Ijumaa tarehe 23 Novemba 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 15 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 23 mwaka 2018.
Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, yaani tarehe 23 Novemba mwaka 1996, ndege moja ya abiria iliyokuwa imetekwa nyara ilianguka katika fukwe za Bahari ya Hindi huko nchini Comoro baada ya kuishiwa na mafuta. Ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Ethiopia aina ya Boeing 767 ilikuwa na abiria 175. Abiria 125 walipoteza maisha yao katika ajali hiyo. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Addis Ababa kuelekea Nairobi.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, alifariki dunia André Malraux mwandishi na msanii maarufu wa Ufaransa. Malraux alizaliwa mwaka 1901 mjini Paris na katika ujana wake alikwenda nchini China na India zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa na kujishughulisha na mapambano dhidi ya ukoloni wa nchi yake huko Mashariki mwa Asia. Wakati akirejea katika safari yake hiyo, aliandika kitabu maarufu kwa jina la ‘Hatma ya Mwanadamu.’ Katika vita vya ndani nchini Uhispania, Malraux alishirikiana na wapigania uhuru wa nchi hiyo. André alikuwa akipinga vita na umwagaji damu na alitetea pia uhuru wa mwanadamu. ‘Vilio vya Ukimya’, ‘Ushawishi wa Magharibi’, ‘Tumaini la Mwanadamu’ na ‘Washindi’ ni miongoni mwa vitabu vilivyoandikwa na msanii huyo wa Kifaransa.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipasisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina. Suala la Palestina lilikuwa miongoni mwa mambo ya mwanzo kabisa kujadiliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakiathiriwa na nchi kubwa zinazowaunga mkono Wazayuni wa Israel na utawala huo ulitumia moja ya maazimio hayo hapo tarehe 14 Mei 1948 kuanzisha dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina.
Na siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, Hanoi mji mkuu wa Vietnam, ulivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Ufaransa. Tukio hilo lilijiri wakati wa vita vya Ufaransa vya kutaka kuzikoloni nchi za India na China. Tangu katikati mwa karne ya 19, Ufaransa ilikuwa ikifanya njama na jitihada za kuongeza makoloni yake suala lililoifanya nchi hiyo pia kuamua kuuvamia mji huo. Hadi mwaka 1885 askari wa Ufaransa waliikalia na kuidhibiti ghuba ya Tonkin na Vietnam. Hatimaye vikosi vya jeshi la Ufaransa vililazimika kuondoka huko Vietnam mwaka 1954 baada ya kushindwa vibaya katika vita hivyo.