Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza mfululizo wa vipindi vipya vya maswali na majibu ambavyo kidogo vitatofautiana na vipindi vya maswali na majibu ambavyo tumekuwa tukivirusha hewani, vipindi ambavyo kimsingi vimekuwa vikitokana na maswali yanayoulizwa na wasikilizaji wetu moja kwa moja.
Mfumo huu mpya wa maswali na majibu utakuwa ukijibu maswali ambayo si
dharura yawe yameulizwa na wasikilizaji bali maswali ambayo kwa kawaida
huwatatiza watu wengi kuhusiana na masuala ya kidini na ambayo
yanapaswa kupatiwa majibu.
Majibu ya maswali haya yatakuwa yakitolewa kwa msingi wa mafundisho ya Thaqalain au vitu viwili vizito ambavyo ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu, Quir'ani Tukufu na Sunna za Ahlul Beit (as) ambao ni Mtume Mtukufu, Bibi Fatma na Maimamu 12. Hii ni kwa sababu muda mfupi kabla ya kuaga duniani, Mtume Mtukufu aliwasihi Waislamu washikamane na vitu viwili hivyo vizito kimaanawi ambavyo aliwahakikishia kwamba kama wangeshikamana navyo ipaswavyo basi wasingalipotea kamwe hadi Siku ya Mwisho.
Bila shaka majibu sahihi ya maswali haya yatatusaidia pakubwa katika kuainisha njia ya wokovu na saada humu duniani na huko Akhera. Hivyo bila kupoteza wakati, tunakukaribisheni wasikilizaji wapenzi tusikilize kwa pamoja na kwa makini kipindi cha kwanza katika mfululizo huu ambapo swali la kwanza tunalouliza na kulijibu ni je, kwa nini tuliumbwa?
Ni nani mbora wa kujibu swali hili muhimu isipokuwa vitu viwili hivi vizito kwa thamani, cha kwanza kikiwa ni Qur'ani Tukufu ambayo haitaifikia batili mbele yake wala nyuma yake, bali ni neno la mwisho la Mwenyezi Mungu linalotenganisha haki na batili. Hiki ndicho kitu kizito cha kwanza, amma cha pili ni Ahlul Beit wa Mtume Mtukufu (saw) ambao walilinda na kuhifadhi mafundisho na Sunna za babu yao al-Mustafa (saw).
Walilinda mafundisho na sunna hizo kutokana na upotevu, ziada au kasoro zozote na kuzieneza kati ya wanadamu ili ziwe minara ya wongofu na saada kwao na kuwakinga kutokana na giza la upotevu.
Na sisi hapa tunayarejea mafundisho yao kwa ajili ya kupata majibu shihi ya maswali yetu muhimu maishani huku tukifanyia kazi wasia na nasaha muhimu na za kudumu milele za Mtume wetu Muhammad (saw), nasaha ambazo zimenukuliwa na madhehebu yote ya Waislamu. Madhehebu hayo yamemnukuu Mtume akisema: "Hakika nimekuachieni vitu viwili vizito; Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Ahlu Beit wangu, vitu ambavyo iwapo mtashikamana navyo sawasawa basi hamtapotea kamwe baada yangu. Amenipasha habari Mwenyezi Mungu, mrehemevu na mjuzi wa mambo yote kuwa vitu viwili hivi havitatengana hadi vitakaponijia pembeni ya Hodhi. Basi tazameni mtaniwakilisha (mtaamiliana) vipi kwenye vitu hivi baada yangu."
Kama tulivyosema mwanzoni, swali muhimu la kwanza kwetu na kwa wanadamu wote humu duniani ni kwamba, je, ni kwa nini tuliumbwa?
Hebu turejeekwaThaqalain ili tupate jibu sahihi la swali hili:
Tuanze na kitabu kitakatifu cha Qur'ani ambapo tunasoma katika aya ya 3 ya Surat al-Ahqaf maneno yafuatayo:
"Hatukuziumba mbingu na ardhi wala yaliyomo baina yake ila kwa haki na kwa muda uliowekwa."
Pia amesema katika aya ya 22 ya Surat al-Jathiyah:
"Na Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa haki na ili kila nafsi ilipwe yale iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa."
Na tunayasikiliza kwa nyoyo zetu yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika aya mbili za 28 na 29 za Surat ad- Dukhan:
"Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo. Hatukuviumba ila kwa haki, lakini wengi wao hawajui."
Mwenyezi Mungu atuepushie mbali sisi na wasikilizaji wetu wote wapenzi balaa la kuwa miongoni mwa watu wasiojua. Tunaendelea kujifunza mengi kutoka kwenye Qur'ani Tukufu kwa kusoma aya ya 36 ya Suratul Qiyamah:
Nam, wapenzi wasikilizaji, amma kuhusiana na sababu ya kuumbwa kwetu humu duniani, Mwenyezi Mungu anajibu swali hili kwa lugha na maneno fasaha ya mawaidha yasiyo ya moja kwa moja kwa kusema "Je! Anafikiri binadamu kuwa ataachwa bure, (asipewe amri za Mwenyezi Mungu wala makatazo yake)?"
Jibu lililotolewa katika aya hii linafanana na lile lililotolewa katika aya 115 ya Surat al-Muminuun inayosema: "Je, mlidhani ya kwamba tumekuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?"
Sasa tunakitizama kitu cha pili kwa uzito ambayo ni maneno ya Mtume na Ahlul Beit wake (as) kuhusiana na suala hilila sababu ya kuumbwa mwanadamu. Tunasoma katika kitabu cha I'tikadaat al Imamiyyah cha Sheikh Swaduq maneno ya maimamu watoharifu waliomnukuu babu yao al-Mustafa (saw) akisema:
"Hamukuumbwa kwa ajili ya kuangamia bali muliumbwa kwa ajili ya kubakia; lakini mnahamishwa kutoka makao mamoja hadi makao mengine."
Na tunasoma katika kitabu cha Makarim al-Akh'laq cha Sheikh Tabarsi hadithi ya Mtume (saw) alipokuwa akimuhusia Ibn Masoud kwa kusema:
"Ewe Bin Masoud! Usiruhusu dunia na matamanio yake kukuchezea (kukupoteza) kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: Je, mlidhani ya kwamba tumekuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?"
Wapenzi wasikilizaji, tunasoma hivi katika kitabu cha Tuhuful Uqul an Aali Rasuul cha Allama Shu'batul Bahrani kuhusiana na kauli ya Imam Ali al-Hadi (as), Imam wa 10 wa madhehebu ya Ahlul Beit (as):
"Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuwaumba bure wanadamu, kuwaacha hivihivi bila majukumu wala kudhihirisha hekima yake kimzaha. Ni kutokana na hilo ndipo akasema: Je, mlidhani ya kwamba tumekuumbeni bure?"
Wapenzi wasikilizaji, baada ya kupitia aya na hadithi tulizotaja, tumepata jibu jumla la swali letu muhimu lililoulizwa mwanzoni ambalo linahusiana na sababu ya kuumbwa kwetu humu duniani.
Kwa maelezo hayo tunapata kufahamu kwamba vitu viliwi vizito tulivyovizungumzia mwanzoni, kwanza kabisa vinapinga fikra yoyote ya kuumbwa mwanadamu bila kuwepo sababu yoyote muhimu na kama mchezo tu bali aliumbwa kwa msingi wa haki na hekima. Pili ni kwamba tuliumbwa kwa ajili ya kuishi milele na sio kuishi kwa muda mfupi tu na kisha tuangamie.
Aya na hadithi hizi zinasisitiza wazi kwamba tuliumbwa na Mwenyezi Mungu na kwamba sote tutarejea kwake. Zinasisitiza kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kutuumba hakutuacha bure bila kutupa majukumu na malengo maalumu.
Na hapa tunajiuliza swali hili muhimu kwamba je, ni nini hekima ya kuumbwa kwetu? Na je, tutathibitisha vipi hekima hii kwa maana kuwa kuishi kwetu milele kutimie katika kivuli cha maisha bora yenye saada na yaliyo mbali na masaibu na mashaka?
Tutazungumzia na kujibu maswali haya katika kipindi kijacho cha Maswali Yetu na Majibu ya Thaqalain, ili tupate kunufaika na majibu yake katika njia ya kuelekea kwenye maisha ya kudumu milele.
Basi hadi tutakapokutana tena katika kipindi kijacho, tunakuageni wapenzi wasikilizaji kutoka hapa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kusema, kwaherini.