Hadithi ya Uongofu (133)
Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu.
Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungungumzia suala la toba na kutubia dhambi. Tulibainisha kwamba, toba maana yake ni majuto au kujuta na kuacha kurejea dhambi na wakati huo huo kurejea katika njia ya haki. Kwa hakika mja mwenye kujutia dhambi, akatubu na kutorejea tena katika dhambi ile, anapendwa mno na Mwenyezi Mungu. Aidha tulikunukulieni hadithi kutoka kwa Bwana Mtume SAW inayoeleza jinsi Mwenyezi Mungu anavyompenda mtu anayefanya toba kuliko kitu kingine chochote. Hadithi hiyo inasema:
لَیْسَ شَیْءٌ أَحَبَّ إِلَى اَللَّهِ مِنْ مُؤْمِنٍ تَائِبٍ أَوْ مُؤْمِنَةٍ تَائِبَةٍ
Hakuna kitu kinachopendwa zaidi na Mwenyezi Mungu kama muumini mwanamume mwenye kutubu au muumini mwanamke mwenye kutubu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 133 ya mfululizo huu, kitaendelea na maudhui ya toba na kutubia dhambi. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa na mapenzi makubwa na huruma kwa waja wake amewafungulia waja hao mlango wa toba na kuufanya mlango huo kuwa fursa ya kufidia dhambi, kuacha ufisadi na mambo machafu na kuondoka katika upotofu sambamba na kurejea katika kufanya harakati kuelekea upande wa mwanga na njia ya kweli na ya haki. Ni ukweli uliowazi kwamba, dhambi na kumuasi Mwenyezi Mungu ni kitendo ambacho kinampeleka mwanadamu upande wa maangamizi. Hata hivyo uwepo wa toba na mlango wa kutubia sambamba na mja kuwa na azma na irada thabiti ya kuacha dhambi na kufanya harakati kuelekea upande wa uongofu huwa ni ushindi mkubwa kwani kwa hatua hiyo, milango ya rehma za Mwenyezi Mungu, humfungukia mja huyo aliyefanya toba na kuazimia kutorejea dhambi ile.
Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, moja ya ujazi na neema kubwa za Mwenyezi Mungu kwa mwanadamu ni fursa ya kufanya toba na kuondoka katika giza nene la upotofu na kurejea katika nuru na mwanga wa uongofu. Kwa hakika toba ni fursa ya dhahabu ya kurejea katika makumbatio ya mapenzi ya Allah na kubadilika hatima na majaaliwa ya mwanadamu kutoka katika hatima mbaya na kuelekea upande wa saada na mafanikio. Hata hivyo swali la msingi ni kuwa, mwanadamu anaweza kustafidi na fursa hii na kuiweka harakati ya maisha yake ya duniani na akhera katika njia sahihi mpaka lini?
Imenukuliwa hadithi kutoka kwa Imam Muhammad Baqir AS akisimulia ya kwamba: Mtukufu Nabii Adam AS alimwambia Mwenyezi Mungu: Ewe Mola Muumba! Umemuachia njia shetani upande wangu na ukamfanya atembee kama inavyosambaa damu katika viungo na mishipa yangu, hivyo basi niwekee kitu mkabala na hilo. Nabii Adam AS akajibiwa: Ninakufanyia hili kwamba, kila mtu miongoni mwa wanao (wanadamu) atakapokusudia kufanya dhambi basi katika faili lake hataandikiwa kitu na endapo atafanya dhambi, basi ataandikiwa dhambi moja. Na kila mtu miongoni mwao atakayenuia kufanya amali njema endapo hataifanya basi ataandikiwa jema moja katika faili lake na kama atafanikiwa kutenda amali hiyo njema aliyokusudia kuifanya, basi ataandika mema kumi. Nabii Adam AS akasema: Niongezee Ewe Mola wangu! Sauti ikamjibu, nitawajaalia toba na nitaipanua muda wake hadi roho itakapofika kooni. Nabii Adam AS akasema, hili linanitosha mimi na wanangu.
Baadhi ya watu wanadhani toba au kutubia ni kutamka tu kwa ulimi. Kwa maana kwamba, kama atataja dhikri na kutamka kwa mfano Astaghafirullah, basi hilo limetosha. La hasha, kufanya toba si kutamka kwa ulimu tu, bali mfanya toba anapaswa kujutia dhambi kwa moyo na kisha baada ya hapo aendeleze kwa wengine na kwa nafsi yake nara ya kuacha dhambi. Hatua inayofuata ni kuvifanya viungo vya mwili kutenda amali njema baada ya kuwa vimefanya dhambi. Na hatua ya tatu ni kuhakikisha kwamba, harejei tena katika uchafu wa hapo kabla wa dhambi.
Kupitia hayo tunafahamu kwamba, toba na kutubia si jambo la kijuu juu na la dhahiri, bali ni jambo la ndani mno. Na watu ambao wanafanikiwa kufanya toba ya kweli, sambamba na kuwa na ufahamu na welewa wanapaswa kurejea kwa Mola kwa ikhlasi na kikweli kweli. Imepokewa katika hadithi kwamba, Bwana mmoja ambaye alikuwa amezoea kufungua kinywa chake na kutamka neno 'astaghafirullah' lakini wakati huo huo hakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya maana ya kweli na uhakika wa toba na kutubia, alisema mbele ya Imam Ali bin Abi Twalib AS "astaghafirullah" Naomba msamaha kwa Allah. Imam Ali AS ambaye alikuwa akitambua na kufahamu vyema ufahamu wa kijuu juu na kutokuwa na maarifa ya kweli ya Bwana yule kuhusiana na istighfaar, akamlaumu na kisha akamuuliza. Je unajua istighfaar ni nini?
Kishaa baada ya hapo Imam Ali AS akabainisha maana ya toba na kuomba maghufira kwa kusema: Kufanya toba na kuomba maghufira ya kweli kuna daraja na cheo cha juu sana. Kabla ya kutamka kwa ulimi neno 'astafhafirullah' yaani naomba maghufira na msamaha kwa Allah, unapaswa kupitia hatua sita.
Kwanza, ujutie kikweli kweli dhambi uliyoifanya. Pili, uchukue uamuzi wa kweli wa kutotenda tena dhambi ile. Tatu, kama dhambi na kitendo kibaya ulichokifanya wewe kilileta madhara kwa watu, basi unapaswa kufidia madhara yake, kiasi kwamba, utakakapokutana na Mwenyezi Mungu Mungu, kusiwe na haki ya mtu katika mabega yako. Nne, jihusishe na kulipa kadha ya kila wajibu ambao ulikupita na hukuutekeleza. Tano, iyeyuke na kupotea nyama ya mwili iliyooota kutokana na haramu na badala yake iote nyama nyingine badala ya ile; na sita, mwili uonje uchungu wa kutii kama ambavyo uliuonjesha ladha ya maasi. Wakati huo, utaweza kusema, 'staghafurullah'!
Katika matukio mengi inawezekana kujiepusha kutenda dhambi kwa kujichunga kidogo na kuwa makini. Lakini kama mtu katika akili yake atakuwa na dhana na fikra ya kudogosha dhambi na kuonyesha kwamba, kutenda dhambi fulani si jambo kubwa sana, basi anapaswa kutambua kwamba, dhambi ile ile ambayyo kidhahiri ni ndogo, kwa hakika ina matokeo mabaya mno. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana toba katika Uislamu inatambulika kama "operesheni ngumu na tiba yenye usumbufu mkubwa". Ni sawa kabisa na jinsi mtu anavyotakiwa kuuchunga mwili wake katika suala la uzima na afya na kuelezwa kwamba, "kinga ni bora kuliko tiba." Hivyo basi kuhusiana na dhambi, mtu pia anapaswa kujikinga. Yaani katika hatua ya awali, mja hapaswi kuruhusu dhambi iingie katika mwili wake kama ugonjwa, kwa matumaini ya kwenda kufanya operesheni baadaye, kwani wakati mwingine mtu hukosa fursa hiyo ya kufanya operesheni yaani ya kutubia dhambi.
Kwa leo tunakomea hapa, tukutane tena wiki ijayo. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…