Jumatatu, tarehe 5 Novemba, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 26 Mfunguo Tano Safar 1440 Hijria, sawa na tarehe 5 Novemba, 2018.
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita alifariki dunia James Clerk Maxwell, mwanafizikia maarufu na mwasisi wa kanuni ya mwanga na umeme. Maxwell alizaliwa Scotland tarehe 13 Novemba mwaka 1831 Miladia. Mwaka 1871 Miladia, alitoa kitabu chake kwa jina la 'Umeme na mvuto wa sumakuu 'Magnetism'. Haukupita muda mrefu akateuliwa kuwa mhadhiri wa elimu ya fizikia katika chuo kikuu cha Cambridge, nchini Uingereza. Katika kitabu chake aliweza kubainisha kwa namna nzuri radiamali na taathira nne mkabala na upeo wa kielektroniki na nguvu ya sumakuu sambamba na kufanikiwa kugundua kanuni ya mwanga na umeme.
Siku kama ya leo miaka 133 iliyopita, alizaliwa Will Durant, mwandishi, mwanafalsafa na mtaalamu wa historia wa jimbo la Massachusetts, nchini Marekani. Baada ya kuhitimu hatua kadhaa za kielimu, alifanikiwa kuchukua shahada ya PHD katika uga wa falsafa huku akiteuliwa pia kuwa muhadhiri. Mwaka 1914 Miladia, aliasisi shule moja mjini New York ambayo aliiongoza kwa karibu miaka 13. Mwaka 1926 Miladia Will Durant alitoa kitabu cha masuala ya historia ya falsafa ambapo mafanikio makubwa ya kitabu hicho yalimfanya aweze kukubalika sana kuhusiana na masuala ya historia. Ni kwa ajili hiyo ndio maana ili kuandaa nyaraka za kihistoria na kufanya utafiti zaidi alilazimika kufanya safari tatu kuizunguka dunia. Hatimaye aliandika kitabu kingine cha juzuu kumi ambapo humo aliashiria masuala muhimu na hivyo kuwavutia wengi. Kitabu hicho kilitarjumiwa kwa lugha 12 za dunia. Will Durant alifariki dunia tarehe 9 Novemba 1981 akiwa na umri wa miaka 96.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, yaani tarehe 5 Novemba mwaka 1944, Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa aliaga dunia. Alizaliwa Juni 28 mwaka 1873 katika mji wa Lyon nchini Ufaransa. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu. Nadharia nyingi za msomi huyo zimo katika kitabu mashuhuri alichokipa jina la "Mwanadamu, Kiumbe Asiyejulikana," ambamo ndani yake anapinga demokrasia ya Kimagharibi.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, wakati wa kuendelea harakati za mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala dhalimu wa Shah, serikali ya Sharif Emami ililazimika kujiuzulu. Jafar Sharif Emami alikuwa kibaraka wa ukoloni wakati wa kupamba moto harakati za wananchi Waislamu na alikuwa akitoa ahadi za uongo kwa lengo la kupotosha mwelekeo wa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya Sharif Imami, Jenerali Azhari aliunda serikali ya kijeshi. Hata hivyo Imam Khomeini aling'amua njama na hila za kiongozi huyo na kutangaza kwamba, mawaziri wakuu wanaobadilishwa ni vibaraka wa Shah na ubeberu na akawataka wananchi wasihadaike na hila za viongozi hao bali waendeleze harakati za mapambano za kutaka kuangusha utawala dhalimu wa Shah.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita kulifunguliwa maonyesho ya kwanza ya kimataifa ya vitabu mjini Tehran. Maonyesho hayo yalishirikisha makampuni na taasisi 196 za uchapishaji vitabu za kigeni kutoka nchi 32 duniani yaliyokuwa na vitabu zaidi ya elfu 16. Vilevile taasisi 215 za uchapishaji za ndani ya Iran zilishiriki katika maonyesho hayo. Tangu mwaka huo Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Tehran yamekuwa yakifanyika kila mwaka hapa nchini.
Na siku kama ya leo miaka 4 iliyopita, alifariki dunia George Jordac, mwandishi na malenga mkubwa wa Kikristo aliyeandika kitabu cha 'Imamu Ali Sauti ya Uadilifu wa Mwanadamu'. Jordac alizaliwa mwaka 1926 katika eneo la Marjayoun nchini Lebanon. Alikuwa mhadhiri wa fasihi na falsafa ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Bairut. Aliandika vitabu 30, muhimu zaidi kikiwa ni kitabu hicho cha 'Imamu Ali Sauti ya Uadilifu wa Mwanadamu' chenye juzuu tano. Akielezea sababu ya yeye kuandika kitabu kuhusu Imam Ali bin Abi Twalib (as) na si mtu mwingine yeyote anasema: "Watu wengi wa nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi na Misri walinipa mapendekezo ya kwa mfano, niandike kuhusu maisha ya makhalifa wengine wa Kiislamu lakini sikukubali. Sisemi kwa sababu hao wengine walikuwa ni wabaya, la hasha! Bali ni kwamba, sikuona mtu mwingine bora na aliyefaa kuzungumziwa kama Imamu Ali bin Abi Twalib. Hii ni kwa kuwa mapinduzi ya mtukufu huyo yalikuwa mapinduzi ya kibinadamu, kijamii, kifikra na kiutamaduni.