaka miwili kuilinda mbele ya uvamizi wa Wajapani. Hata hivyo na baada ya kupata hasara kubwa, tarehe 25 Aprili 1939 bandari ya Canton ikatwaliwa na Japan. Utawala wa Japan uliendelea kujipanua katika ardhi ya China kwa kudhibiti maeneo mengine ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo Wajapani walilazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano makali ya wananchi wa China.

Vita vya China na Japan

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, kufuatia kushindwa kikamilifu Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kwa mujibu wa maazimio ya Kongamano la Potsdam, maeneo ya kaskazini mwa Korea yalidhibitiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani. Kabla ya kushindwa Japan, maeneo hayo yalikuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo. Aidha baada ya siku chache maeneo ya kusini ambayo ni kisiwa  yakadhibitiwa na Marekani. Kudhibitiwa maeneo ya kaskazini na kusini ya Korea ulikuwa utangulizi wa kugawanywa ardhi hiyo katika nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini.

Peninsula ya Korea

Na siku kama ya leo miaka  3 iliyopita mahujaji zaidi ya 100 walipoteza maisha baada ya winchi kuanguka katika Msikiti mtakatifu wa Makka karibu na Kaaba Tukufu. Mbali na kuua mahujaji zaidi ya mia moja, tukio hilo lililotokea Ijumaa tarehe 27 Dhulqaada saa 11 na dakika kumi alasiri kwa wakati wa Makka, lilijeruhi mahujaji wengine 238. Mahujaji wengi walioaga dunia katika tukio hilo ni kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Wakati huo serikali ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa, sababu ya kuanguka winchi hiyo ni upepo na kimbunga kikali kilichotokea katika mji mtakatifu wa Makka. Tukio hilo ambalo vielelezo vyote vinaonesha kuwa lilitokana na uzembe na utendaji mbaya wa serikali ya Saudia na lile la mauaji ya Mina katika siku ya Idul Haj mwaka huo huo ni miongoni mwa matukio machungu zaidi ya ibada ya Hijja.  

Winchi lililoua zaidi ya mahujaji mia moja ndani ya Masjidul Haraam

 

Tags