Jumatatu, tarehe 12 Novemba, 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 4 Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na 12 Novemba 2018.
Siku kama ya leo miaka 254 iliyopita alifariki dunia huko Karbala, Iraq faqihi, mpokezi wa hadithi, mhakiki na mwandishi maarufu wa Kiislamu katika karne ya 12 Hijria Sheikh Yusuf Bahrani. Alijifunza elimu ya msingi kwa baba yake na baadaye alielekea Bahrain na Makka kwa ajili ya kupata elimu ya juu. Baadaye alielekea katika mji wa Fasa kusini mwa Iran ambako alianza kufundisha na kuandika vitabu. Wakati huo alianza kuandika kitabu chake kikubwa zaidi cha fiqhi kinachoitwa "al Hadaiqun Nadhirah". Mwanzuoni huyo ameandika vitabu 32 katika taaluma mbalimbali vikiwemo vya "Anisul Musafir" na "Jalisul Khawatwir.''

Tarehe 12 Novemba miaka 178 iliyopita alizaliwa mjini Paris, Ufaransa Auguste Rodin, mtengeneza masanamu mashuhuru wa karne ya 19 Miladia. Uvutiwaji wake wa sanaa hiyo ulidhihiri tangu akiwa na umri mdogo. Miaka kadhaa baadaye alianza kuunda athari nzuri na za kuvutia na hivyo kupata umashuhuri kama mtengenezaji mashurhuri wa masanamu katika zama zake. Auguste Rodin alifariki dunia mwaka 1917 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 121 iliyopita alizaliwa Ali Isfandiyari mashuhuri kwa jina la Nima Yushij, mwasisi wa mashairi ya kisasa nchini Iran. Isfandiyari alizaliwa katika mojawapo ya vijiji vya mkoa wa Mazandaran kwa jina la Yush huko kaskazini mwa Iran. Malenga huyo baadaye alielekea Tehran na kuanza kujifunza lugha ya Kifaransa. Nima Yushij alianza kutunga mashairi na kubuni mfumo mpya wa mashairi. Miongoni mwa sifa za mfumo huo wa mashairi ni kueleza masuala ya jamii kwa lugha nyepesi. Kazi muhimu zaidi ya malenga huyo mashuhuri wa Iran ni maarufu kwa jina la "Afsaneh".
Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita maulama wakubwa wa Iraq, walitoa fatwa ya kukabiliana na uvamizi wa Uingereza dhidi ya nchi yao wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi hicho ardhi ya Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa Othmania ambao askari wake hawakuwa na uwezo wa kupambana na Uingereza. Baada ya fatwa hiyo Waislamu wa Kishia ambao walikuwa wakikandamizwa sana na utawala wa Othamania waliamua kupambana na mvamizi huyo Mwingereza na kuitetea nchi yao ya Iraq bila kuzingatia ukandamizaji waliokuwa wakifanyiwa watawala wao. Ushiriki wa baadhi ya maulama wakubwa katika harakati ya mapambano dhidi ya mkoloni huyo ulizivutia hisia za wananchi na kuwafanya washiriki kwa wingi kupambana na mvamizi huyo. Hata hivyo la kusikitisha ni kuwa, badala ya utawala wa Othmania kuziunga mkono harakati hizo uliziona kama tishio dhidi yake na kuanza kuzikandamiza kwa lengo la kuzifuta kabisa, suala ambalo lilitoa mwanya kwa London kuidhibiti kikamilifu nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita yaani Novemba 12 mwaka 1918, utawala wa kifalme ulifikia tamati nchini Austria na kuanza kipindi cha utawala wa Jamhuri baada ya kushindwa utawala wa Austria na Hungary katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutengana nchi hizo mbili. Mfalme wa mwisho wa Austria, Charles wa Kwanza ambaye alitawazwa kuwa mfalme wa nchi hiyo tarehe 21 Novemba mwaka 1916, alijiuzulu uongozi siku moja tu baada ya kutiwa saini makubaliano ya kusimamisha Vita vya Kwanza vya Dunia hapo tarehe 11 Novemba mwaka 1918 na kuomba hifadhi nchini Uswisi.
Na tarehe 12 Novemba miaka 62 iliyopita, askari wa utawala haramu wa Israel walifanya mauaji mengine ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika kambi kubwa ya Wapalestina mjini Rafah huko katika Ukanda wa Gaza. Jinai hiyo ilifanyika siku chache tu baada ya kutangazwa usitishaji vita baina ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri. Hujuma hiyo ya kinyama ilisababisha mauaji ya Wapalestina 110, wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine wapatao 1,000.