Jumatatu tarehe 17 Disemba 2018
Leo ni Jumatatu tarehe 9 Rabiuthani 1440 Hijria sawa na Disemba 17 mwaka 2018.
Siku kama ya leo miaka 240 iliyopita, alizaliwa Humphrey Davy mwanakemia na mwanafikizia wa Kiingereza. Katika majaribio yake ya kimaabara, msomi huyo aliweza kutenganisha elementi za Sodium, Potassium, Calcium, Barium, Magnesium na Strontium miongoni mwa elementi nyinginezo na hatua hiyo ilihesabiwa katika zama hizo kuwa mafanikio makubwa katika sayansi ya kemia. Davy mbali na kuwa mwasisi wa elimu inayojulikana kama "electrochemical", aliweza pia kuwasilisha nadharia ambayo iliitaja gesi ya Hydrojen kuwa gesi inayoweza kuzitambua asidi. Mwanakemia huyo wa Kiingereza alifariki dunia mwaka 1829 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alimu na msomi mkubwa wa sheria za Kiislamu. Ayatullah Nahavandi alibobea katika elimu ya fiqhi na usulu fiqhi, na kutokana na hali hiyo wasomi wengi wa Iraq na Iran waliweza kustafidi na elimu yake. Inafaa kufahamisha kwamba, Ayatullah Haj Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alizaliwa katika mji wa Nahavand, ulio magharibi mwa Iran na akiwa kijana alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo hususan Sheikh Murtadha Answari, ambapo kwa kipindi cha miaka 30 alijikita katika shughuli ya ufundishaji wa sheria za Kiislamu.
Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 58, Ayatullah Sayyid Haidar Hilli. Abul-Hassan Sayyid Haidar Bin Sulaiman Bin Daud Hilli Husseini, ni miongoni mwa malenga na viongozi mashuhuri wa fani hiyo katika zama hizo. Ufasaha na uwezo mkubwa wa kiimani aliokuwa nao, vilimsukuma katika kuwasifu Ahlu Baiti wa Mtume (saw) kupitia mashairi yake. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'ad-Duraru-Yatim' na 'al-Aqdul-Mufaswal.'
Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Disemba mwaka 1903, ndege ya kwanza duniani iliyokuwa ikitumia injini ya mota, ilifanikiwa kuruka na kupaa angani kwa dakika moja baada ya kufanyiwa majaribio kadhaa. Ndege hiyo ilitengenezwa na ndugu wawili walioitwa Wilbur na Orville Wrights na kufanyiwa majaribio katika jimbo la North Carolina nchini Marekani. Ndugu hao wawili walikuwa watengeneza baiskeli ambao baadaye walipatwa na shauku kubwa ya kutengeneza ndege yenye kutumia injini ya mota.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita mwili wa Mhandisi Muhammad Jawad Tundguyan, waziri wa mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejeshwa nchini Iran kutoka Iraq baada ya kupita miaka 11. Waziri Tundguyan na maafisa wengine kadhaa wa wizara hiyo walitekwa nyara na wanajeshi wavamizi wa Iraq wakati walipokuwa katika ziara ya kutembelea visima vya mafuta vya kusini mwa Iran. Waziri huyo na wenzake walitekwa nyara mwezi mmoja baada ya Iraq kuvamia ardhi ya Iran. Utawala wa Saddam wakati huo uliendelea kukanusha kutekwa nyara Mhandisi Tundguyan kwa muda fulani, lakini hatimaye ulikiri kumteka nyara waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran. Uchunguzi wa kidaktari na ushahidi uliotolewa na watu waliokuwa karibu na Waziri Muhammad Jawad Tundguyan ulithibitisha kwamba waziri huyo wa zamani wa mafuta wa Iran alikufa shahidi kutokana na kuteswa vikali na askari jeshi wa utawala wa Baath wa Iraq.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, sawa na tarehe 17 Disemba mwaka 1992 utawala wa Kizayuni wa Israel, kwa kisingizio cha kuuawa polisi wake mmoja wa mpakani, uliwabaidisha kusini mwa Lebanon viongozi 415 wa harakati ya Jihadul Islam na Hamas kutoka Palestina. Baada ya serikali ya Lebanon kupinga hatua hiyo isiyo ya kibinadamu na kukataa kuwapokea Wapalestina hao, hasira na upinzani wa ulimwengu wa Kiislamu ulilifanya Baraza la Usalama kupitisha azimio nambari 977 lililolaani hatua hiyo ya Tel Aviv na kutaka kurejeshwa Wapalestina hao waliobaidishwa nchini kwao.

Tarehe 17 Disemba miaka 8 iliyopita kijana mmoja wa Kitunisia kwa jina la Tariq Mohamed Bouazizi alijiteketeza kwa moto na kuanzisha harakati ya ukombozi wa wananchi wa nchi hiyo dhidi ya utawala wa kidikteta wa Habib Bourguiba na Zainul Abidin bin Ali uliodumu kwa kipindi cha nusu karne. Kujichoma moto kwa Bouazizi ilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Tunisia na katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.
Bouazizi ambaye alikuwa na shahada ya chuo kikuu alikuwa akiuza bidhaa za mkononi mitaani aliponyanganywa bidhaa zake na kudhalilishwa na afisa wa kike wa halmashauri ya mji na ndipo alipoamua kujiteketeza kwa moto, kitendo ambacho kiliamsha hasira za wananchi wa Tunisia na kuwa chachu ya harakati iliyohitimisha utawala wa dikteta Zainul Abidin. Dikteta huyo alikimbia nchi na kwa sasa anapewa hifadhi na watawala wa kifalme wa Saudi Arabia.