Nov 03, 2018 12:27 UTC
  • Ruwaza Njema (3)

(Kumfuata al-Mustafa (saw) katika maneno na kimya chake)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Ruwaza Njema ambapo kwa leo tutazungumzia sifa nyingine njema za Mtume wetu Mktukufu Muhammad al-Mustafa (saw). Tunaanza mjadala wetu wa leo kwa kuzungumzia baadhi ya sifa hizo njema kwa kuashiria Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam wetu mpendwa al-Imam Ali (as) ambaye anatunasihi kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu ya kumfuata Bwana wa Mitume al-Habib al-Mustafa (saw). Hadithi hii kwa hakika ni moja ya hadithi zilizo wazi zaidi katika kufafanua akhlaqi bora na aali ya Bwana Mtume (swa) ambapo tutachambua sehemu fupi tu ya Hadithi hiyo ndefu ambayo inahusiana na suna ya Mtume katika mantiki, maneno na kimya chake. Kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

*******

Imepokelewa katika vitabu vya Makarim al-Akhlaq na Uyun Akhbari ar-Ridha (as) Hadithi ndefu ambapo ndani yake Imam Ali (as) amenukuliwa akisifu maadili na tabia njema ya Mtume (saw) kwa kusema: 'Mtume Mtukufu (saw) akiwa mbele ya watu alikuwa ni mwenye uso wa bashasha, mwenye kutabasamu na mwenye maadili ya kupendeza na mpole. Kamwe hakuwa ni mkali, mwenye moyo wa jiwe (mgumu), mchokozi, mwenye mdomo mbaya, mtafuta makosa  ya wengine wala mkaidi. Hakuna mtu yeyote aliyekata tamaa kuhusiana naye, na kila mtu aliyemtembelea nyumbani kwake, hakurejea alikotoka hali ya kuwa amekata tamaa. Aliachana na vitu vitatu: Ubishi kwenye mazungumzo, maneno mengi na kuingilia mambo yasiyomuhusu. Na aliachana na mambo matatu kuhusu watu: Hakuwa akiwalaumu, kuwakemea wala kudadisidadisi mitelezo (makosa) na aibu zilizojificha (za siri) za watu.

 

Imam Ali (as) anaendelea kusifu suna za ndugu yake Muhammad al-Mustafa (saw) katika mantiki na maneno yake kwa kusema: Mtume (saw) alikuwa hazungumzi ila kwa kutarajia thawabu kutokana na maneno aliyoyasema. Na alipokuwa akizungumza, watu wote waliokuwa wameketi mbele yake walikuwa wakinyamaza kimya ni kana kwamba ndege walikuwa wamesimama kwenye vichwa vyao. Na alipomaliza kuzungumza na kunyamaza, wengine walipata fursa ya kuzungumza. Hakuna mtu aliyeruhusiwa kuzungumzia mambo ya watu wengine kwenye vikao vyake. Mtu alipokuwa akizungumza mbele yake wengine wote walinyamaza kimya hadi aliyekuwa akizungumza amalize alichokuwa akisema na kisha wengine kupewa fursa ya kuzungumza. Mtume (saw) alikuwa akicheka kile walichokuwa wakicheka, kushangaa walichokuwa wakishangaa na kuonyesha subira kubwa mbele ya watu wageni wasiojua mambo, ambao walikuwa wakiuliza maswali kwa njia ya dharau na isiyokuwa ya heshima.  Alikuwa akisema: Mkiona mtu anatafuta haja (jambo) fulani, msaidieni. Alikuwa hakubali kusifiwa na watu waliokuwa na imani dhaifu na wanafiki na wala hakuwa akimkatisha maneno mtu aliyekuwa akizungumza hadi mtu mwenyewe amalize kuzungumza.'

**********

Ndugu wasikilizaji, je, kimya cha Mtume (saw) kilikuwa vipi? Anayejibu swali hili si mwingine bali ni yule anayejua zaidi tabia na akhlaqi ya Mtume ambaye ni ndugu na wasii wake wa karibu al-Imam Ali (as). Amepokelewa katika vitabu viwili vya Makarim al-Akhlaq na Uyun Akhabr ar-Ridha (as) akizungumzia baadhi ya sifa na akhlaqi ya Mtume (saw) kwa kusema: 'Mtume (saw) alikuwa akinyamaza kimya juu ya mambo manne: Subira, tahadhari, kupima (kukadiria) mambo na kutafakari.' Kwa maana kwamba kimya cha Mtume Mtukufu (saw) kilikuwa ni chenye baraka kubwa katika mambo manne yaliyotajwa. Hii ni kusema kuwa kimya chake kilikuwa ni kimya chanya kilichokuwa na matunda muhimu ya heri na baraka, na hilo ndilo jambo linalobainishwa kwa uwazi mkubwa na Imam ali (as) kama tukakavyoona hivi punde.

 

Kuhusiana na hali hizi nne ambazo zinaandamana na kimya cha Bwana Mtume (saw) Imam Ali (as) anasema: 'Ama kupima na kukadiria kwake mambo kulihusiana na kutazama na kuwasikiliza watu kwa usawa. Kutafakari kwake kulihusiana na mambo yanayobaki (kudumu milele) na yanayoangamia. Subira na uvumilivu kwake vilikusanywa pamoja; hivyo hakuna kilichomghadhabisha wala kumkasirisha. Alikuwa akifanya tahadhari kubwa katika mambo manne: Kufanya mambo mema ili watu wengine waweze kufuata mfano wake, kuacha mambo mabaya ili wengine wapate kuyaacha pia, kufanya juhudi na kuwa makini katika kurekebisha umma wake na kufanya mambo ambayo yana heri ya duniani na ya Akhera.'

Hivyo, kimya cha Mtume Mtukufu (saw) kinatufundisha kwamba hatupasi kuzungumza ila mambo mema na ya heri na kwamba tunapasa kujiepusha kutamka mambo mabaya na yasiyo na faida yoyote kwa ajili ya kurekebisha tabia na mienendo ya watu kwa ajili ya manufaa yao ya humu duniani na ya huko Akhera.

**********

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atupe sote, wapenzi wasikilizaji, taufiki ya kuweza kufuata na kutekeleza mema yote aliyotuletea Mtume Mtukufu (saw) kama alivyotuamuru kufanya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kipindi hiki kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiisamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapota fursa ya kukutana tena katika kipindi kingine cha Ruwaza Njema, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags