Sep 09, 2018 11:16 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (63)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 63.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka mtakuwa na mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tulichambua utendaji wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu ambayo sasa ni Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu hadi kipindi cha mwaka 2011 na kufanya tathmini ili kuona ni kwa kiwango gani utendaji huo umewezesha kufikiwa malengo yaliyokusudiwa na OIC hususan la kuleta umoja na mshikamano kati ya nchi za Kiislamu. Tulisema kwamba kwa ujumla, mafanikio iliyopata jumuiya hiyo katika suala hilo ni ya kiwango cha wastani. Tukaangazia pia kasoro zilizopo katika maamuzi na hatua zinazochukuliwa na OIC na nchi wanachama wa jumuiya hiyo na katika uhakiki na upembuzi tuliofanya kuhusu sababu za kuwepo kasoro na upungufu huo tukataja mambo matatu ambayo ni mosi: kufadhilisha maslahi ya taifa badala ya maslahi ya pamoja; pili: misuguano na uingilianaji wa misimamo na maslahi ya OIC na ya baadhi ya taasisi na jumuiya za kikanda; na tatu: kutokuwepo hakikisho na dhamana ya utekelezaji wa maamuzi yanayopitishwa. Hizo, kama tulivyotangulia kueleza, ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi zilizoikwamisha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, katika kipidi cha hadi mwaka 2011 au lilipoanza vuguvugu la Mwamko wa Kiislamu, kufikia kikamilifu malengo iliyojiwekea. Kuanzia sehemu hii ya 63 na mifululizo mingine kadhaa itakayofuatia, tutajikita kujadili na kuchambua matukio yaliyojiri katika nchi za Kiislamu katika kipindi cha miaka sita ya karibuni, hali ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu na hasahasa misimamo iliyochukuliwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu katika kipindi hicho.

 

Cheche ya moto wa mabadiliko ya kisiasa na kimapinduzi maarufu kama Mwamko wa Kiislamu katika nchi za Kiarabu ilianza kuwakia nchini Tunisia. Mnamo tarehe 18 Desemba mwaka 2010, Muhammad Bu Azizi, kijana mhitimu wa chuo kikuu asiye na ajira, ambaye alilazimika kuwa mchuuzi wa bidhaa za mkononi aliamua kujimiminia mafuta na kujichoma moto kulalamikia ufisadi na idhilali aliyofanyiwa na askari polisi. Tukio hilo lilikuwa mithili ya ghala la baruti lililokuwa likisubiri kuripuka, la manung'uniko na malalamiko ya wananchi hususan vijana dhidi ya hali ya kijamii na kisiasa ya nchi hiyo. Baada ya hapo moto wa malalamiko ulioanza kuwakia nchini humo ukasambaa na kuenea katika nchi nyingine za Kiarabu. Maandamano ya wananchi na hasa vijana nchini Tunisia yaliyoanza kwa kulalamikia ukosefu wa ajira, hali mbaya ya uhaba wa chakula, ufisadi, kukosekana uhuru wa maoni na aina nyingine za uhuru wa kisiasa pamoja na hali mbaya ya maisha yaligeuza mkondo wake kwa kasi na kuilenga mihimili ya utawala wa Zine El Abidine Ben Ali. Hali ya mambo ikabadilika kwa kuzuka makabiliano makali kati ya wananchi na askari polisi na matokeo ya mapambano hayo yakawa ni maafa ya kuuawa na kujeruhiwa idadi kubwa ya watu kulikosababishwa na utumiaji nguvu kupindukia wa askari wa usalama na hatua kali na kandamizi zilizochukuliwa na askari polisi dhidi ya waandamanaji. Lakini hatimaye wananchi walishinda; na mnamo tarehe 14 Januari 2011, utawala wa Tunisia ulipinduliwa, kwa rais Zine El Abidine Ben Ali kutoroka nchi na kukimbilia Saudi Arabia; na huo ukawa mwisho wa kipindi cha miaka 23 ya dikteta huyo kuweko madarakani. Kilichofuatia baada ya hapo ilikuwa ni kutangazwa hali ya hatari na kuundwa serikali ya mseto nchini Tunisia.

Baada ya ushindi wa wananchi wa Tunisia na kuitoroka nchi Ben Ali, wimbi la mapambano na malalamiko ya upinzani wa wananchi yalivuka mipaka na kusambaa hadi nchi jirani ya Misri. Wananchi wa Misri, ambao walikuwa hawaridhishwi na sera na uendeshaji mambo wa utawala wa Hosni Mubarak, walimiminika mabarabarani kumtaka dikteta huyo ajiuzulu.

Maandamano ya umma nchini Misri yalianzia maeneo maalumu, lakini yalisambaa kwa kasi ya kustaajabisha katika miji mingine mingi ya nchi hiyo. Kilichojiri hasa ni kwamba ndani ya muda wa siku kumi, uasi wa watu elfu moja uligeuka kuwa mapinduzi ya mamilioni ya watu waliofurika kwenye uwanja wa Mzunguko wa At-Tahrir. Hatimaye kwa kutangazwa mshikamano wa jeshi na wananchi na kung'atuka madarakani Hosni Mubarak, mapinduzi ya Misri yalipata ushindi ndani ya muda mfupi. Baada ya ushindi wa mapinduzi na kufanyiwa mabadiliko katiba, uchaguzi wa rais wa Misri ulifanyika na Muhammad Morsi, mmoja wa viongozi wa harakati ya Ikhwanul Muslimin akamshinda Ahmad Shafiq na kuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia kwa kura za wananchi katika historia ya nchi hiyo.

 

Baada ya Misri, wimbi la upinzani wa umma lilivuka mpaka na kusambaa hadi nchi jirani ya Libya. Vuguvugu la upinzani nchini Libya lilianza tarehe 13 Januari mwaka 2011 na kufikia kilele tarehe 17 Februari, iliyopewa jina la Siku ya Ghadhabu. Kilichofuatia baada ya hapo ilikuwa ni kuingia mikononi mwa wapinzani wa utawala wa Muammar Gadafi miji ya mashariki na nusu ya miji ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo. Na kuanzia kipindi hicho na kuendelea majeshi kutoka nje ya Libya yakawa na nguvu na nafasi kubwa zaidi katika matukio na mabadiliko yaliyojiri katika nchi hiyo.

Baada ya kushtadi mapigano kati ya jeshi la Libya na wapinzani, na kuuawa maelfu ya waandamanaji, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililaani mauaji hayo na kumtangaza Gaddafi mhalifu na mtenda jinai za kivita. Siku chache baada ya hapo, Ufaransa, Marekani na Uingereza zilianzisha mashambulio ya anga dhidi ya vikosi vya utawala wa Libya na kwa msaada na uungaji mkono huo wa madola ajinabi kwa wapinzani, utawala wa miaka 42 wa Muammar Gaddafi ulipinduliwa na kuhitimishwa rasmi.

Yemen na Bahrain wapenzi wasikilizaji, zilikuwa nchi nyingine ambazo ziliathiriwa na wimbi la Mwamko wa Kiislamu. Maandamano ya upinzani yalianza katikati ya Januari mwakan 2011 katika miji mingi ya kaskazini na kusini mwa Yemen. Malalamiko ya waandamanaji, kwanza yalihusu upinzani wao kwa mipango ya serikali ya kuibadilisha katiba, kukosekana ajira, hali mbaya ya uchumi na ufisadi uliokithiri. Lakini matakwa na madai yao yalibadilika ghafla yakawa ni kumtaka aliyekuwa rais wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh ajiuzulu.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo inshaallah, katika siku na saa kama ya leo katika sehemu ya 64 ya mfululizo huu nakuageni, huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.