Dec 19, 2018 10:42 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 791 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 36 ya Ya-Sin. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 13 na ya 14 ambazo zinasema:

وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا أَصْحَابَ الْقَرْيَةِ إِذْ جَاءَهَا الْمُرْسَلُونَ

Na wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.

 إِذْ أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمُ اثْنَيْنِ فَكَذَّبُوهُمَا فَعَزَّزْنَا بِثَالِثٍ فَقَالُوا إِنَّا إِلَيْكُم مُّرْسَلُونَ

Tulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawaongezea nguvu kwa (mwingine) wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.

Aya tulizosoma katika darsa iliyopita zilifanya mlinganisho baina ya waumini na makafiri kuhusiana na namna walivyoyapokea mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu. Aya hizi za 13 na 14 zinaendeleza maudhui hiyo kwa kusema: Ewe Mtume! Ili kutoa ibra na mazingatio kwa washirikina wa Makka, hebu watolee mfano wa moja ya umma zilizotangulia ambayo watu wake walipelekewa Mitume kadhaa wa kuwafikishia uongofu, lakini kutokana inadi na ukaidi wao, hawakuusadiki wito wa Mitume wao wakasimama kuwapinga Mitume wote hao. Ni kama kwamba hawakuwa tayari kukubali kuwa Mwenyezi Mungu amemtuma kwa watu mtu ambaye ni Mtume. Walikuwa wakidhani kwamba Allah SW amewaacha kama walivyo na kwa hivyo inajuzu wao kufanya lolote lile watakalo kwa mujibu wa ufahamu wao. Kwa sababu hiyo, Mitume wao wakawa wanawasisitizia nukta hii, kwamba haya tunayokwambieni hayatokani na sisi wenyewe ila tumetumwa na Mwenyezi Mungu tukufikishieni wito wake wa uongofu. Sisi ni Mitume na wajumbe tu na hatutaki chochote kile kwa ajili yetu wenyewe. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kuyasoma yaliyojiri katika kaumu zilizotangulia na kujua hatima ya watu wa kaumu hizo kunatoa mwanga wa kuongozea njia kwa kaumu zinazofuatia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume walikuwa wakiwaendea watu kuwafikishia ujumbe wa risala zao na si kuwaongojea watu wawaendee wao. Aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kuna wakati Mitume kadhaa walikuwa wakitumwa kwa pamoja kwenda kuwafikishia wito wa uongofu watu wa kaumu yao.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 15, 16 na 17 ambazo zinasema:

قَالُوا مَا أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَمَا أَنزَلَ الرَّحْمَـٰنُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَكْذِبُونَ

Wakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.

قَالُوا رَبُّنَا يَعْلَمُ إِنَّا إِلَيْكُمْ لَمُرْسَلُونَ

Wakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.

وَمَا عَلَيْنَا إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

Wala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.

Makafiri na wakanushaji huwa hawana hoja za mantiki za kukabiliana na wito wa Mitume isipokuwa kusema: kwani nyinyi mna tofauti gani na sisi? Nyinyi pia ni watu kama sisi; na kama Mungu angetaka kumtuma mtu wa kutuletea uongofu ingebidi awe ni malaika mtukufu na si binadamu aliye sawa na sisi. Kwa maneno mengine, makafiri walitaka kusema: sisi hatuwezi kumtii mtu aliye sawa na sisi; Mtume wa Mungu lazima awe kiumbe aliyetukuka na aliye tofauti kabisa na sisi. Ilhali hata kama malaika angelitumwa kuwafikishia uongofu wanadamu, watu haohao wangesema: maamrisho anayotupa kuhusu vilaji na vinywaji na mahusiano baina ya mwanamke na mwanamme yeye mwenyewe hayatekelezi isipokuwa anatuamrisha sisi tu tufanye. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu amemtuma kuwafikishia watu uongofu mwanadamu aliye sawa na wao, ambaye kwa upande wa hali ya kimaada na ya mahitaji ya kibinadamu yuko sawa na wao. Isitoshe, Yeye Allah SW amemwajibisha Bwana Mtume SAW awe wa mwanzo kutekeleza maamrisho yake ili watu wasije wakadhani kwamba yale anayowaamrisha ni mambo ambayo hayafanyiki wala hayatekelezeki. Kama washirikina wanakubali kwamba kuna Mungu basi kwa hekima na rehma zake Mungu huyo inapasa amtume mtu miongoni mwa wanadamu wa kuwaelekeza viumbe hao kwenye uongofu na si kuwaacha kama walivyo. Lakini wao washirikina walikuwa wakimtaja Mwenyezi Mungu kwa sifa moja tu ya Ar-Rahman ili wapate kusema, Mungu aliye na huruma na urehemevu hatuwekei sisi sharia ngumu, ila hutuacha kama tulivyo tufanye chochote kile tutakacho! Jibu la Mitume kwa watu hao lilikuwa ni kwamba, Mungu huyohuyo aliyekuumbeni na mnayemwamini ndiye aliyetutuma sisi; na sisi hatuna jukumu jengine isipokuwa kukufikishieni maamrisho yake. Kama sisi tungekuwa waongo lazima Mwenyezi Mungu angetufedhehesha wala asingemwacha mtu aseme uongo wa kujitangaza kuwa ni Mtume wake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba baadhi ya watu wanadhani kuwa maana ya rehma za Allah ni kuachwa mtu afanye lolote lile bila kuwekewa kiwango na mipaka maalumu. Ilhali hata katika mfumo wa familia, ambapo baba na mama ni madhihirisho ya huruma kwa mtoto wao, huwa hawamwachi mtoto kama alivyo afanya vyovyote vile atakavyo. Ila humpeleka skuli apate mafunzo na malezi na kumhimiza kila mara afanye kazi zake za masomo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa wanachozingatia Mitume ni kutekeleza wajibu na jukumu lao la kuwaelimisha na kuwabainishia haki watu bila kujipa hakikisho la kupatikana tija. Ijapokuwa watu wengi hawakuwa, na hadi sasa hawaiamini haki, lakini sifa ya Mitume ni kutekeleza jukumu lao kikamilifu hata kama ni kwa gharama ya kutoa mhanga maisha yao.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 18 na 19 ambazo zinasema:

قَالُوا إِنَّا تَطَيَّرْنَا بِكُمْ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهُوا لَنَرْجُمَنَّكُمْ وَلَيَمَسَّنَّكُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ

Wakasema: Hakika sisi tunapata mkosi kwa ajili yenu. Kama hamtakoma, basi hakika tutakupigeni mawe, na itakufikeni adhabu chungu kutoka kwetu.

قَالُوا طَائِرُكُم مَّعَكُمْ ۚ أَئِن ذُكِّرْتُم ۚ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ مُّسْرِفُونَ

Wakasema: Mkosi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizopita kwa kuashiria mantiki na hoja za wapinzani wa haki na kueleza kwamba: wao badala ya kuyasikiliza maneno ya Mitume na kuyazingatia mafundisho yao ya kiutu na kiakhlaqi waliamua kutumia lugha ya vitisho na ya kutaka kuwadunisha Manabii hao kwa kuwaambia: kuwepo kwenu nyinyi katika jamii yetu ni nuhusi na kunatuletea mikosi. Kwa hivyo ama achaneni na mnayoyasema au uhameni mji wetu au tutakufanyieni maudhi ya namna mbaya kabisa ya hata kukuueni! Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kukadhibisha, kudunisha na kutoa vitisho ndio hoja na mantiki za wapinzani mbele ya wito wa haki wa Mitume. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kuamini khurafa na uzushi kama wa uaguzi na mwengineo ni katika desturi za kijahilia. Mtu siye na mantiki hutegemea mambo ya khurafa na uzushi. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kukufuru na kufanya madhambi huwa sababu ya kuhasirika mtu hata kama kidhahiri atajiona yuko kwenye raha na uneemevu. Vilevile aya hizi zinatufunza kuwa israfu haiko katika matumizi tu, lakini kila aina ya upindukiaji mpaka na ukaidi mbele ya haki ni kukivuka kiwango na kipimo cha utu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 791 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags