Sep 03, 2018 02:41 UTC
  • Jumatatu tarehe 3 Septemba 2018

Leo ni Jumatatu tarehe 22 Dhulhija 1439 Hijria sawa na tarehe 3 Septemba 2018.

Katika siku kama ya leo miaka 1379 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi. Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali. Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwaunga mkono Ahlul Bait (as). 

Mahala lilipo kaburi la Maitham Tammar

Siku kama ya leo miaka 958 iliyopita alifariki dunia malenga na arif mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari. Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mohabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar."

Khaja Abdullah Ansari

Miaka 360 iliyopita katika siku kama ya leo, Oliver Cromwell Rais wa kwanza na wa mwisho wa Uingereza aliaga dunia. Alianza harakati za kisiasa na kijamii katika rika lake la ujana na mwaka 1640 alichaguliwa kuwa mwakilishi wa Bunge. Katika zama hizo Charles I ndiye aliyekuwa mfalme wa Uingereza.

Oliver Cromwell

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza

huko kusini mwa Iran. Manzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliazimia kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatua ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui. Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7.  

Rais Ali Delvari

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hat hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake Damascus ilidhibitiwa na Ufaransa. 

Haram ya Bibi Zainab, mjukuu wa Mtume (saw) katika mji wa Damascas.

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hiterl pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poand bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo. 

Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki. Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita. 

Waziri Mkuu wa zamani wa Italia Benito Mussolini

Miaka 47 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.

Bendera ya Qatar