Nov 03, 2018 12:37 UTC
  • Ruwaza Njema (4)

(Kumfuata al-Mustafa (saw) katika maneno na kimya chake)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya nne ya kipindi hiki ambapo kwa leo tunajadili sifa nyingiene nzuri na za kupendeza katika akhlaqi ya Mtume wetu mpendwa Muhammad (saw), kwa kutegemea maandiko matakatifu ambayo yanatubainishia suna za mtukufu huyo (saw). Kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

*********

Ndugu zanguni katika imani, Mwenyezi Mungu amemsifu Mtume wake Mtukufu (saw) kuwa ni rehema kwa walimwengu wote, na hilo linaoonekana wazi katika Aya ya 107 ya Surat al-Anbiyaa ambapo anamuhutubu kipenzi wake huyo kwa kusema: Nasi hatukukutuma ila uwe ni rehema kwa walimwengu wote.

Kutokana na Aya hii tunafahamu kwamba maadili na akhalaqi ya Mtume Muhammad (saw) ilijaa na kububujika rehema ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, rehema ambayo iliongezeka zaidi kwa waumini. Kwa maana kwamba kadiri imani ya watu ilivyoongezeka ndivyo rehema hiyo ya Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake kwao nayo ilizidi kuongezeka na kuwanufaisha zaidi. Kuhusu suala hilo Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 61 ya Surat at-Tauba: Na miongoni mwao wapo wanaomuudhi Nabii na kusema: Yeye huyu ni sikio tu. Sema: Basi ni sikio la kheri kwenu. Anamuamini Mwenyezi Mungu, na ana imani na waumini, naye ni rehema kwa wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu watapata adhabu inayoumiza.

Na katika mifano ya kufuzu waumini kutokana na rehema hiyo maalumu ya Mwenyezi Mungu ni kumfuata kipenzi chake Muhammad al-Mustafa (saw) katika rehema yake kwa watu wote, hususan kwa waumini.

Wapenzi wasikiliza, miongoni mwa mifano ya wazi ya rehema ya Mtume (saw) kwa waumini ni kuzingatia hisia zao, kuwanyenyekea na kuwaondolea kila aina ya matatizo, udhia na dhana mbaya. Hebu na tuzingatie hapa Hadithi hii ambayo imepokelewa na Thiqatul Islam wal Muslimeen al-Kuleini katika kitabu chake cha al-Kafi akimnukuu Imam Ja'ffar as-Swadiq ambaye amesema: 'Walimletea Mtume kitu (katika mali na chakula) naye akaamua kukigawa miongoni mwa wakazi wa as-Swaffa. Lakini kwa kuwa kilikuwa ni kidogo, hakikuweza kuwaenea wote hao. Hivyo Mtume (saw) akawa na wasiwasi kwamba huenda wahitaji ambao hawakupata msaada huo wakawa wameumizwa na jambo hilo. Hivyo aliamua kuwaendea na kuwaomba radhi kwa kusema: Nililetewa kitu ambacho nilitaka kukigawa miongoni mwenu nyote, lakini kwa bahati mbaya hakikuwaenea watu wote. Hivyo niliamua kukigawa miongoni mwa watu wasiojiweza na walio na njaa ambao nilihofia wana matatizo zaidi.'

**********

Wapenzi wasikilizaji, na Anas bin Malik amenukuliwa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq akisema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipokosa kumuona mtu katika ndugu zake kwa muda wa siku tatu, alimuulizia. Ikiwa (mtu huyo) alikuwa amesafiri (nje ya mji/kijiji), alimuombea dua, na ikiwa alikuwa mjini, alimtembelea na iwapo alikuwa ni mgonjwa, alienda kumpa pole (kumfariji).'

*********

Wapenzi wasikilizaji, Sheikh mwema Muhammad al-Baraqi amenukuu katika kitabu chake cha al-Masin Hadithi kutoka kwa Imam Baqir (as), ambayo inazungumzia suna za Mtume Muhammad (saw) katika kuomba baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuhusiana na chakula kwa kusema: 'Mtume (saw) hakuwa akila chakula wala kunywa kinywaji ila alisema: 'Allahuma! Tujaalie ndani yake baraka na utubadilishie kilicho bora zaidi.' Imam Baqir (as) anaendelea kusema: 'Isipokuwa maziwa ambapo Mtume (saw) alikuwa kisema: "Allahuma! Tujaalie ndani yake baraka na utuzidishie.'

 

Mtume kuomba dua ya kutaka kubadilishiwa chakula na kinywaji alichokunywa hakukutokana na nia yake ya kutaka kubadilishiwa ladha, harufu, rangi wala bei ya chakula na kinywaji alichokunywa, kwa sababu alifikia upeo wa juu wa zuhdi na kukinai vitu vya dunia na kwa hivyo hakuwa akifuatilia mambo ya kidunia kuhusiana na suala hilo. Lengo lake hapa lilikuwa ni kubainisha kuwa kila chakula na kinywaji kina madhara yake isipokuwa maziwa. Dalili ya jambo hili ni kuwa mtu mmoja alifika mbele ya Imam Swadiq (as) na kumwambia kwamba likuwa amekunywa maziwa na maziwa hayo kumdhuru. Hapo Imam (as) akamjibu kwa kusema: La hasha, Wallahi! Maziwa hayana madhara yoyote. Huenda ulikunywa maziwa na kitu kingine na kitu hicho kikawa kimekudhuru, na wewe kudhani kuwa ni maziwa.'

*******

Na katika tabia njema na desturi za Mtume katika kushukuru na kuheshimu neema ya chakula ni kuepuka kwake tabia ya watu wajeuri wanaokufuru neema za Mwenyezi Mungu wanapokula, ili kumnyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu. Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alisema: 'Tokea abaathiwe na Mwenyezi Mungu hadi alipochukua roho yake (kumfisha), na kwa ajili ya kumyenyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mtume (saw) kamwe hakuwahi kula chakula hali ya kuwa ameegemea kitu, kuwacha wazi magoti yake mbele ya watu waliohudhuria vikao vyake wala kumpa mtu mkono wake (kumsalimia) na kisha kuuvuta mkono huo kabla ya mtu huyo mwenyewe kuuvuta mkono wake kwanza.' Na Ibn Abbas amenukuliwa katika kitabu cha Aamali cha Sheikh Tousi akisema: 'Mmtume (saw) alikuwa akiketi sakafuni (bila zulia), kulia sakafuni na kuitikia mwaliko wa watumwa aliokula nao mkate wa shayiri.'

*******

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Ruwaza njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunakushukuruni nyote kwa kuwa pamoja nasi hadi mwisho wa kipindi. Basi hadi tutakapokutana tena panapo majaliwa tunakuageni nyote wapenzi wasikilizaji kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.