Nov 29, 2018 23:17 UTC
  • Ijumaa, Novemba 30, 2018

Leo ni Ijumaa tarehe 22 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1440 Hijria sawa na 30 Novemba 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1436 iliyopita, yaani tarehe 22 Rabiul-Awwal mwaka wa 4 Hijiria, kulianza vita kati ya Waislamu na Mayahudi wa kabila la Bani Nadhir baada ya watu wa kabila hilo kufanya njama za kutaka kumuua Mtume Muhammad (SAW). Bani Nadhir ni moja ya makundi matatu ya Mayahudi waliokuwa wakiishi katika vitongoji vya mji wa Madina, ambao kwa mujibu wa mkataba waliotiliana saini na Mtume (SAW), hawakupaswa kuchukua hatua yoyote iliyo dhidi ya mtukufu huyo na Waislamu kwa ujumla. Baada ya Mayahudi kuvunja mkataba huo, Mtume Muhammad (SAW) aliwaamuru waondoke Madina. Hata hivyo Mayahudi hao ambao tayari walikuwa wamepewa ahadi za kuungwa mkono na wanafiki wa mji huo, hawakuwa tayari kutii amri hiyo. Ni kwa sababu hiyo, ndipo mtukufu Mtume kwa kushirikiana na Waislamu akazizingira ngome za watu hao kwa muda wa siku kadhaa na kuwalazimisha kuondoka katika maeneo yao.

Moja kati ya ngome za bani Nadhiir

Katika siku kama ya leo miaka 351 iliyopita, Jonathan Swift mwandishi mashuhuri wa Ireland alizaliwa huko Dublin mji mkuu wa nchi hiyo. Swift alishiriki pakubwa katika harakati za ukombozi wa Ireland. Baadae, Jonathan Swift alianza kujishughulisha na kazi ya uandishi. Swift alifariki dunia akiwa na miaka 78.

Jonathan Swift

Siku kama ya leo miaka 201 iliyopita, alizaliwa Theodor Mommsen mwanahistoria na mtafiti wa Ujerumani. Baada ya kumaliza masomo, Mommsen alijishughulisha na utafiti kuhusiana na vitabu tofauti na athari zilizobakia za tamaduni za zamani. Miongoni mwa vitabu vyake maarufu zaidi ni kitababu kinachoitwa 'Historia ya Roma ya Kale' ambacho ni kitabu kamili cha historia kuhusiana na mji wa Roma. Mwanahistoria huyo wa Ujerumani alitunukiwa tuzo ya Nobel katika fasihi hapo mwaka 1902 Miladia na kufariki dunia mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 86.

Theodor Mommsen

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, aliaga dunia katika mji wa Cairo Misri, Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad, mmoja wa waalimu na maqarii wakubwa wa Qur'ani Tukufu. Abdul-Basit alianza kujifunza Qurani Tukufu tangu akiwa mdogo na alipofikia umri wa miaka 12 akafanikiwa kupata tunzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani. Ustadh Abdul-Basit katika maisha yake alijishughulisha na usomaji wa Qurani Tukufu na kutunukiwa zawadi na tunzo muhimu katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani tukufu kwenye nchi mbalimbali za Kiislamu, sambamba na kuwavutia Waislamu wengi kwenye kusoma maneno hayo ya Mwenyezi Mungu. Abdul Basit ameacha kanda nyingi za sauti yake nzuri ya Qur'ani Tukufu.

Ustadh Abdul-Basit Abdul-Samad