Ijumaa tarehe 24 Agosti 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Dhulhija 1439 Hijria sawa na Agosti 24, 2018.
Siku kama leo 27 iliyopita, nchi ya Ukraine ilipata uhuru wake toka kwa Umoja wa Kisovieti. Ilikuwa katikati mwa karne ya 17 wakati Russia ilipoanza kuikalia kwa mabavu nchi hiyo ambayo katika zama hizo ilikuwa chini ya udhibiti na utawala wa Poland. Hata hivyo mwaka 1922, nchi hiyo ikaunganishwa na mataifa yaliyokuwa yakiunda Umoja wa Sovieti. Hadi mwaka 1980, harakati za wapigania uhuru nchini humo hazikuwa na nguvu. Hatimaye katika tarehe kama ya leo, Ukraine ikajipatia uhuru.
Miaka 40 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hassan Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha.
Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, mapambano ya Ukuta wa Nudba huko Baitul Muqaddas yalianza. Ukuta wa Nudba huko magharibi mwa Masjidul Aqswa ni eneo alilotumia Mtume Muhammad SAW wakati wa kupaa mbinguni katika safari ya Miiraj na kwa sababu hiyo eneo hilo lina umuhimu wa kidini na kihistoria kwa Waislamu. Tangu wiki moja kabla ya kuanza mapambano ya Ukuta wa Nudba, Wazayuni ambao kidogo kidogo walikuwa wameanza kuikalia kwa mabavu Palestina wakiungwa mkono na Uingereza walianzisha harakati dhidi ya Waislamu. Siku hiyo Wapalestina waliokuwa na hasira walianzisha mapambano makali dhidi ya Wazayuni. Mapambano hayo yalienea kwa kasi kwenye miji mingine ya Palestina na Waingereza wakaamua kutangaza utawala wa kijeshi huko Palestina kwa kuhofia hasira za Wapalestina.
Na miaka 499 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 12 Dhul-Hijja mwaka 940 Hijria, aliaga dunia Ali bin Hassan Karaki Amili mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu. Alipata masomo ya awali katika eneo alikozaliwa la Jabal Amil nchini Lebanon. Baadaye akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu alifanya safari katika nchi za Kiislamu. Mhakiki Karaki kama anavyojulikana zaidi, ameacha athari nyingi za vitabu vyenye thamani kubwa. Jamiul Maqaasid na Risatul Adalah ni baadhi ya vitabu vyake mashuhuri.
