Nov 03, 2018 11:38 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (132)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu. Kama tulivyoashiria katika vipindi vyetu vilivyotangulia, kipindi hiki hujadili maudhui mbalimbali za kijamii, kimaadili, kidini na kadhalika na kukunukulieni hadithi zinazohusiana na maudhui hizo kutoka kwa Bwana Mtume SAW na Maimamu watoharifu AS.

Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungungumzia suala la waadhi na nasaha. Tulibainisha kwamba, taathira ya mawaidha na nasaha  inafungamana na kiwango cha imani na uaminifu wa msikiaji kwa mzungumzaji. Kadiri kiwango cha uratibu na uwiano baina ya matendo ya mtoaji waadhi na nasaha na maneno yake kinavyokuwa kidogo, vivyo hivyo taathira yake kwa anayehutubiwa hupungua na kuwa kidogo. Tulieleza pia kwamba, Nukta muhimu ni kuwa, mtoaji nasaha naye anapaswa kutumia mbinu nzuri na ya ujanja ili kumfanya yule anayemnasihi asiudhike sana, na hivyo kumuandalia mazingira ya kuipokea nasaha.  Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 132 ya mfululizo huu, maudhui yake ni toba. Endeleeni kuuwa name hadi mwisho wa kipindi hiki.

*******

Miongoni mwa ishara za rehma na mapenzi makubwa ya Mwenyezi Mungu ni neema ya Mwenyezi Mungu kukubali toba. Toba maana yake ni kuacha dhambi, kurejea kwa Mwenyezi Mungu na kuomba msamaha na maghufira. Moja ya matatizo ya maisha ni mwanadamu kukumbwa na mghafala na hali ya usahaulifu katika kumtaja na kumdhukuru Allah. Mtu ambaye ameghafilika na kumsahau Mwenyezi Mungu huwa rahisi kwake kutenda dhambi. Hata hivyo kwa kuzingatia kwamba, Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa rehma na Mwenye kurehemu, amewawekea waje wake njia ya kurejea nayyo ni kutubu baada ya kuwa wametenda dhambi.

Kwa hakika toba maana yake ni majuto au kujuta na kuacha kurejea dhambi na wakati huo huo kurejea katika njia ya haki. Kwa hakika mja mwenye kujutia dhambi, akatubu na kutorejea tena katika dhambi ile, anapendwa mno na Mwenyezi Mungu. Aaya ya 22 ya Surat al-Baqarah inasema:

"Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao tubu" 

Kiwango cha huba na mapenzi ya hali ya juu ya Mwenyezi Mungu ya kurejea na kutubu waja wake waliotenda dhambi tunaweza kukishuhudia katika hadithi iliyopokewa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (AS). Imam Baqir AS anasema: Wakati wowote ule wa usiku wa giza wakati mtu anapopoteza ngamia au mzigo wake wa safari na kisha akaupata mzigo au ngamia wake huyo, ni kwa namna gani huwa na furaha, Mwenyezi Mungu huwa na furaha zaidi yake kwa mfanya toba.

Bwana Mtume SAW amenukuliwa akieleza jinsi Mwenyezi Mungu anavyompenda mja mwenye kutubia pale aliposema:

 لَيْسَ شَيْءٌ أَحَبَّ إِلَى اَللَّهِ مِنْ مُؤْمِنٍ تَائِبٍ أَوْ مُؤْمِنَةٍ تَائِبَةٍ

Hakuna kitu kinachopendwa na Mwenyezi Mungu kama muumini mwanamume mwenye kutubu au muumini mwanamke mwenye kutubu.

Aidha Mtume SAW amenukuliwa akisema kuwa, mwenye kufanya toba ni rafiki wa Mwenyezi Mungu.

 

Kwa upande wake Imam Jafar bin Muhammad al-Sadiq AS anasema: Wakati mja anapofanya toba ya kweli, Mwenyezi Mungu humpenda na hufunika dhambi zake duniani na akhera na kila dhambi alizofanya na ambnazo zimeandikwa na malaika wawili (waliowakilishwa na Allah kuandika matenda ya waja) huwafanya wazisahau na hushusha wahyi katika viungo vya mwili kwamba, vifiche dhambi zake na maeneo ambayo mja huyo alitenda dhambi, Allah huyapa amri yazifiche dhambi za mja huyo.

Kwa hakika kupitia hadhithi hizo tulizotangulia kuzisoma na nyingi nyinginezo tunadiriki umuhimu mkubwa wa kufanya toba na kutubia madhambi ambayo mtu kayatenda.

Wapenzi wasikilizaji, dhambi na kumuasi Mwenyezi Mungu ni kama shimo na korongo refu au sehemu ya maji baharini au ziwani ambapo maji yake yanazunguka ambapo mtu akiangukia hapo huangamia. Dhambi pia ni hivyo hivyo hupelekea maangamizi kwa mtendaji wake.

Hata hivyo toba na uamuzi wa kweli wa kuacha dhambi na humfanya afanye harakati kuelekea upande wa pwani salama ambapo milango ya rehma za Mwenyezi Mungu imefunguliwa kwa ajili yake. Baada ya kuacha dhambi na kujisafisha na kila aina ya uchafu, mtu aliyefanya toba anapaswa kutenda amali njema akiwa na lengo la kufidia dhambi zake. Kwa maana nyingine ni kuwa, mtu aliyeacha dhambi na kufanya toba ni mithili ya mgonjwa ambaye baada ya kutumia dawa kutibu maradhi yake, sasa anapaswa kutumia dawa na chakula cha kurejesha nguvu zilizopotea na kufidia udhaifu wa mwili uliosababishwa na maradhi. Mtu aliyefanya toba pia, baada ya kutubia dhambi na kuwa na azma imara ya kutorejea tena kutenda dhambi, anapaswa kufanya jambo ambalo sambamba na kufuta faili lake la dhambi aondoe kutu na weusi uliosababishwa na dhambi katika baadhi ya nukta na kuyafanya maeneo hayo yang'are kupitia kutenda amali njema na mambo ya kheri.

Kwa mfano kama mtu amemuudhi baba au mama yake, baada ya kutubu na kuondoka ile hali ya maudhi iliyosababisha machungu kwa wazazi wake, anapaswa kuwafanyia huba na mapenzi na hivyo kuibadilisha hali ya uchungu na kuwa utamu.

Toba

 

Imam Muhammad Baqir AS analitambua suala la kuwaridhisha watu ambao haki zao zilipotea kutokana na dhambi kuwa ni jukumu la mfanya toba wa kweli na anasema: Pindi ishara za toba zisipodhihiri, basi mhusika si mfanya toba ya kweli, kudhihirika ishara za toba ni pale wanaodai haki kwake watakaporidhia, atapolipa Swala zilizompita, atakapokuwa mnyenyekevu mbele ya waumini na atakapojilinda na mawimbi ya ushawishi wa nafsi.

Imam Ali bin Abi Twalib AS anazungumzia matunda na athari za kufanya toba kwa kusema: Matunda na athari za toba ni kufidia makosa.

Kwa hakika kufidia dhambi kwa kutenda amali na mambo mema kunaweza kufanyika kwa njia na sura tofauti kama kutoa msaada wa fedha, kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kufunga Saumu, kukesha na kufanya ibada na kadhalika. Hata hivyo kilicho muhimu ni kwamba, mhusika anapaswa kufanya mambo kinyume kabisa na ilivyokuwa hapo awali. Kwa maana kwamba, abadilike na kufanya mambo mema na mazuri kwa ajili ya kutafuta ridhaa za Mwenyezi Mungu.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kukunukulieni hadithi kutoka kwa Imam Muhammad Baqir As inayoyataja mambo kama kuwatendea watu mema na kukesha kwa shabaha ya kufanya ibada kwa ajili ya Allah kuwa ni kafara na mambo yanayofidia dhambi.

Na hadi hapa ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa juma hili, basi hadi tutakapokutana tena, nikakuageni nikumuomba Allah atupe tawfiki ya kufanya toba baada ya kuteleza na kutenda dhambi.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.