Nov 13, 2018 23:05 UTC
  • Jumatano, Novemba 14, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 6 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 14, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 53 iliyopita mwafaka na tarehe 23 Aban mwaka 1344 Hijria Shamsia, alifariki dunia mwandishi na mhakiki mkubwa wa Kiirani, Said Nafisi akiwa na umri wa miaka 71. Baada ya kupata elimu ya upili, Nafisi alielekea Ufaransa kwa ajili ya elimu ya juu. Baada ya kumaliza masomo yake huko Ufaransa alirejea Iran na kufunza katika vyuo vikuu hapa nchini. Said Nafisi ameandika na kutarjumu vitabu zaidi ya 180 ikiwemo kamusi ya lugha ya Kifaransa na Kifarsi.

Jalaluddin Muhammad Balkhi

Siku kama ya leo miaka 129 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India. Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.

Jawaharlal Nehru

Miaka 129 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri alizaliwa. Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa. Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri.

Taha Hussein

Katika siku kama ya leo miaka 485 iliyopita, Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kisha kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania. Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu.Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa.

Bendera ya Ecuador

Katika siku kama ya leo miaka 302 iliyopita, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo. Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani.

Gottfried Wilhelm Leibnitz

Na miaka 836 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulavi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Balkh ambao ni moja kati ya miji ya Iran ya wakati huo. Molavi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya muda Maolavi alihamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maanavi, Fihi Ma Fihi, Maktubat Maulana na Rabaiyyat. Malenga huyo mkubwa wa Kiirani alifariki dunia mwaka 672 Hijria Shamsia.

Jalaluddin Muhammad Balkhi