Ijumaa, Disemba 14, 2018
Leo ni Ijumaa tarehe 6 Mfunguo Saba Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Disemba 14 mwaka 2018 Milaadia.
Katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, makubaliano ya amani ya Bosnia yaliyojulikana kwa jina la "Dayton Peace Agreement" yaani Makubaliano ya Amani ya Dayton" yalithibitishwa kwa mara ya mwisho katika kikao kilichofanyika mjini Paris, Ufaransa. Makubaliano hayo ambayo yalifanyika kwa mashinikizo ya viongozi wa Marekani tarehe 21 Novemba 1995, yalitiwa saini na Marais wa wakati huo wa Bosnia Herzegovina, Serbia na Croatia. Mafanikio pekee ya makubaliano hayo kwa upande wa Waislamu, yalikuwa ni kuhitimishwa mauaji ya kinyama yaliyokuwa yakifanywa dhidi yao na Waserbia.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1981 Bunge la utawala haramu wa Israel 'Knesset' liliiunganisha rasmi miinuko ya Golan ya huko Syria na ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hatua hiyo ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa nchi za Kiislamu, Kiarabu pamoja na jamii ya kimataifa. Utawala dhalimu wa Israel uliikalia kwa mabavu miinuko hiyo ya Golan ya Syria katika vita baina yake na Waarabu mwaka 1967.
Miaka 107 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Disemba 1911, baada ya juhudi na jitihada za miaka mingi, hatimaye Ncha ya Kusini yaani South Pole ilivumbuliwa na kwa mara ya kwanza na wavumbuzi kadhaa waliwasili katika eneo hilo. Katika siku hii, Roald Amundsen baharia mashuhuri wa Kinorway aliyekuwa akishindana na Robert Falcon Scott wa Uingereza ili kuifikia ncha hiyo ya kusini, aliibuka mshindi na kuitundika bendera ya Norway katika ncha hiyo. Robert Falcon Scott akiwa na wenzake walikumbana na theluji kali wakati wanarejea na kupoteza maisha yao.
Miaka 213 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na 14 Disemba 1805, iligunduliwa nishati ya joto ya makaa ya mawe na George Branclon, mhunzi kutoka Uingereza. Kabla ya hapo, makaa ya mawe yalikuwa yakitumiwa kama mojawapo ya vifaa vya kujengea nyumba. Shehena ya kwanza ya madini ya makaa ya mawe yaliyotumiwa katika nishati ya joto, ilipatikana katika bandari moja iliyoko Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 588 iliyopita, sawa na tarehe sita Rabiuth-Thani mwaka 852 Hijiria, alizaliwa Ibn Iyas, mwanahistoria mashuhuri wa nchini Misri. Ibn Iyas alinakili habari mbalimbali za kihistoria kwa mfumo wa nathari nyepesi, mfumo ambao ulikuwa hautumiwi na wanahistoria wengine. Mfumo huo ulikuwa na umuhimu mkubwa kwenye fani ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari muhimu ya kihistoria za Ibn Iyas ni pamoja na kitabu cha "Badaaiuz-Zuhuur fii Waqaaiud-Duhuur" ambacho kinaelezea historia ya Misri tangu karne za nyuma hadi kipindi chake. Aidha alifafanua maisha ya watawala wa Misri, ujenzi na uimarishwaji wake na mambo mbalimbali yaliyowahi kuikumba nchi hiyo katika karne za nyuma.

Siku kama ya leo miaka 624 iliyopita alifariki dunia Mir Sayyid Sharif Gorgani, mtaalamu wa fasihi wa Iran huko Shiraz. Gorgani alizaliwa mwaka 740 Hijiria karibu na mji wa Gorgani ya leo, kaskazini mwa nchi hii. Mir Sayyid Sharif Gorgani alihesabika kuwa msomi mkubwa katika zama hizo hususan katika uga wa elimu ya fasihi. Ameacha athari mbalimbali mojawapo ikiwa ni kitabu kiitwacho "Risaalatul-Kubra fil-Mantwiq" na "Sharhu Mawaaqif Qadhi Adhdud-Diin Iji."
Na katika siku kama ya leo miaka 1315 iliyopita, alifariki dunia Hisham Bin Abdul-Malik, kiongozi wa 10 katika silsila ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuwa madarakani kwa karibu kipindi cha miaka 20. Hisham aliyekuwa dikteta alizaliwa mwaka 72 Hijiria na kushika uongozi wa Waislamu mwaka 105 Hijiria. Aidha Hisham anafahamika kwa kuwa bahili, katili na dhalimu, ambaye aliwakandamiza Waislamu wa zama zake hususan wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume (saw) yaani Mashia. Mtawala huyo wa Bani Umayyah aliishi katika kipindi cha Imam Muhammad Baqir (as) mmoja wa wajukuu watukufu wa Nabii wa Uislamu ambapo alimfanyia maudhi mengi mtukufu huyo na baadaye kutoa amri ya kuuawa kwake. Mbali na hapo Hisham alifanya ukandamizaji mkubwa dhidi ya harakati za Zaid bin Ali, mjukuu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuliwa Zaid, mtawala huyo dhalimu alitoa amri ya kuchomwa moto mwili wa mtukufu huyo. Licha kwamba katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah, Uislamu ulienea maeneo ya mashariki na magharibi mwa dunia, lakini kulishuhudiwa harakati kadhaa za Kiislamu za kupinga dhulma, kutokana na kushadidi dhulma na ukandamizaji wa Hisham bin Abdul-malik, harakati ambazo zilipelekea kudhoofika kwa dola hilo la Bani Umayyah.
