Nov 03, 2018 11:24 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (130)

​​​​​​​Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia suala la kupeana mikono, umuhimu wake na jinsi lilivyotiliwa mkazo katika Uislamu.

Tulikunukulieni hadithi kutoka kwa Bwana Mtume SAW inayozungumzia umuhimu wa kusalimia kwa kupeana mikono ambapo amenukuliwa akisema: Wakati mnapokutana, amkuaneni na peaneni mikono kwani kupeana mikono ni salamu bora kabisa, kwani kufanya hivyo hupelekea kuondoa vinyongo, chuki na husuda. Kadhalika tulibainisha adabu za kupeana mikono ambapo tulisema kuwa, wanaopeana mikono wabananishe viganja vyao vya mikono hali ya kuwa vidole vimetengana na kadiri inavyowezekana kila mtu ajitahidi kuchelewa kuondoa mkono wake kutoka katika mkono wa mwenzake. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 130 ya mfululizo huu kitajadili na kuzungumzia suala la kunong'ona kwenye maana ya kusema kwa sauti ndogo na ya chini inayosikika tu na mtu aliye karibu nawe. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

*****

Kunong'ona au kumsemesha mtu masikioni ni kusema kwa sauti ndogo na ya chini kiasi kwamba, hawezi kusikia mtu mwingine isipokuwa aliye karibu nawe. Katika maisha ya kawaida, mazungumzo binafsi ya mtu na mtu ni jambo la kawaida na ni katika mambo ya dharura ya mwanadamu na dini ya Kiislamu imeruhusu jambo hilo. Kwani watu wawili wanaponong'oneza bila shaka wanakuwa na siri au mazungumzo yanayowahusu wao tu na hawapendi asiyekuwa wao ayasikie. Kufanya hivyo huwazuia wale wenye kueneza habari za watu na ambao ni mafisadi kukosa fursa ya kufanya hivyo. Hata hivyo Uislamu umeruhusu unong'onezaji na kunong'onezana watu kwa namna ambayo, hatua hiyo ilinde na kuchunga hisia za watu wengine na hatua hiyo isije kupelekea kutokea mifarakano na hitilafu baina ya watu. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana katika baadhi ya mazingira kunong'onezana kumekatazwa na kuzuiwa. Mtume Muhammad SAW amewausia waumini kwa kusema kwamba: Wanapokuwa watu watatu sehemu fulani, basi watu wawili wasinong'onezana. Kwani kuna uwezekano mtu wa tatu akashawishiwa na shetani na kuingiwa na huzuni. Lakini kama atatokea mtu wa nne na kujiunga nao, wakati huo makundi mawili ya watu wawili wawili yanaweza kunong'onezana na kuzungumza mambo yao yanayowahusu kwa sauti ya chini bila ya wenzao kusikia.

Moja ya sababu za kukatazwa kumnong'oneza mtu kitu masikioni hali ya kuwa kuna mtu mwingine wa tatu ni kwamba, kitendo hicho kikawaida kinaweza kuleta dhana na fikra nyingine mbaya. Mtu ambaye anashuhudia minong'ono ya watu wawili huwa katika mazingira maalumu ya kiroho na kinafsi na hujiona na kujihisi kwamba, yeye kabaguliwa na si mwaminifu kutokana na kutoshirikishwa katika mazungumzo na minong'ono ya wawili wale.

Hadithi ya Leo

Katika upande mwingine, kitendo hicho huwa sababu ya dhana nyingi mbaya au tuhuma au hata kufikiria kwamba, kuna njama zinapangwa dhidi ya mtu wa tatu. Ghairi ya hivyo kusingekuwa na haja ya watu wawili kunong'onezana mbele ya mwenzao. Aidha kwa upande mwingine, Mwislamu ana jukumu la kujiepusha na mazingira ya kutuhumiwa. Kwa maana kwamba, kama ana asilimia fulani kwamba, kumsemeza mwenzake masikioni kutapelekea kutokea dhana mbaya na kumuweka katika mazingira ya kusengenya na kutoa tuhuma, basi anapaswa kujizuia kufanya hivyo. Ndio maana katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Qur'ani kuna aya zinazozikitaja wazi kitendo cha kunong'ona ambacho ndani yake hakina kheri kuwa ni cha kishetani. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 10 ya Surat al-Mujadalah:

Kwa hakika minong'ono hiyo inatokana na Shetani ili awahuzunishe walioamini, na wala haitawadhuru chochote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu tu ndio wategemee Waumini.

Aidha Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 114 ya Surat Nisaa:

Hakuna kheri katika mengi ya wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu.

*******

Katika aya hii Mwenyezi Mungu anabainisha kwamba, hakuna kheri katika minong'ono na katika mengi ya wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa kama hilo litafanyika kwa ajili ya kulinda anga ya kirafiki na heshima ya watu. Kwa maana kwamba, kama katika mkusanyiko wa watu, mtu fulani atamlingania mwingine kwa siri kwa ajili ya kutoa sadaka, kuleta suhulu na upatanishi katika mahusiano ya watu na kurejesha anga ya urafiki na maridhiano baina yao na mengine mfano wa hayo bila shaka atakuwa amefanya moja ya ibada bora kabisa. Hata hivyo katika hili pia mtu anapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya kutafuta radhi zake. Aya ya 9 ya Surat al-Mujaadalah inasema:

Enyi mlio amini! Mnapo nong'ona msinong'one kwa sababu ya mambo ya madhambi, na uadui, na kumuasi Mtume. Bali nong'onezane kwa kutenda mema na kuacha maovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa nyote.

Kwa hakika Qur'ani Tukufu inakitambua kuwa dhambi kubwa kitendo cha kuwaudhi wanaume na wanawake Waumini. Aya ya 58 ya Surat al-Ahzab inaashiria hilo kwa kusema:

Na wale wanaowaudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi ziliodhaahiri

Imam Ali bin Abi Twalib AS anasema kuhusiana na kunong'ona kwa mtazamo wa Uislamu. Kusema kwa siri kuliko kwa juu kabisa ni kule ambako kuna misingi dini na uchaji Mungu na matunda yake ni kufuata njia ya haki na kupingana na hawaa na matamanio ya nafsi.

Na sema na watu maneno mazuri

 

Hata hivyo inapaswa kuzingatia kwamba, kiujumla kumnong'oneza mtu kitu masikioni ni kitendo ambacho kwa mujibu wa Qur'ani Tukufu hakipendezi, isipokuwa tu kama ndani yake kutakuwa na kheri. Hivyo basi, inapasa kuzingatia kwamba, mtu ambaye tunamnong'oneza jambo anapaswa kuwa na ustahiki wa kusikiliza hilo.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kusema kuwa, Mwenyezi Mungu yupo kila mahala na msimamizi wa kila kitu. Mwenyezi Muingu huyo huyo mwenye huruma hapendi kuona mja miongoni mwa waja wake anaingiwa na shaka na dhana kutokana na minong'ono ya watu wengine. Hivyo basi Mwislamu popote alipo anapaswa kuchunga harakati, maneno na matendo yake ili asije akamuudhi mtu na hivyo kumfanya Mwenyezi Mungu kutokuwa radhi naye.

Muda wa kipindi chetu umefikia tamati kwa leo, tukutane tena juma lijalo siku na wakati kama wa leo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…