Ijumaa, Novemba 16, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 8 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 16 mwaka 2018 Milaadia.
Miaka 1180 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Rabiul Awwal 260 Hijria, aliuawa shahidi Imam Hassan al Askari (AS) mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu SAW katika mji wa Samarra nchini Iraq. Imam Askari AS alizaliwa mwaka 232 Hijria katika mji wa Madina na alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hadi (AS). Kipindi cha Uimamu wake kilikuwa kigumu na nyeti sana kutokana na kuzaliwa Imam wa Zama Mahdi (AS) wakati huo. Alichukua hatua kubwa za kuhuisha Uislamu na kueneza maarifa sahihi na asili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu. Imam Hassan al Askari aliuawa shahidi kwa kupewa sumu na utawala wa Bani Abbas.

Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, yaani tarehe 16 Novemba mwaka 1946, kwa mara ya kwanza ilitengenezwa mvua bandia. Mvumbuzi wa mvua hiyo aliyekuwa mtaalamu wa masuala ya hali ya hewa wa Marekani akishirikiana na mwanakemia mmoja wa nchi hiyo, walitumia gesi ya kaboni na hewa katika kutengeneza mvua hiyo. Mvua bandia hutumiwa katika maeneo yenye ukame au yenye uhaba wa mvua.
Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita inayosadifiana na tarehe 16 Novemba mwaka 1945, vikosi vya jeshi la Ufaransa viliishambulia Vietnam na kuanza mapambano ya muda mrefu ya wananchi kwa ajili ya kuikomboa nchi hiyo. Baada ya karne moja ya kukoloniwa Vietnam na Ufaransa, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Japan iliidhibiti nchi hiyo. Japan iliondoka Vietnam baada ya kushindwa katika vita hivyo, na Vietnam ikaanza kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa.
Miaka 38 iliyopita katika siku kama leo mji wa mpakani wa Susangerd huko kusini magharibi mwa Iran ulishuhudia mapambano kati ya wapiganaji wa Kiislamu na wanajeshi vamizi wa utawala wa zamani wa Iraq. Oparesheni hiyo ya kujihami ilifanywa na wapiganaji shupavu 200 wa Iran waliojumuisha wanajeshi wa ulinzi, wanamgambo wa kujitolea na idadi ya kadhaa ya wenyeji wa mji huo waliokuwa wakitumia silaha nyepesi dhidi ya jeshi vamizi la Saddam. Katika operesheni hiyo wapiganaji shupavu wa Iran chini ya uongozi wa shahidi Dakta Mustafa Chamran, walipambana vikali na kufanikiwa kuukomboa mji wa Susangerd.