Nov 03, 2018 12:57 UTC
  • Uislamu dini ya amani
    Uislamu dini ya amani

(Kumuiga al-Mustafa (saw) katika zuhudi na muamala wake mwema)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Je, Mtume Mtukufu (saw) aliamiliana vipi na dunia na vilevile watu wa pembeni yake katika sira na maisha yake ya kila siku? Jibu la swali hili ndilo tutakalolijadili na kulifuatilia katika kipindi chetu cha leo. Na hili litawezekana tu kwa kufutilia jibu hilo katika maandiko matakatifu ili tuweze kuwa wafuasi wazuri wa tabia njema na aali za mtukufu huyo, kama tulivyoamrishwa kufanya na Mwenyezi Mungu mwenyewe, karibuni.

********

Kwanza kabisa wasikilizaji wapenzi tunategea sikio Hadithi iliyonukuliwa katika kitabu cha Aamali cha Sheikh Mufid (MA) kutoka kwa Maulana al-Imam al-Hussein (as) ambaye anasema: 'Baba yangu Amir al-Mu'mineen Ali bin Abi Talib (as) aliniambia: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: Malaika alinikujia na kusema: Ewe Muhammad! Hakika Mola wako anakupa salamu na anasema: Ukipenda nitaligeuza jangwa lote la Makka kuwa dhahabu kwa ajili yako. Mtume (swa) akainua kichwa chake na kukielekeza mbinguni na kusema: Ewe Mola wangu! Ninataka siku moja niwe nimeshiba na hivyo kukuhimidi na kukushukuru na siku nyingine nihisi njaa ili nipate kukuomba.'

Nam, hivi ndivyo alivyofanya Bwana wa Maurafaa na wanaofahamu vyema hakika ya dunia hii (saw). Alikataa kujaaliwa jangwa lote la Makka kuwa dhahabu ili apate kumiliki utajiri huo mkubwa na usio na mfano wake duniani na kufadhilisha apewe riziki ndogo ya kimaada kila siku ili apate kuhifadhi mawasiliano ya kudumu yaliyopo baina yake na Mwenyezi Mungu, ili awe akimshukuru kutokana na kushibishwa na kumuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu wakati anapohisi njaa na mahitaji mengine.

 

Ndugu wasikilizaji, naye Sheikh mwema al-Hussein bin Said al-Ahwazi (MA) amenukuu katika kitabu chake cha az-Zuhd Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (as) inayosema: 'Mtu mmoja aliingia kwa Mtume (saw) na kumkuta akiwa amelala kwenye mkeka ambao ulikuwa imeacha alama kwenye mwili wake na mto uliotengenezwa kutokana na nyuzi za mti wa mtende ambao ulikuwa pia umeacha alama (za mikunyo na mistari) kwenye shavu lake. Mtu yule alianza kupanguza na kulainisha sehemu iliyokuwa na alama hizo kwenye mwili wa Mtume (saw) huku akiwa anasema: Kamwe Kisra (Mfalme wa Iran) na Kaisari (Mfalme wa Roma) hawaridhii maisha ya namna hii. Wao wanalala kwenye hariri (ya kawaida) na hariri ya Kimashariki iliyotariziwa hali ya kuwa wewe unalalia mkeka huu!! Mtume (saw) akasema: Wallahi! Mimi ni mbora kuwaliko wao! Wallahi! Mimi ni mtukufu kuwaliko wao! Kisha akasema: Nina haja gani na dunia mimi?! Dunia ni mfano wa mpanda mnyama (farasi/ngamia/punda) mpita njia ambaye anapopita karibu na mti (wa kijani) ulio na kivuli huamua kushuka na kupumzika kwa muda chini ya kivuli hicho, lakini mara tu (kivuli hicho) kinapohama na kugeukia upande wa pili (mpanda myama huyo) huondoka chini ya mti huo pamoja na kivuli chake na kuendelea na safari yake.'

**********

Wapenzi wasikilizaji imepokelewa katika kitabu cha Uyun Akhbar ar-Ridha (as) na Makarim al-Akhlaaq na vitabu vingine vya Hadithi ndefu ambayo inabainisha sifa nzuri za Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) ambapo imepokelewa kwamba Imam Hussein alimuuliza baba yake Amir al-Mu'mineen (as) kuhusiana na sifa za Mtume Muhammad (saw) ambapo Imam Ali (as) ambaye alikuwa mjuzi zaidi kuhusiana na Mtume (saw) alisema: 'Mtume (saw) alipoingia nyumbani kwake, aligawa wakati wake katika sehemu tatu: Sehemu ya kwanza kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, ya pili kwa ajili ya familia yake na ya tatu kwa ajili ya nafsi yake. Kisha aliigawa sehemu yake kwa ajili ya nafsi yake na watu, akitanguliza watu wa karibu yake na masahaba zake na kisha watu wa kawaida na wala hakuwa akiwanyima chochote - kwa maana kwamba elimu yake ilikuwa ikiwafikia watu wa kawaida kupitia watu wa karibu yake.'

 

Na Imam Ali (as) anaendelea kubainisha sira na jinsi Mtume (saw) alikuwa akiwafikishia watu wa kawaida baraka zake za kimaanawi kwa kusema: 'Kuhusu sehemu ya umma, sira yake (tabia/njia) ilikuwa ni kwamba alikuwa akiwafadhilisha watu waliokuwa na fadhila, kwa mujibu wa viwango tofauti vya fadhila zao katika dini, juu ya watu wengine. Badhi yao walikuwa na haja moja, wengine haja mbili na wengine haja zaidi. Hivyo alikuwa akizishughulikia haja hizo na pia kuamiliana nao kwa mujibu wa mambo yaliyowarekebisha na kurekebisha umma mzima, kukiwemo kuwajulia hali zao na pia kuwaambia mambo ya dharura. Alikuwa akisema: Watu walio hapa wawaambie wasiokuwepo na ifikisheni kwangu haja ya mtu asiye na uwezo wa kunifikia kwa sababu kila mtu anayefikisha kwa mtawala haja ya muhitaji asiyekuwa na uwezo wa kiwasilisha mwenyewe haja yake hiyo mbele ya mtawala, Mwenyezi Mungu atamuimarisha Siku ya Kiama.'

Na hizi wasikilizaji wapenzi, ni miongoni mwa sifa muhimu ambazo watawala wema wanapasa kuwa nazo katika kila zama na sehemu.

*********

Ndugu wasikilizaji, Imam Ali (as) anaendelea kutusimulia sifa njema na za kuvutia za Mbora wa Viumbe na Bwana wa Manabii, Mtume Mtukufu (saw) katika kuamiliana na watu wa kawaida kwa kusema: 'Mtume (saw) alikuwa hazungumzi ila mambo yanayomuhusu. Alikuwa akiunganisha nyoyo (kuimarisha upendo miongoni mwa watu) na kutowafukuza watu (kwa ukali). Alikuwa akiheshimu na kumchagua mtukufu na mkuu wa kila kabila (aliyekuwa na maadili mema) kuwa kiongozi wao. Alikuwa akiwatahadharisha watu kuhusiana na adhabu ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha kuwasumbua au kuwadhuru. Alikuwa akiwajulia hali masahaba zake, kuwatembelea wagonjwa na kuwauliza watu mambo yaliyokuwa yakiendelea miongoni mwao. Bila ya kupindukia mipaka, alikuwa akisifu na kushajiisha wema na kukemea mabaya pamoja na kutoyapa thamani yoyote. Alikuwa na msimamo mmoja na wa kati kwa kati. Hakughafilika na jambo lolote lile ili kuwafanya watu nao wasije wakaghafilia au kuchoshwa na jambo fulani. Hakuzembea katika haki yoyote wala kuikiuka. Watu waliomzunguka Mtume walikuwa ni Waislamu bora zaidi, na aliyekuwa mbora na wa daraja ya juu zaidi mbele ya Mtukufu huyo ni yule ambaye wema na manufaa yake yaliwafikia watu wote. Kila Mtu aliyekuwa na huruma zaidi kwa wenzake na kuwasaidia ndiye aliyekuwa na nafasi ya juu na kubwa zaidi mbele ya Mtukufu huyo.'

***********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Riwaza Njema ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapopata taufiki ya kukutana nanyi tena katika kipindi kijacho, kwaherini.

Tags