Jumanne tarehe 13 Novemba 2018
Leo ni Jumanne tarehe 5 Rabil Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 13, 2018.
Tarehe 5 Mfunguo Sita miaka 172 iliyopita kilifunguliwa Chuo Kikuu cha kwanza nchini katika muundo na sura ya kisasa. Chuo hicho kilichojulikana kwa jina la 'Darul Funuun' kilianza kutoa mafunzo katika zama za Ufalme wa Nasiruddin Shah Qajar kwa hima ya Amir Kabiir. Lengo la kuanzishwa chuo hicho lilikuwa kufunza sayansi mpya na kuiwezesha Iran kupata viwanda na teknolojia ya kisasa. Miongoni mwa taaluma zilizokuwa zikitolewa katika chuo hicho ni masuala ya tiba, upasuaji, utaalamu wa madini na utengenezaji dawa. Kuanzishwa chuo hicho kulifungua ukurasa mpya katika historia ya elimu nchini Iran.
Miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 13 Novemba 1970, tufani kubwa na kimbunga cha kutisha kiliikumba nchi ya Bangladesh. Janga hilo lilitokea wakati mapambano ya Wabangali kwa ajili ya kujitenga na Pakistan na kupata uhuru yalipokuwa kileleni. Tufani hiyo kubwa ilisababisha vifo vya watu laki mbili na kujeruhi wengine laki nane. Kimbunga na tufani hiyo pia iliwalazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao na kusababisha hasara kubwa katika mashamba, viwanda, makazi ya raia na miundombinu ya nchi hiyo. Bangladesh ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na majanga ya kimaumbile kama vimbunga, tufani na mafuriko ya mara kwa mara.
Siku kama ya leo miaka 48 iliyopita hayati Hafidh Assad alichukua hatamu za uongozi wa Syria baada ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 1970 na baadaye akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha Baath. Hafidh Assad alizaliwa mwaka 1930 na mwaka 1964 alichaguliwa kuwa kamanda wa kikosi cha anga cha jeshi la Syria. Miaka mitatu baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo. Hafidh Assad alifariki dunia mwezi Juni mwaka 2000 baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Na miaka mitatu iliyopita tarehe 13 Novemba saa tatu na dakika 16 usiku kwa wakati wa Ulaya ya kati milipuko kadhaa ya kigaidi ilitokea katika maeneo nambari 1, 10 na 11 ya jiji la Paris nchini Ufaransa na kuua watu 130 na kujeruhiwa wengine 368. Baadhi ya milipuko hiyo ilitokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France ulioko kaskazini mwa jiji la Paris wakati wa mechi ya mpira wa miguu kati ya timu za taifa za Ufaransa na Ujerumani. Wakati huo huo watu wengine 87 waliuawa katika utekeji nyara uliofanyika katika ukumbi wa michezo ya kuigiza wa Bataclan mjini Paris. Mashambulizi hayo yalihesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea nchini Ufaransa baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Siku moja baadaye kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo.