Hadithi ya Uongofu (125)
Ni wakati mwingine mpenzi msikilizaji wa kujiunga nami katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la ukorofi, ukaidi na kutoa visingizio. Tulisema kuwa, mtu ambaye ana tabia ya kutoa visingizio licha ya kuwa na elimu na ufahamu kamili juu ya ukweli, kimsingi huwa ni mkaidi na mkorofi na hukwepa kukubaki haki na ukweli. Tabia na mwenendo huu mbaya, baadhi ya wakati kutokana na kukaririwa, hudhihirika na kuwa sifa za wazi za mtu. Sifa ambayo humfanya na kumgeuza mtu huyo kuwa muasi katika jamii anayoishi. Kipindi chetu cha wiki hii ambacho ni sehemu ya 125 ya mfululizo huu, kitazungumzia suala la kutoifanyia kazi elimu yaani elimu bila amali. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Kama inavyofahamika Aya ya kwanza aliyoteremshiwa Bwana Mtume saw na Malaika Jibril AS kutoka kwa Mwenyezi Mungu ilikuwa ikimuasa na kumtaka mbora huyo wa viumbe asome na kujifunza elimu. Baada ya hapo makumi ya Aya zikashuka zikibainisha umuhimu wa elimu, kujifunza na kutafuta elimu. Hata hivyo kwa mtazamo wa Uislamu ni kuwa, lililo na umuhimu ni kuifanyia kazi elimu na sio kuwa na elimu tu.. Kwa maana kwamba, kuifanyia kazi elimu aliyonayo mtu kuna umuhimu maradufu ikilinganishwa na kuwa na elimuu pasi na kuifanyia kazi. Hii ni kutokana na kuwa, mtu ambaye hanufaiki na elimu yake ni mithili ya punda aliyebeba mzigo ambaye hana anachofahamu na kudiriki ghairi ya uzito wa mzigo.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 5 ya Surat al-Jum’ua kwamba: Mfano wa waliobebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
Bwana Mtume SAW katika kukemea wasomi na wajuzi ambao hawanufaiki na elimu yao anasema: Kila ambaye elimu yake itaongezeka, lakini hidaya yake isiongezeke, basi elimu yake haina kitu kingine ghairi ya kumuweka mbali na Mwenyezi Mungu.
Alimu na msomi ambaye hayafanyii kazi maneno yake, kimsingi maneno yake chimbuko lake sio imani. Mtu huyo ambaye kutokana na kuwa na malengo ya kimaada na yasiyo ya Kimwenyezi Mungu endapo atazungumza kuhusiana na dini ya Mwenyezi Mungu, maneno yake hayawezi kuwa na taathira kwa anaowahutubu. Hii ni kutokana na kuwa, wakati watu wanapoona kwamba, matendo yake yanakinzana na maneno yake, hutilia shaka maneno yake na hujiuliza huku wakiwa na shaka kwamba: Kwa nini yeye mwenyewe hakifanyi kile anachokisema?
Imam Ja’afar bin Muhammad al-Swadiq AS anasema akibainisha hilo kwamba: Kila wakati alimu asipoifanyia kazi elimu yake, nasaha zake huteleza katika nyoyo kama matone ya mvua yanavyodondoka juu ya jiwe safi.
Elimu ni sababu na wenzo wa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, lakini kama elimu hiyo isipofanyiwa kazi, huwa mzigo kwa mtu na badala ya kumfikisha mja katika kilele, humporomosha mwanadamu huyo na kumfikisha katika madhila. Si hayo tu, bali watu wa aina hiyo yaani wenye elimu na ambao hawaifanyii kazi elimu yao, huandaliwa adhabu kali na huwekwa chini zaidi katika moto wa Jahanamu.
Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW kwamba: Watu wa motoni watakuwa wakiudhika na harufu mbaya ya alimu na mwanazuoni ambaye (hapa duniani) hakuwa akiifanyia kazi elimu yake; na miongoni mwa watu wa motoni ambaye atakuwa akijuta zaidi kuliko wengine ni alimu na mwanazuoni ambaye alimlingania mtu mwingine katika njia ya Mwenyezi Mungu na yule aliyemlingania akaingia peponi kutokana na kumtii mwenyezi Mungu, lakini yule mlingania yeye akaingia motoni kutokana na kutoifanyia kazi elimu yake na kufuata hawaa na matamanio ya nafsi yake.
Kuna wakati maulama na wanazuoni ambao hawazifanyii kazi elimu zao wakiwa na malengo ya kimaada huegemea nafasi ya tablighi na kueneza mafundisho na sharia za dini na hivyo kuwanyima fursa watu ya hidaya na kupata ujumbe na risala ya Allah na kwa muktadha huo, huwa chimbuko la watu kupotea. Imam Ali bin Abi Twalib AS amewalaani watu wa aina hiyo kwa kusema: Mwenyezi Mungu awalaani watu ambao wanaamrisha mambo mema na wao wenyewe si wenye kutekeleza hilo, wanakataza watu mambo mabaya na wao wenyewe ni wenye kuyafanya hayo.
Alimu asiyeifanyia kazi elimu yake ni mfano wa matone ya mvua yanayodondoka katika jiwe na kuteleza.
Kwa hakika wasomi na wanazuoni wakweli ni wale ambao wanakifanyia kazi kile wanachokisema. Imam Ja’afar bi Muhammad al-Swadiq AS amenukuliwa akisema: Mtu ambaye matendo yake hayasadikishi maneno yake, sio alimu. Kimsingi ni kuwa, katika maisha ya kawaida katika jamii, watu hutazama zaidi matendo ya alimu na kumfuata kuliko maneno yake. Kwa maana kwamba, hujifunza zaidi kupitia matendo na mwenendo wake kuliko maneno na miongozo yake. Alimu anapoifanyia kazi elimu yake hata akiwa amenyamaza na hazungumzia, kimsingi huwa anafundisha. Hii ni katika hali ambayo, alimu asiyeifanyia kazi elimu yake sio tu kwamba, maneno yake hayana taathira bali huwa na madhara. Imam Ali bin Hussein al-Sajjad AS anamfananisha na mbweha alimu na msomi ambaye haifanyii kazi elimu yake. Alimhutubu mmoja wa wanafunzi wake mashuhuri aliyejulikana kwa jina la Zurarah bin A’yan kwa kumwambia: Ewe Zurarah! Katika zama zetu watu wamo katika makundi sita; Simba, mbwa mwitu, mbweha, mbwa, nguruwe na kondoo… Amma mbweha ni wale watu ambao wanaitumia dini kwa ajili ya kutarazaki yaani kujipatia riziki na kile ambacho wanakitamka kwa ndimi zao hakipo katika nyoyo zao.
Kwa hakika jambo baya zaidi ya elimu bila amali ni mtu kuamrisha kitu ilihali yeye mwenyewe si mwenye kukifanya. Yaani yule ambaye anatoa maneno na miongozo katika hali ambayo yeye mwenyewe hanufaiki na hilo. Qur’ani tukufu imewakemea watu ambao wanaamrisha mambo ilihali wao wenyewe si wenye kuyafanya. Aya ya pili na ya tatu katika Surat Swaff zinasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لا تَفْعَلُونَ
كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّهِ أَن تَقُولُوا مَا لا تَفْعَلُونَ
Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda? Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda.
Katika aya hii Mwenyezi Mungu anabainisha wazi kwamba, kitendo cha watu kusema mambo wasiyoyatenda kinamchukiza mno. Aidha nukta nyingine tunayojifunza katika aya hii kwamba, maneno yasiyo na vitendo hayana thamani yoyote ile bila kujali yanatoka kwa nani na hata kama msemaji wake kidhahiri ataoneana kuwa muumini. Hii ni kutokana na kuwa, kuongezeka maneno bila vitendo hupelekea hali ya kutoaminiana itawale katika jamii.
Imenukuliwa kutoka kwa Bwana Mtume SAW ya kwamba amesema: Katika usiku wa Miraji nikutana na watu ambao midomo yao ilikuwa ikikatwa kwa mikasi ya moto. Nikauliza, hawa ni akina nani? Nikajibiwa kwamba, hawa ni watu ambao walikuwa wakiwaamrisha watu kutenda wema ilihali wao wenyewe walikuwa wameghafilika.
Aidha mbora huyo wa viumbe alimwambia Abu Dharr mmoja wa masahaba zake wema na watiifu kwamba: Ewe Abu Dharr! Kundi miongoni mwa watu wa peponi watalililia kundi miongoni mwa watu wa motoni na kuwaambia: Nini kulichokuingizeni motoni ilihali kwa mafundisho na malezi yenu sisi tumeingia peponi? Kundi lile litajibu kwa kusema: Sisi tulikuwa tukikuamrisheni mtende wema, ilihali sisi hatukuwa ni wenye kuyatenda hayo.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu umefikia tamati la leo. Ninakuageni huku nikumbuomba Allah atujaakie kuwa miongoni mwa wanaomarisha mema na kuwa mstari wa mbele katika vitendo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.