Ijumaa tarehe 7 Disemba 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 29 Mfunguo Sita mwaka 1440 Hijria sawa na Disemba 07 mwaka 2018.
Tarehe 7 Disemba miaka 129 iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929.
Miaka 77 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl (Pearl Harbor). Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilipokuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ilitangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia.
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita, inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah. Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Muswaddeq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran. Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo" hapa nchini.

Na katika siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Abdul Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni.