Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-13
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 13 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia aina nyingine iliyosisitizwa na Imam Khomein katika masuala ya uadilifu wa kimahakama kuwa ni kutofuatilia na kudadisidadisi imani ya mtu binafsi. Leo pia tutazungumzia aina nyingine ya masuala muhimu yaliyosisitizwa na Imamu Khomeini (MA), hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Ndugu wasikilizaji suala lingine lililoashiriwa na katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kadhia ya mtu kuwa hana hatia hadi ithibitike kinyume chake. Kipengee cha katiba kinasema: "Msingi wa mtu kuwa hana hatia ni kwamba mtu yeyote huwa hahesabiwi kuwa aliye na hatia (mkosa) hadi pale litakapothibitika kosa lake kupitia mahakama zinazofaa." Ni kwa kutumia kipengee hicho, ndipo marufuku dhidi ya vitendo vya utesaji kwa ajili ya kumlazimisha mtuhumiwa kukiri kosa na pia ulazima wa kulindwa matukufu na heshima ya watuhumiwa, ukawa miongoni mwa maudhui ambazo zimesisitizwa na katiba kwa ajili ya kufikiwa uadilifu na usalama wa kimahakama kwa wananchi. Aidha faslu ya 38 ya katiba imefafanua aina yoyote ya utesaji kwa ajili ya kumfanya mtuhumiwa akiri kosa kuwa ni kitendo kisichoruhusiwa na kwamba haifai kumlazimisha kutoa ushahidi au kutoa kiapo kwa ajili ya kuthibitisha jambo fulani. Kwa mujibu wa faslu hiyo ushahidi na kiapo cha kulazimishwa hakina itibari wala thamani yoyote, kama ambavyo mtu anayekiuka sheria hiyo, anatakiwa kuadhibiwa. Faslu ya 39 inaeleza kwamba, kumvunjia heshima mtu ambaye ametiwa mbaroni kwa mujibu wa sheria, mateka, wafungwa au watu waliobaidishwa, ni jambo lililopigwa marufuku na ambalo muhusika wake anatakiwa kuchukuliwa hatua.
**********
Vipengee vingine vya katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia vinaashiria na kusisitiza udharura wa kusimamiwa na kulindwa haki za wananchi na kufikiwa uadilifu na usalama wa kimahakama nchini hapa. Kwa mfano tu, katika kipengee cha 32 cha katiba kumeandikwa kwamba, mtu hapaswi kukamatwa hadi pale kutakapotolewa hukumu na taratibu za kisheria kumuhusu. Mbali na hayo, vipengee vingine kadhaa vinabainisha kwamba, iwapo mtu atatiwa mbaroni, ni lazima kitendo hicho kiende sambamba na kutajwa haraka tuhuma na sababu ya kukamatwa kwake kupitia maandishi kwa mtuhumiwa na kisha faili lake litumwe kwa vyombo vya mahakama katika kipindi kisichozidi masaa 24. Kadhalika kipengee cha 35 cha katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinasisitizia umuhimu wa pande zote mbili za mmashtaka kuwa na wakili katika mahakama zote za nchi, kwa maana kwamba mtuhumu na mtuhumiwa wote wana haki ya kuwateua mawakili ambao watawatetea katika kesi na iwapo hawatakuwa na uwezo wa kuwaajiri mawakili hao, basi mahakama inatakiwa kuwapatia mawakili wa kuwasaidia katika uendeshaji wa kezi yao. Mbali na hayo ni kwamba, ni katika kujaribu kuzuia fujo na kupotea haki za wananchi, ndipo jukumu la kutoa hukumu na kutekelezwa kwake likakabidhiwa mahkama zinazostahiki. Aidha kufungua mashtaka na kwenda mahakamani, ni haki ya wananchi wote ambapo kipengee cha 34 kinafafanua kwamba hakuna mtu mwenye haki ya kuizuia mahkama iliyoidhinishwa kisheria, kutekeleza wajibu wake. Ili kufikiwa uadilifu na usalama wa kimahakama katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefafanua wazi makosa na umuhimu wa wahalifu kuadhibiwa na kwamba, kufanya kitendo chochote au kukiacha kabla ya kupitishwa sheria inayohusiana nacho, hakuhesabiwi kuwa ni kosa.
*******
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 13 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu uadilifu wa vyombo vya mahakama kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndugu wasikilizaji masuala tuliyotangulia kuyazungumzia yanaonyesha kwamba, daghadagha zinazohusiana na uadilifu na usalama wa kimahakama ni mambo yaliyopewa uzito na kuzingatiwa sana na Imam Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vipengee vya katiba hiyo pia vinaashiria masuala mengine kama vile kutolewa hukumu katika mazingira ya wazi, kama ambavyo kuhusu kesi za uhalifu wa kisiasa na vyombo vya habari, kunatakiwa kubuniwa jopo maalumu la kisheria la kusikiliza kesi hizo. Kiujumla tunaweza kusema kuwa, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazingatia sana haki za raia na vyombo vya mahkama vina jukumu la kulinda haki hizo pamoja na uadilifu na usalama wa kimahakama.
*************
Baada ya hayo sasa tuzungumzie suala lingine la uhuru unaoandamana na uadilifu na ambalo ni kati ya mambo ambayo wanamapambano duniani wamekuwa wakilipigania kwa nguvu zao zote. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana katika fasihi ya kisiasa duniani likawa na nafasi yenye thamani kubwa. Kama ilivyo katika falsafa yakisiasa na mapambano ya kisiasa, suala la uhuru limekuwa likizua mjadala mkubwa sana duniani. Katika uwanja huo, kila mrengo hutoa tafsiri na maana tofauti kuhusiana na suala hilo. Tunaweza kusema kuwa, kati ya harakati na mirengo mingine yote ya kifikra na kisiasa, uleberali ndio umekuwa ikidaiwa kutetea zaidi uhuru, hata kama kumekuwepo na mivitano na tofauti nyingi ndani ya falsafa ya mrengo huo weyewe kuhusu uhalalishaji na mipaka ya uhuru huo. Katika uwanja huo, Isaiah Berlin, mmoja wa wanafikra wakubwa wa mrengo wa uleberali, aliutambulisha uhuru kuwa wa aina mbili, chanya na hasi, ambapo katika kufafanua aina hizo za uhuru alisema, uhuru hasi ni ule ulio na maana ya kuepuka uingiliaji wa serikali katika masuala ya watu binafsi huku ule chanya ukiwa na maana ya kuandaliwa uwanja na nafasi kwa ajili ya ushiriki na utendaji wa wananchi. Mirengo yote hiyo, ilitoa nadharia ya uhuru kwa kuzingatia misingi ya kibinaadamu na kiakili, lakini katika maktaba ya Kiislamu na ambayo ilipewa uzito wa kwanza katika fikra na nadharia ya Imam Khomeini (MA), uhuru unatakiwa kusimama juu ya mafundisho ya Uislamu na mfumo wa kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Kilele cha uhuru wa namna hiyo ni kufikia uhuru wa kiroho na kumkurubia Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo na fikra ya Imam Khomeini, pande zingine zote za uhuru kama vile uhuru wa kiimani, kisiasa na kijamii zote hizo zimezingatiwa na dini ya Kiislamu.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 13 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.