Nov 21, 2018 01:09 UTC
  • Jumatano tarehe 21 Novemba 2018

Leo ni Jumatano tarehe 13 Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 21 mwaka 2018.

Miaka 235 iliyopita inayosadifiana na tarehe 21 Novemba mwaka 1783, kwa mara ya kwanza katika historia ya jitihada za mwanadamu za kupaa angani, puto lilitumwa angani. Puto hilo lilikuwa limepandwa na watu wawili mmoja akiwa mwanafizikia wa Ufaransa aliyejulikana kwa jina la Pilatre De Rozier. Tangu alipokuwa masomoni De Rozier alikuwa akifikiria kutengeneza wenzo wa kupaa angani na kwa kutengeneza puto hilo mwanafizikia huyo akawa amefanikiwa kuruka angani.

Pilatre De Rozier

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Butros Butros Ghali alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Umoja wa Mataifa. Butros Ghali alizaliwa mwaka 1922 katika familia ya Kikristo katika mji mkuu wa Misri Cairo. Baada ya kumaliza masomo yake Butros Butros Ghali alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Siasa cha Cairo. Mwanadiplomasia huyo ndiye aliyemshawishi na kumshajiisha Anwar Sadat Rais wa zamani wa Misri kutia saini mkataba wa Camp David mwaka 1978 na katika kuutambua rasmi utawala ghasibu wa Israel.

Butros Butros Ghali

Siku kama ya leo miaka 23 iliyopita inayosadifiana na 21 Novemba 1995, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Makubaliano ya Amani ya Dayton", yalitiwa saini. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa na Waserbia. Zaidi ya Waislamu laki moja waliuawa kwa umati katika vita vya Bonsia.

Mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Bosnia

Katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza na kuiainisha siku hii ya tarehe 21 Novemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Televisheni. Lengo la Umoja wa Mataifa la kuianisha siku hii lilikuwa ni kuweko mabadilishano ya vipindi vya runinga hususan vipindi vinavyotayarishwa kwa lengo la kueneza amani, ustawi wa kijamii na kiuchumi na kuimarisha masuala ya kiutamaduni katika jamii.