Sep 09, 2018 11:09 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (61)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 61.

*******

Katika mifululizo kadhaa iliyopita mbali na kutupia jicho awamu tofauti za harakati za Jumuiya ya Nchi za Kiislamu hadi kufikia mwaka 2011, tuliutathmini utendaji wa asasi hiyo katika kufikia malengo iliyojiwekea hususan ya kuleta umoja na mshikamano kati ya nchi wanachama; na tukabainisha kwamba kama kipimo cha tathmini hiyo ni ufikiwaji wa malengo yaliyoainishwa kwenye hati ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, basi mafanikio iliyopata jumuiya hiyo ni ya kiwango cha wastani au ya kati na kati; na kwa maneno mengine, katika kipindi chote hicho OIC haikuweza kufikia kikamilifu malengo iliyojiwekea, lakini pia hatuwezi kudai kwamba jumuiya hiyo haikupata mafanikio yoyote yale; kwani laiti kama OIC isingelikuwepo, hapana shaka kuwa hali ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu ingelikuwa mbaya zaidi.

Katika kuendelea na uhakiki na tathmini hiyo tulizungumzia pia nukta za "kudhamini usalama wa pamoja kwa ajili ya nchi wanachama" na "kutatua kwa njia za amani hitilafu baina ya wanachama", masuala mawili ya msingi yaliyobainishwa kwenye hati ya OIC; na katika tathmini tuliyofanya kuhusu kiwango cha mafanikio yaliyopatikana katika kufikia malengo hayo tukafanya hitimisho kwamba, katika kudhamini usalama wa pamoja wa nchi wanachama, Jumuiya ya Nchi za Kiislamu haina rekodi ya kujivunia katika uwanja huo, kwa sababu katika matukio mengi yaliyojiri, ilichofanya zaidi ni kujaribu kudhibiti tu hali ya mambo badala ya kutatua tatizo lililopo. Na katika suala la "kutatua hitilafu kwa njia za amani", pia OIC haijapata mafanikio; na hata katika baadhi ya matukio, ilichukua hatua za kushadidisha mgogoro, vita na umwagaji damu baina ya nchi wanachama. Kwa kuzingatia tathmini hizo tulizotoa, katika kipindi chetu cha leo tumekusudia kuzifanyia upembuzi na uchanganuzi sababu za OIC kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 

Ikiwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu haijaweza kupata mafanikio katika kufikia malengo yake, hali hiyo itakuwa imesababishwa na mambo gani? Tukiyachunguza matukio yaliyojiri katika Ulimwengu wa Kiislamu katika vipindi tofauti vya umri wa OIC tutabaini kuwa, moja ya sababu kuu za kutofanikiwa jumuiya hiyo kimalengo ni nchi wanachama kujali zaidi maslahi yao binafsi kuliko maslahi ya pamoja na ya jumuiya. Katika hali ambayo, kimsingi hakuna mtazamo mmoja baina ya nchi za Kiislamu kuhusu ufahamu wao juu ya Uislamu, ukweli ni kwamba kuzingatia manufaa na maslahi yao ya pamoja ndiko kunakoweza kuwa chachu ya kuziunganisha na kuleta umoja kati yao; lakini hata msingi huo pia umedhoofishwa katika jumuiya ya OIC, kiasi kwamba kufadhilisha na kuweka mbele manufaa ya kitaifa badala ya manufaa ya jumuiya na ya pamoja kumesababisha utengano na misimamo kinzani katika stratejia na mikakati ya jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu na kuzusha hitilafu na mfarakano baina ya nchi wanachama. Ni wazi kwamba katika jumuiya ya ushirikiano wa kieneo na kimataifa, pale nchi wanachama zinapoamua kufumbia macho na kuipa kisogo misingi na hati ya ushirikiano wao na kufadhilisha manufaa yao binfasi badala ya manufaa na maslahi ya pamoja na ya jumuiya, hakuna shaka kuwa hali ya kuaminiana na ya ushirikiano katika jumuiya hiyo itakuwa dhaifu tu.

Kwa kulitolea mfano suala hili ni kwamba, wakati Misri, ambayo ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ilipoona maslahi yake yatakidhiwa kwa kufanya suluhu na utawala haramu wa Israel, iliamua kuukanyaga mmoja wa misingi muhimu zaidi ya ushirikiano ya OIC ambao ni kukabiliana na utawala huo wa Kizayuni kwa ajili tu ya kurejeshewa eneo lake la jangwa la Sinai, na hivyo ikasaini mkataba wa mapatano wa Camp David. Hatua hiyo ya Misri ilijenga hisia miongoni mwa nchi wanachama wa OIC kwamba licha ya kuwemo kwenye ushirikiano wa kijumuiya, inawezekana kukiuka na kuipa kisogo misingi ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu na kuyatoa mhanga manufaa ya muda mrefu ya OIC kwa ajili ya maslahi yao ya kitaifa na ya muda mfupi. Hatua ya Misri ya kusaini mkataba wa Camp David na kufanya suluhu na Israel, mbali na kujenga hali ya kutoaminiana kati ya wanachama wa OIC ilisababisha kufukuzwa mmoja wa wanachama muhimu zaidi wa jumuiya na kuyumbisha uthabiti wa kiwango fulani iliokuwa nao jumuiya hiyo ya nchi za Kiislamu. Lakini isitoshe pia ni kwamba, hatua hiyo ya Misri iliondoa zile hisia za kuona ni uovu na ubaya kuchukua hatua za aina hiyo ndani ya OIC na kuzifanya baadhi ya nchi nyingine wanachama, nazo pia zifuate mkondo huo. Miongoni mwa nchi hizo ilikuwa ni Jordan.

 

Mfano mwengine tunaoweza kuuashiria wa hatua ya kufadhilisha na kutanguliza mbele maslahi ya kitaifa badala ya manufaa ya pamoja ya OIC ni uvamizi wa kijeshi uliofanywa na Iraq dhidi ya Iran. Hatua hiyo ya Iraq ya kuivamia kijeshi Iran ilichukuliwa katika hali ambayo misingi ya hati ya Jumuiya ya Nchi za Kiislamu imebainisha wazi kuhusu kutatuliwa kwa njia za amani mizozo inayojitokeza baina ya nchi wanachama na ulazima wa kuheshimiwa suala hilo na nchi husika. Kutokea Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kushika hatamu za uongozi utawala wa Kiislamu kungeliweza kuifanya jumuiya ya OIC iwe thabiti na imara zaidi; lakini kwa kuwa Iraq ilitaka kufanikisha malengo yake ya kitaifa kuhusiana na kadhia ya Mto Arvand, si tu iliukiuka mkataba wa Algeria iliosaini na Iran mwaka 1975, lakini iliidharau na kuipuuza pia misingi iliyokubaliwa na nchi wanachama wa OIC. Vita hivyo vilizitumbukiza nchi hizo mbili muhimu na athirifu katika Ulimwengu wa Kiislamu na zilizokuwa mstari wa mbele katika kupambana na Israel, kwenye lindi la vita haribifu na angamizi vya muda wa miaka minane, na kudhoofisha kwa kiwango kikubwa nguvu na uwezo wao. Hakuna shaka yoyote kuwa laiti kama Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ingeushughulikia mgogoro huo ipasavyo na kwa insafu ingeweza kuepusha kutokea hasara na uharibifu huo sambamba na kuziunganisha pande mbili hizo na kuzielekeza kwenye njia ambayo ingeinua kimataifa nafasi na hadhi ya nchi za Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo ili kuendelea na maudhui hii katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

 

Tags