Nov 28, 2018 23:35 UTC
  • Alkhamisi tarehe 29 Novemba 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na Novemba 29 mwaka 2018.

Katika siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, Harakati ya Ukombozi ya Kupambana na Ufashisti iliundwa nchini Yugoslavia chini ya uongozi wa Josip Broz Tito. Wapiganaji wa harakati hiyo walitoa pigo kubwa kwa wanajeshi wa Ujerumani wakati Yugoslavia ilipokuwa ikikaliwa kwa mabavu na jeshi la Ujerumani. Mwaka 1944 wapiganaji wa harakati ya ukombozi ya kupambana na Ufashisti nchini Yugoslavia waliwafukuza nchini mwao wanajeshi vamizi wa Ujerumani kwa kusaidiwa na jeshi Jekundu la Urusi ya zamani.

Josip Broz Tito

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliunga mkono kwa wingi wa kura chache suala la kugawanywa ardhi za Palestina baina ya serikali mbili yaani ya Palestina na ya Kiyahudi. Uamuzi huo usio wa kiadilifu na usio wa kimantiki ulichukuliwa chini ya ushawishi wa nchi za Magharibi hususan Marekani na Uingereza.

Siku ya Kimataifa ya Kushikamana na Taifa la Palestina

Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 103. Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na kujifunza elimu ya dini kwa maulamaa wakubwa hususan Ayatullahil Udhma Hairi. Ayatullah Muhammad Ali Araki alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum kwa kipindi cha miaka 35 na kulea wanazuoni na wasomi hodari. Mwanazoni huyo mkubwa wa Kiislamu amezikwa katika Haram tukufu ya Sayyida Maasuma (as) katika mji mtakatifu wa Qum.

Ayatullah Muhammad Ali Araki

Siku kama ya leo miaka 8 iliopita, Madakta Majid Shahriyari na Fereydun Abbasi waliokuwa wahadhiri wa fizikia ya nyuklia wa Iran walilengwa katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi mjini Tehran. Dakta Abbasi alijeruhiwa, na Dakta Majid Shahriyari mhadhiri wa Chuo Kikuu, mwanafizikia na msomi wa nyuklia wa Iran aliuawa shahidi katika shambulio hilo. Magaidi waliofanya jinai hiyo walitiwa nguvuni na kukiri kwamba, walishirikiana na shirika la ujasusi la Israel MOSSAD kutekeleza jinai hiyo.

Majid Shahriyari