Jumapili, Disemba 16, 2018
Leo ni Jumapili, tarehe 8 Mfunguo Saba Rabiu Thani, Mwaka 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 16 Disemba, Mwaka 2018 Miladia.
Miaka 1208 iliyopita katika siku kama hii ya leo, yaani tarehe 8 Rabiu Thani mwaka 232 Hijria Qamaria, Imam Hassan Askari AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina. Akiwa katika umri wa utotoni, mtoto huyo alilazimishwa na makhalifa wa Bani Abbas akiwa na baba yake Imam Hadi AS, kuondoka mji huo na kuhamia katika mji wa Samarra ambao wakati huo ulikuwa makao makuu ya utawala wao. Hata kama mtukufu huyo hakuweza kuishi zaidi ya miaka 28 lakini aliacha nyuma maarifa muhimu na adhimu ya Kiislamu. Imam Hassan Askari AS alikuwa na huruma na upendo mkubwa uliokuwa ukiwavutia watu wengi. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Hassan Askary alichukua jukumu zito la kuwaongoza Waislamu sambamba na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu. Kama walivyokuwa Maimamu wengine watukufu, Imam Hassan Askary naye aliitumia karibu sehemu yote ya umri wake kulinda na kueneza mafunzo sahihi na a'ali ya dini tukufu ya Kiislamu.
Katika siku kama ya leo miaka 1081 iliyopita, Abu Feras Hamdani mshairi na mwandishi wa Kiarabu alifariki dunia. Sambamba na kuwa mshairi, Abu Feras alikuwa mpiganaji vita na alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa Seif al-Daulah mtawala wa Halab na alikuwa mmoja wa makamanda wa jeshi.
Miaka 172 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 1268 Hijria, alizaliwa Ayatullah Sayyid Murtadha Kashmiri, mmoja wa maulama na maurafaa mahiri. Alimu huyo alizaliwa katika familia iliyokuwa ikiheshimika. Akiwa kijana mdogo alianza kusoma elimu za Kiislamu kwa baba yake na kwa maulama wengine wa eneo hilo. Akiwa na umri wa miaka 16 Murtadha Kashmiri alifunga safari na kuelekea Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu pia katika maudhui mbalimbali.
Miaka 101 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Sheikh al-Shari'a Isfahani mwalimu mkubwa wa Chuo Kikuu cha Kidini cha mjini Najaf Iraq. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria katika mji wa Isfahan nchini Iran. Mwaka 1295 Hijria alielekea Najaf Iraq kwa lengo la kujiendeleza zaidi kimasomo na kufanikiwa kuhudhuria masomo na darsa za wanazuoni mahiri wa zama hizo kama Mullah Ahmad Sabzawar, Muhammad Hussein Kadhmeini, na Mirza Habibullah Rashti. Miongoni mwa wanafunzi wake ni Muhammad Taqi Khonsari, Abdul Karim Hairi na Muhammad Hussein Borujerdi. Sheil al-Shar'ia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 73 na amezikwa katika haram ya Imam Ali bin Abi Talib mjini Najaf Iraq.
Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Nikola Tesla mwanafizikia wa Yoslavia. Nikola alizaliwa mwaka 1856 na katika kipindi cha masomo yake alikuwa na mapenzi makubwa na elimu ya fizikia. Msomi huyo wa Kiyugoslavia alifanya tafiti na uvumbuzi wake mwingi katika uwanja wa nishati ya umeme na kupata mafanikio makubwa. Umeme mbadala au Altenative electricity unahesabiwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa Nikola Tesla. Mwanafikizia huyo alikipa jina lake la Tesla, kifaa kinachotumika kupimia kiwango na mtiririko wa sumaku yaani (magnetic flux).
Siku kama hii ya leo miaka 20 iliyopita Mahakama ya Rufaa ya Paris ilimhukumu kifungo na kumtoza faini mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchi hiyo, Roger Garaudy, kwa kosa eti la kukana jinai dhidi ya binadamu katika kitabu chake cha 'The Founding Myths of Israeli Politics'. Katika kitabu hicho msomi huyo Mfaransa alithibitisha kisayansi na kwa hoja madhubuti kwamba Wazayuni walishirikiana na Manazi katika Vita vya Pili vya Dunia. Vilevile amethibitisha kwa hoja na ushahidi kwamba, kwa shabaha ya kutaka kupata uungaji mkono wa kuunda dola bandia la Israel katika ardhi ya Palestina, Wazayuni walikuza na kutia chumvi kupita kiasi jinai zilizofanywa na Adolph Hitler dhidi ya Mayahudi. Katika kitabu cha 'The Founding Myths of Israeli Politics' Profesa Garaudy anasema, idadi ya Mayahudi milioni 6 inayotajwa na Wazayuni kuwa iliuawa na Wajerumani wa zama za Hitler imetiwa chumvi kupita kiasi kwani jamii ya Wayahudi katika kipindi hicho haikuwa kubwa kiasi hicho. Msomi huyo alikamatwa na kuhukumiwa kifungo nchini Ufaransa kutokana na maoni yake, suala ambalo limethibitisha urongo wa madai ya demokrasia na uhuru wa maoni nchini Ufaransa.