Jumamosi, 8 Septemba, 2018
Leo ni Jumamosi tarehe 27 Mfunguo Tatu Dhulhija 1439 Hijria sawa na tarehe 8 Septemba 2018 Miladia.
Tarehe 8 Septemba ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ujinga. Kujua kusoma na kuandika ni miongoni mwa vielelezo vya ustawi katika jamii ya mwanadamu na ujinga husababisha umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mkakati wa kupambana na kutokujua kusoma na kuandika haukuwa wa kuridhisha katika baadhi ya nchi na hadi sasa idadi kubwa ya watu hawajapata neema hiyo. Nchini Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kulifanyika jitihada kubwa za kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa kadiri kwamba Disemba mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuasisiwa Harakati ya Kupambana na Ujinga. Taasisi hiyo imepiga hatua kubwa hapa nchini. ***

Katika siku kama ya leo miaka 748 iliyopita, alifariki dunia Muslihud-Din Sa’adi Shirazi, malenga na mwalimu mkubwa wa mashairi na tenzi za lugha ya Kifarsi. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika uga wa lugha na masomo ya dini, Sa’adi Shirazi alielekea mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kujiendeleza kielimu. Akiwa mjini hapo alijifunza masomo ya elimu za enzi hizo, huku akifanya safari katika maeneo mbalimbali kama vile Sham, Palestina, Hijazi, Roma na maeneo mengi ya dunia. Katika safari hizo, Sa’adi Shirazi aliweza kujifunza tamaduni za watu tofauti na hivyo akaongeza kipaji chake katika kusoma mashairi. Baadaye alirejea eneo alikozaliwa na kujikita katika kutoa elimu kwa vijana wa mji huo. Mwaka 655 malenga huyo alihitimisha kazi ya kuandika kitabu muhimu kwa jila la Bustan kilichojumuisha masuala ya akhlaqi na malezi bora ambacho alianza kukiandika akiwa katika safari zake hizo. ***

Miaka 255 iliyopita katika siku kama ya leo, baada ya mapigano ya muda mrefu na kwa mujibu wa makubaliano ya Paris, Canada iliondoka chini ya udhibiti wa Ufaransa na kudhibitiwa rasmi na Uingereza. Hata hivyo mivutano baina ya Wacanada wenye asili ya Ufaransa na Waingereza waliokuwa wakiishi Canada iliendelea kwa muda mrefu. Licha ya Canada kujitangazia uhuru na mamlaka ya kujitawala mwaka 1867 lakini nchi hiyo inafuata Uingereza katika mfumo wake wa kisiasa. ***

Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, wanajeshi wa Ujerumani ya Kinazi waliuzingira mji wa Leningrad, Saint Petersburg ya sasa. Hata hivyo mji huo haukutekwa na jeshi la Kinazi licha ya matarajio ya Adolf Hitler na makamanda wake. Wakazi wa Leningrad waliendeleza mapambano ya ukombozi hadi Januari mwaka 1944 wakati walipofanikiwa kujiondoa katika mzingiro wa wanajeshi wa Ujerumani. ***

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, kulitiwa saini mkataba wa ulinzi wa mataifa ya Asia ya kusini mashariki (SEATO) katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila. Mkataba huo ulitiwa saini na nchi za Marekani, Uingereza, Australia, Pakistan, Thailandi, Ufaransa, New Zealand na Ufilipino. Kwa mujibu wa mkataba huo, nchi mwanachama itakapokabiliwa na mashambulio ya kijeshi kutoka nje, uasi na vitisho vya ndani, basi nchi wanachama zinapaswa kuisaidia nchi hiyo kijeshi au kwa kutumia wenzo wa vikwazo.***

Na miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi wa utawala wa kidikteta wa Pahlavi walishambulia maandamano makubwa ya wananchi wa mji wa Tehran na kuua raia wengi. Wananchi Waislamu wakazi wa Tehran siku hiyo walianza kuandamana tangu asubuhi, hayo yakiwa maandamano ya siku kadhaa mfululizo kuwahi kufanywa na wakazi wa mji wa Tehran dhidi ya utawala wa kibaraka wa Pahlavi. Wakati huo, utawala wa kijeshi ulikuwa umetangazwa katika mji wa Tehran, lakini wananchi Waislamu walipuuza hali hiyo na wakamiminika mitaani wakipiga nara dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo huo walinzi maalumu wa Shah walifanya mashambulizi na katika muda mfupi wakawaua shahidi wananchi zaidi ya elfu nne wa Tehran waliokuwa wakipigania haki zao.***
